Haya hapa mafundisho ya uongo tunayoaminishwa wakatoliki
LAKINI jamani, sisi nasi tu watu kamili wala hakuna aliyelaaniwa kati yetu.
Sikiliza orodha hii ya mambo yanayofundishwa kuwa ishara za mtu aliyelaaniwa.
Sikiliza uniambie atapona nani
katika orodha hii: magonjwa ya
kifafa, kisukari, moyo, BP, saratani, ukoma, ukichaa, upofu wa macho, asthma,
ukimwi, kifua kikuu; hali za ugumba wa kutozaa, utasa, ufakara, umaskini,
kuonewa na kunyanyaswa; vifo vya ghafla, vifo vya ajali kama magari, pikipiki
na baskeli; tabia za ulevi, kukojoa kitandani, kupenda ushirikina (uchawi),
kuoa wanawake wengi, kuoa na kuacha, uzinzi au uasherati, uvivu au uzembe;
mikasa ya kuibiwa, kuunguliwa nyumba au vitu moto, kuumwa na mbwa, kuumwa na
nyoka; hali za kutoolewa, kufiwa na waume au wake na kuachika.
Shida zingine katika orodha
hiyo ni: kutopata kazi, kutofikia daraja la upadre au utawa, kutomaliza mambo
fulani fulani, kutopendwa, kusingiziwa mambo, mafarakano katika familia au
ukoo, fedha kutokukaa, kutofunga ndoa katika familia, kukataliwa, kuzaa watoto
wafu, kuzaa watoto nje ya ndoa, kutopenda kujihusisha na wokovu;
Kudhulumiwa, kutokuwa na
makazi, kujiua au kuua, kufa kwa mifugo, kupelekwa jela au mahakamani, kuliwa
na wanyama wakali, kuzaa kwa kufanyiwa upasuaji, kutopandishwa cheo,
kutoaminiwa na kutegemewa, kunyang’anywa mke, kununua vitu vilivyoharibika n.k.. Je, umepona hapo?
Halafu katika kitabu kiitwacho Tufanye
Nini Kabla ya Kuanza Mafungo? Moyo Mtakatifu wa Yesu na Mapambano Dhidi ya
Ushirikina, Uchawi – Mazindiko - Ramli na Maruhani cha Pd. H.J. Mambwe, imeandikwa kwamba kuna mikoa hapa Tanzania imelaaniwa.
Unashtuka? Usishtuke, inasomeka hivi:
“Laana ya kitaifa inafanya kazi kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini katika
taifa husika, kuanzia ngazi ya – Kata, Wilaya, Majimbo, Mikoa na Taifa.
Inategemea na agano lilofanywa na watu au viongozi husika na katika jamii
husika, kwa wakati uliopo au uliopita. Hata hivyo, zipo laana zenye kutawala
watu wa jamii fulani zaidi. Mfano, ukitazama kwa makini ipo mikoa inayoongoza
kwa vitendo vya uchawi na ushirkina.
Maagano yanayosimama katika mikoa hiyo au jamii hiyo na watu wa eneo hilo
ni pamoja na uasherati na uzinzi, ombaomba, kutoa wasichana wa kazi za ndani
(house girls), kutoa watu wa kufanya biashara za mikononi na katika mazingira
magumu na pia watu wake hupendelea kujinyonga.
Haya na mengine mengi ukiyafuatilia utagundua ipo mikataba mbalimbali
iliyowekwa na viongozi au watawala wa jadi waliotangulia katika jamii husika
kwa ulimwengu wa giza, na kusababisha roho hiyo kuendelea na kurithiwa kutoka
vizazi hadi vizazi kwa jamii husika” (uk. 27-28).
Hebu sasa tujiulize, maneno
haya kweli ni ya Kikristo? Hivi kama si ya kuwadhalilisha Wakristo ni nini?
Mikoa iliyolaaniwa na nchi zilizolaaniwa ni katika bara la Afrika, Asia au
Marekani na Ulaya pia? Hivi kweli mambo kama haya unaweza kuthubutu
kuwafundisha Wakatoliki wa Ulaya na Marekani pia?
Hivi Baba Mtakatifu na
Cantalamesa wanaweza kupokea mawazo ya kipuuzi kama haya? Karismatiki
aliyoiruhusu Baba Mtakatifu ndiyo yenye kufundisha mambo kama haya kati ya
wanadamu? Thubutu yake, siyo. Haya yetu hapa hapa Tanzania!
Basi, kumbe ukiaminishwa mambo
ya laana, lazima utaniuliza, “Nifanye nini kwa vile nimelaaniwa?” au “Tufanye
nini kwa vile kata, wilaya, jimbo au taifa letu limelaaniwa?” Hapo ndipo
nitakapokuja na upotoshaji mwingine. Nitakuambia eti uvunje mti wa ukoo au mti
wa familia. Aidha nitakwambia taifa lifanye maombi livunje laana yake.
Wapi na wapi! Kama jambo la
laana ya ukoo au familia lingelikuwa kweli angepona nani? Au taifa gani
lingepona? Kwa hilo hata Yesu asingelikuwa mtakatifu, maana babu yake Daudi
alikuwa mzinzi mkubwa aliyemuua Uria kwa shauri la mkewe na Sulemani alioa
wanawake mia saba na kuwa na nyumba ndogo ndogo mia tatu (rej. 1Fal 10:1-3).
Hapo Yesu mjukuu wao
asingeliweza kuishi useja, hata kidogo. Kwa kuwa fundisho la laana halina
mashiko, ndiyo maana hatusikii Yesu eti akivunja mti wa ukoo au kulizungumzia
jambo hilo katika Agano Jipya.
Kumbe, tuliachilieni mbali
fundisho la laana. Kwa hakika hili ni fundisho linalotudhalilisha sana
Waafrika. Waliokuwa wakituchukia walitumia sana mafundisho ya laana ili
tutawalike. Zamani, tulifikiriwa kuwa manyani makubwa (chimpazee) hata huko
Afrika ya Kusini, Dutch Reformed Church lilikuwa linawabatiza Waafrika kwa
sharti, wakisema, “Kama huyu ni mtu, nambatiza kwa jina la Baba, na la Mwana,
na la Roho Mtakatifu”.
Lakini enzi hizo zimepita,
tusiseme tena wenyewe kwamba tumelaaniwa. Tuchange karata zetu vyema, tuishi
vyema.
Matatizo, magonjwa, vifo na
dhiki ni mambo ya kawaida ulimwenguni pote (rej. YbS 40:1-11). Tusiyachukulie
kama laana za koo zetu, makabila yetu au mataifa yetu. Tungeweza kuyachambua
matatizo yetu kisayansi na kisiasa. Sijui mnaiona aibu iliyopo? Hivi ajira,
inapatikana kwa kuvunja miti ya familia na ukoo au kuadhimisha misa ya
kufunguliwa? Kwanza ni misa gani hiyo?
Hivi wasomi wetu wanakubali
kwamba ajira inapatikana kwa kuombeana? Hivi umaskini na ufukara wetu
unasababishwa na laana iliyopo katika familia, koo zetu, mikoa yetu au taifa
letu?
Msinitake nicheke. Kweli
tumefikia kiwango cha chini cha umbumbumbu hivi? Hivi hatuwezi hata kujua
zinavyotengenezwa ajira katika nchi?
Hivi hatuelewi wanachofanya
Wajapani, Wachina, Wamerakani na Wazungu? Wao wanapotengeneza ajira kati yetu
hatuoni? Wanapochukua rasilimali zetu hatuoni? Ndiyo suluhisho liwe kwenda
kuomba makanisani na kuvunja miti ya familia na ukoo?
Basi, kwa aibu yetu kuna
maelezo mawili tunayonadishiwa. Mosi, kwenye vyuo vyetu vikuu majalimu
yanafundisha kwa utaalamu somo la uchumi na kujaribu kufafanua sababu za
kukosekana ajira na kutamalaki kwa umaskini na ufukara.
Pili, kuna wanaojiita
Wakatoliki wanaopita huko na huko wakiporomosha usomi na kusema kukosekana kwa
ajira na kutamalaki kwa ufukara na umaskini sababu yake ni laana tu na dawa
yake ni rahisi tu – kuombeana na kukemea laana hizo zilizomo katika familia na
koo zetu. Nani wanasema ukweli hapo? Lazima kundi moja liwe linasema uongo,
wanazuoni au wahubiri holela? Amueni.
Mimi wala siko njiapanda. Huo
msimamo wa pili, mimi nauonea haya sana, natamani kuuficha hata uso wangu. Huo
si msimamo wa watu katika karne hii ya ishirini na moja, karne ya sayansi na
teknolojia. Aidha si msimamo wa Kanisa makini kama Kanisa Katoliki. Ni msimamo
wa watu wa zamani kabisa. Ni msimamo wa enzi za ujima!
Kumbe mtu aliyekubalishwa uongo
wa kwamba amelaaniwa anaweza kuingizwa kuingizwa katika ushauri na sala ya
kitoto kama ifuatayo:
“Fanya maombi na ukiri, ukitamka kwa kinywa chako. Mfano: Ewe laana ya
ufukara ninakutaa kwa jina la Utatu Mtakatifu ondoka kwangu. Laana ya magonjwa
ondoka kwangu. Laana ya kutangatanga ondoka kwangu. Laana ya ukahaba ondoka
kwangu. Laana ya wizi ondoka kwangu. Laana ya fitina, chuki, uongo, wivu,
usengenyaji, uchonganishi, ushirikina, ondoka kwangu. Laana ya kutaka ukubwa
kwa njia ya ushirikina ondoka kwangu.
Laana ya kukata tamaa, kutoamini, kutokuwa na matumaini ondoka kwangu.
Laana ya maneno niliyojinenea au niliyonenewa na wahenga, babu na bibi na
wazazi wangu baba na mama ondoka kwangu.
Kataa nafasi ya wanadamu walio hai na waliokufa kuishi ndani yako. Nafasi
za mizimu. Nafasi za wachawi ziambie zikuache kwa nguvu ya Utatu Mtakatifu na
kwa maombezi ya Mama Maria.
Angusha ngome zote ziletazo balaa
katika maisha yako. Ngome ya mawazo na kila kinachojiinua, kinyume na mapenzi
ya Mungu. Jitangazie kuwekwa huru, na uanze kumshukuru Mungu Baba, Mwana na
Roho Mtakatifu kwa maombezi ya Mama Bikira Maria” (Tufanye Nini
Kabla ya Kuanza Mafungo uk. 31).
Hebu niwaulizeni ndugu zanguni,
hivi haya kweli ni mafundisho na sala katika Kanisa Katoliki? Utatu Mtakatifu
umetajwatajwa mahali ambapo hapana mafundisho ya Kikatoliki kabisa.
Aidha Mama Maria ametajwa
mahali ambapo hapana mafundisho ya Kikatoliki. Kanisa Katoliki linatangaza
kuzimu kumefungwa na Bwana Yesu na badala yake kufungua hali tatu tu: mbinguni,
toharani na motoni. Sasa ni Wakatoliki gani hawa wanaoamini tena habari za
kuzimu? Semeni, msiogope. Semeni, Kanisa lipone.
Na Padri Titus Amigu
Ahsante Baba natamani niendee kupata mafundisho halisi ya kanisa nitayapata wapi kwa njia ya mtandao
ReplyDelete