Zakayo, shuka upesi
JACK Higgens ni mwandishi wa riwaya ‘The Eagle Has Landed’ –
‘Tai Ametua’ – aliulizwa ni kitu gani alipendelea kukijua au kukifahamu
alipokuwa bado kijana. Jibu likawa, laiti ningejua kwamba ukifika juu, hakuna
lo lote pale.
Naye mwandishi R. H. Benson anasema
kuwa – ukuu wa maisha ya mtu haupo katika sifa zake mbalimbali za nje bali
katika majitoleo na sadaka zake.
Ndugu wapendwa, tunaona katika somo
letu la Injili kuwa katika watu waliokuwa na mafanikio katika mazingira ya
wakati wake ni huyu Zakayo ambaye leo tunasikia habari yake katika Injili Takatifu.
Kama mtoza ushuru alikuwa kibaraka wa watawala wapagani Warumi. Watoza ushuru
walifanya kazi kwa niaba ya hawa watawala. Kwa hiyo walichukiwa kama vibaraka
wa wapagani Warumi ambao hawakupendwa na Wayahudi na pia walichukiwa kwa kuwa
kodi ilichukiwa na wenyeji.
Mbele ya wenyeji walikuwa ni watenda
dhambi. Huyu Zakayo alikuwa mtoza ushuru mkuu wa mji wa Yeriko. Kwa kawaida
utawala uliweka kiwango cha kodi cha kutoa kwa mwaka lakini mtoza ushuru mkuu
alikuwa na uwezo wa kuongeza kiwango ili abaki na kiasi kikubwa.
Kiuchumi na kijamii alikuwa na hali
nzuri sana. Ila mbele ya watu wake alikuwa mtenda dhambi mkubwa. Huyu alisikia
kuwa Yesu anapita mtaani kwao na alipenda kumwona. Huyu alivutwa na Yesu. Kwa
kuwa alikuwa hapendwi na watu, ni mtu tajiri na maarufu alitafuta namna ya
kumwona Yesu bila kuonekana na watu anaowatesa kwa kuwadai kodi. Aliazimia
kupanda juu mtini na kujificha.
Hata hivyo halikuwa chaguo zuri
kwani kwa hadhi yake kupanda mtini kulimshushia hadhi zaidi. Yeye hakujali hayo
ila kumwona tu Yesu. Hata hivyo Yesu alimwona na kumwita ashuke chini na kutaka
kwenda nyumbani kwake. Na huo ukawa ndio wokovu wake.
Huu ukawa mwanzo mpya wa maisha
yake. Ungamo la hali yake linamfanya ampate Yesu. Wengi wetu hatufikii hali hii
ya ungamo au kujitambua na hivyo inakuwa vigumu kufanya mabadiliko. Zakayo
ambaye alihukumiwa kuwa mdhambi anasema nusu ya mali yangu nawapa maskini na
kama nimenyang’anya mtu kwa hila nitarudisha mara nne.
Huyu Zakayo anafanya sikitiko juu ya
dhambi zake na anaweka nia ya kujisahihisha. Anakiri na kukubali ubaya
aliotenda na anaweka nia ya kutotaka kufanya tena ule udhalimu.
Ndugu zangu, kama Zakayo hatuna budi
kujitafakari sana juu ya hali ya maisha yetu ya kimwili, kiroho, kijamii n.k. Baada
ya kusikia sehemu hii ya Injili hatuna budi kuangalia na kuchunguza mazingira
ya kazi zetu na wajibu zetu mbalimbali. Ni nini tija yake? Mbele ya Mungu, watu
na jamii inatazamwaje? Ipo hatari ya kuzama katika mahangaiko au majukumu yetu
ya maisha na kutotambua watu wanasemaje au ni nini faida yake kwa jamii.
Ni yapi matokeo ya kazi tuzifanyazo?
Hivi kazi yangu ni ipi? Kuna falsafa moja ya kazi inasema ‘kazi yako ni jina
lako’. Je kazi yako au wajibu wako unatazamwaje na jamii? Wale unaowahudumia
wanakuitaje au wanatambua hicho unachofanya?
Je uadilifu wetu katika kutimiza
majukumu mbalimbali ukoje? Imekuwa lugha ya kawaida siku hizi kusikia habari
juu ya ufisadi, rushwa, uvivu, ujambazi, wafanyakazi hewa, wanafunzi hewa,
asilimia kumi, kupiga dili, mauaji ya albino na mambo kama hayo? Je sote au
wenye dhamana ya uongozi tumekuwa wote kina Zakayo? Ni nani wanaofanya hayo
yasiyofaa kwenye jamii? Ni wale? Wengine? Wao? Sisi je au mimi je nikoje? Je
mimi, wewe, sisi ni Zakayo au Myahudi au Mrumi mtawala?
Jamii yetu inahangaika sana kujiweka
vizuri kiuchumi, kimaadili, kiutawala n.k. Hakika inahitajika tafakari ya
binafsi na hata ya kijamii. Tukoje? Tuko vizuri? Hatuna budi kuwa na ujasiri
kama wa Zakayo. Pamoja na ukuu wake na hali yake katika jamii aliamua
kujitokeza na Yesu akamwona na kumwita. Kwa lugha ya siku hizi alijiongeza na
Yesu akamwona na kumwita.
Hatuna budi sisi au wale wenye
afadhali au waliokomaa kiimani wakaweza kuona wenye mahangaiko, kutambua waliko
au wanayofanya na kunyoosha mkono wetu kuwaita. Hatuna budi kuwaona kama Yesu
alivyomuona Zakayo juu mtini na kuita. Huu ndiyo uongofu unaohitajika kama
alivyofanya Zakayo.
Mtu mmoja alinunua gazeti na kwa
bahati mbaya katika ukurasa wa matangazo ya vifo uliandikwa wasifu wake ukiwa
na kichwa ‘mfalme wa mabomu ya kutega ardhini afariki dunia’. Pamoja na
kusikitika kwa taarifa hiyo iliyokosewa lakini akawa na hamu ya kujua mtazamo
wa watu juu yake baada ya maisha yake hapa duniani. Kwa msisitizo taarifa
iliandika na kusisitiza na kumtaja tajiri huyo kama ‘mfanya biashara wa kifo’.
Ni kweli alivumbua mabomu ya kutega
ardhini na alipata utajiri mkubwa kwa kuuza mabomu hayo. Kilichomshtua na
kujiuliza ni kuwa ni kweli alidhamiria kuwa mfanya biashara wa kifo? Kwa
changamoto hiyo akapata kuongoka kutoka kuwa muuaji na kuwa mtu wa amani.
Akaelekeza fedha zake, nguvu zake na mali yake katika kutafuta amani na
kuboresha maisha ya watu. Leo hii anakumbukwa si kama mfanya biashara wa kifo
bali mtu wa amani na huyu ndiye mwanzilishi wa NOBEL PEACE PRIZE – ALFRED
NOBEL.
Huu ndiyo uongofu unaohitajika kwa
kila mmoja wetu. Leo tunaalikwa kufanya tafakari ya kazi zetu, wajibu wetu na
majukumu yetu mbalimbali na kuona kama yana tija inayotakiwa. Kama tuonavyo
hapo juu mwandishi R. H. Benson anavyosema ukuu wa maisha ya mtu haupo katika
sifa zake mbalimbali za nje bali katika majitoleo na sadaka zake. Nasi pia
hatuna budi kutoa sadaka za maisha yetu ili wengine wapate kuokoka.
Injili inaweka wazi tena leo “Mwana
wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea”.
Tumsifu Yesu Kristo.
Comments
Post a Comment