TAFITI BINAFSI: HATUA MUHIMU YA KURITHISHA MALEZI BORA.
Kila
mwanadamu ana sauti ya ndani ambayo humpa taarifa juu ya mwenendo wake. Taarifa
hii ambayo twaweza kuiita “mazungumzo binafsi” (self-talk) kwa
kiasi kikubwa huwa ya msaada endapo mtu atakuwa na muda wa kupalilia taarifa au
mitazamo hii ya ndani iwe chanya.
Malezi bora
ambayo pia yanafaa kuwashirikisha
wengine lazima yaanzie na kujiamini
kwa mtoaji , kuwa yeye mwenyewe anaamini atakayotoa ni sahihi. SAUTI HIZI NI
LAZIMA ZISIKIKE NDANI MWETU ILI KUTOA MALEZI BORA.
MIMI NDIO MABADILIKO
YENYEWE:
Upendo
huanzia nyumbani. Huwezi kutoa usicho nacho. Mzazi ni lazima ajiamini kuwa jinsi
anavyoishi, maadili aliyonayo ni safi na bora, ndipo itakuwa rahisi kwake
kumfundisha mtoto hayo anayoamini kuwa bora. Ni rahisi sana kuwaelekeza wengine
mema kama sisi wenyewe ni wema. Ni kwa kutojua tunakosea mara nyingi
tunaposubiri kupata sifa za mtu kioo katika jamii [model] ndipo eti tuwalee watoto wetu kadri ya sifa za mtu huyo.
MIMI NI WA MUHIMU:
Tunaposahau
umuhimu wetu mara nyingi tunajikuta tukifanya vitu vinavyopingana na jinsi
tulivyo. Sisi sote ni wa muhimu kwa jinsi tulivyoumbwa na Mungu. Kwa mantiki
hii kwa nini usiwe kielelezo cha ubora unamtafuta mtu mwingine ili uige kwake?.
Ni wangapi
tunajijua kuwa tuna sura nzuri, sauti nzuri, tabia nzuri?, kinyume chake
tunapoteza muda kutafuta tabia njema kwa fulani. Nasema hivi, RAHA
JIPE MWENYEWE! lazima utafute mazuri ndani yako mwenyewe, ukisubiri
hadi wakuambie una maadili mema ni siku ya
maziko yako kwa taarifa yako ndipo watasoma wasifu wako, huko kuzimu unaenda
kutoa malezi gani, utakuwa umechelewa.
Siku moja
niliuliza kikundi kimoja, nani mwenye
tabia nzuri hapa anyooshe kidole?. Nilishangazwa na umati ule kwa jinsi
walivyokaa kimya bila jibu. Nikawahoji tena kwa nini hamnyooshi vidole
nikifikiri labda wote walikuwa wameungua vidole walau hata niwaambie wanyooshe
hata miguu. Wakasema, BABA PADRI HUWEZI KUJUA TABIA YAKO MPAKA WENGINE
WAKUELEZE. HAAA! Ni shida. Hawakukosea sana kwani ni kweli zipo tabia huwezi kuzijua
wewe wengine wanajua, ila ni zote?. Tuanze kufanyia kazi zile tabia njema zilizomo ndani mwetu.
“MCHAWI” NI MTAZAMO WAKO:
Neno “mchawi”
hapa lieleweke kuwa ni bahati mbaya, jambo lolote baya, chanzo cha matatizo au kutokufanikiwa.
Hivi mwaikumbuka ile hadithi ya BABU NA KIOO? tukumbushane kwa wale
waliosahau.
Babu mmoja
wa kijijini aliamua kwenda zake mjini. Alipofika katika kukaa kwake siku moja
aliona kioo akajiangalia na bila kujua alisema “ Haa! hii ni picha nzuri ya Baba yangu”. Akaamua kuinunua ile
picha(kioo). Akiwa njiani alikumbuka kuwa mke wake alikuwa hampendi baba yake, akanuia
moyoni kuwa ni lazima aifiche ile picha(kioo) awe anaangalia tu kwa muda. Asubuhi
moja baada ya kuondoka, mke wake alienda kuangalia ni nini kile ambacho mme
wake alikuwa akikitazama mara kwa mara. Alipoenda akaangalia na kusema “ Kwa hiyo huyu mchawi mbaya hivi ndio mume
wangu anamwangalia kila mara, kweli mjinga huyu!” (meseji senti).
Ni muhimu
kujijua upoje. Watu wengi wana picha mbaya yao wenyewe, ya familia zao, bila
kujijua. Jiulize mwenyewe nini kizuri ulicho nacho? na hapo utaweza
kushirikisha wengine.
Mtazamo wa
jinsi tulivyo ndio utakaotusaidia kuwalea watoto na vijana wetu kwani tunaamini
katika yale yaliyopo ndani mwetu yanayotusaidia. Mwandishi THICH NHAT HANH anasema “…..huhitaji kukubaliwa na wengine. Jikubali
mwenyewe”.
Tujikubali
kuwa tuna maadili mema ndipo itakuwa rahisi kuwapa wengine ushauri mzuri kwani
unalowashauri wanaliona kwako. Tujitafiti tuna mazuri gani ili iwe rahisi
kuwapa wengine.
Padri SAMUEL KALISTI MVATI
(PAROKIA
YA NDUNGU)
JIMBO KATOLIKI SAME.
Comments
Post a Comment