HII NDIYO MISINGI YA SALA KWA KILA MWAMINI
Ndugu wapendwa, karibuni sana katika tafakari ya neno la Mungu dominika hii ya leo. Dhamira inayotuongoza leo ni sala. Tunaambiwa kuwa sala kama upendo haina mahesabu. Huwa hatuulizi tupende mara ngapi. Hivyo hatupaswi kuuliza tusali mara ngapi. Yesu anasema tusali daima. Maisha yetu hayana budi kuwa maisha ya sala. Mt. Augustino anasema msingi wa sala ni tamaa. Kama tamaa ya Mungu ikiwa hai, vivyo hivyo na hamu ya sala itakuwa hai.
Padre J. Healey katika kitabu ‘Hadithi za Kiafrika’ uk. 87 anatushirikisha juu ya sala hii ya kiafrika: Ee Bwana, uwe kwetu mwenzi wa furaha na shangwe, uwawezeshe vijana wapate nguvu, na mtu mzima atunze nguvu zake. Umwezeshe mwenye mimba kujifungua, na mwananke aliyejifungua amnyonyeshe mtoto wake. Umwezeshe mgeni kufika kwenye ukomo wa safari yake, wale wanaobakia waishi salama nyumbani mwao. Uyawezeshe makundi ya mifugo kwenda kwenye malisho na kurejea yakiwa yameshiba. Ee Bwana, uwe mwenzi wa mavuno na mitamba. Uweze kuwa mwenzi wa ukarabati na wa afya njema. Amina.
Hakika hapa tunaona nafasi au uwezo wa mwanadamu kumtambua muumbaji, yaani Mungu na uwezo wa kuendelea kutambua ukuu huo wa Mungu. Yote ni mali yake Bwana na sala inatoa ombi ili vyote viendelee kuwa na uzima. Hata mahali fulani katika injili tunaona wafuasi wakimwomba Yesu awafundishe kusali. Wanatambua ukuu wa Mungu juu ya hali zao na vile walivyo navyo.
Hata kutoka Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika kipengele ‘Ufunuo’ tunasoma kuwa Mungu, mwanzo na mwisho wa yote, aweza kufahamika kwetu kwa njia ya viumbe tukitumia mwanga wa akili ya mwanadamu. Kwamba mwanadamu anaweza kumfahamu Mungu na kuishi kadiri ya amri na maagizo yake na mwisho kumfikia yeye.
Mtakatifu Clement wa Alexandria Misri anasema kuwa sala ni mazungumzo na Mungu.
Hii siri ya hamu ya Mungu inahusisha kumbukumbu. Tunamshukuru Bwana Wetu Yesu Kristo kwani ni mfano kamili wa namna ya kusali – asubuhi, mchana, jioni, makesha – muda wote. Yesu alishiriki kikamilifu maisha ya sala ya Wayahudi. Mt. Saturnius anasema mkristo hawezi kuishi bila jumapili ambapo fumbo la ekaristi takatifu huadhimishwa. Kumbuka kuwa mkristo huishi kwa ekaristi na ekaristi ni kwa ajili ya mkristo. Alisema maneno haya alipokuwa mbele ya kiti cha hukumu pamoja na mashahidi wenzake akishutumiwa kwa kushiriki ibada siku ya jumapili.
Katika somo la kwanza tunaona kuwa kwa njia ya maombi, neema na nguvu ya Mungu hutufikia – Musa. Udumifu wa sala kwa njia ya Musa unamsaidia Yoshua kushinda vita dhidi ya Waameleki.
Mambo matano (5) yahitajika au hufanya msingi wa sala;
- Hitaji la imani – James Taharey anasema Mungu hasikilizi sala ila matumaini yetu. Ukisali kuomba mvua, basi ukitoka nyumbani usisahau mwavuli.
- Tunaposali kwa Mungu kuomba basi nasi tuinue mikono yetu – Mt. 17:20 … . Ili kung’oa mlima anasema Sr. Ruth Fox tunahitaji chepe. Halafu hufuata nia ya kutumia hiyo chepe na imani pia kuwa Mungu atasaidia katika kuondoa kazi ngumu iliyo mbele yako. Kusali kama vile kila kitu humtegemea Mungu na kufanya kazi kama vile kila kitu hutegemea mwanadamu. Mfano wa bondia hapo chini unaingia hapa. Hitaji la kujituma.
- Sala hailengi kumfunga Mungu miguu. Hitaji la kusali kwa heshima.
- Sala haimlazimishi Mungu, bali yatafuta huruma yake. Hitaji la udumifu. Tunaambiwa kuwa Mt. Monika aliomba uongofu wa mwanawe Mt. Augostino kwa miaka 30 kabla ya kufanikiwa.
- Kuacha mapenzi yetu bali mapenzi ya Mungu yatimizwe. Hitaji la unyenyekevu – yule mama mjane katika injili.
Mtu wa imani anajua wazi kuwa hakuna mazingira ya hovyo (hopeless situations). Ila kuna watu waliojijengea mazingira ya hovyo (hopeless situations) au magumu juu ya hali zao. Mwanamke katika somo la injili atualika daima tusijenge mazingira ya hovyo ya hali zetu hata kama ni magumu kiasi gani na kwamba yawezekana kuepuka hali hizo. Katika mazingira na tamaduni za Waisraeli mwanamke mjane alikuwa hana haki yo yote. Huyu anadhihirisha kuwa haridhiki na hizo hali za hovyo. Anaomba mpaka anapata haki yake.
Ndiyo hali iliyowapata wakristo wa kwanza baada ya Kupaa Bwana. Matumaini yao ya wokovu yalipotea kabisa baada ya kuharibiwa hekalu la Yerusalemu mwaka 70 B.K. Hata hivyo hawakukata tamaa na juhudi zao zisizo kikomo zinawapatia ushindi dhidi ya udhalimu wo wote uliokuwa mbele yao. Injili inaanza vizuri – salini daima na bila kukata tamaa. Sala hueleza matumaini yetu na hulisha imani yetu. Tumwombe Mungu atuimarishe katika imani yetu, atujalie uthabiti katika matumaini na kutufanya imara katika sala.
Somo la pili latupa changamoto na kutukumbusha kuwa sote ni wanafunzi wa kudumu wa Neno na sote ni walimu wa Neno. Katika somo hili tunaona kuwa neno la Mungu lililo hai ni Yesu Kristo mwenyewe. Huhuisha maisha ya mwamini. Injili inamalizika kwa kusema lakini atakapokuja Mwana wa mtu, ataikuta imani duniani?
- Ina maana kwamba kama Mungu atataka kutimiza maombi yako, je atakukuta imara katika maombi au umekata tamaa? Bado unaamini? Kama Musa katika somo la kwanza?
- Je Bwana akija kama hakimu, atakukuta bado mwaminifu? Ukisali na kukesha?
Tumsifu Yesu Kristo.
Na Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.
Comments
Post a Comment