Ushirikina chanzo kikuu cha mauaji Kanda ya Ziwa - Askofu Kasalla

USHIRIKINA umetajwa kuwa sababu kubwa ya kukithiri kwa mauaji kwa Kanda ya Ziwa, na kwamba kuamini zaidi katika imani za kishirikina kuliko Mungu kunachochea wimbi hilo la mauaji.


Hayo yamebainishwa na Askofu Flavian Kasalla wa Jimbo Katoliki Geita katika ziara yake ya kichungaji aliyoifanya katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima iliyopo Geita mjini, iliyoambatana na utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 153 wa Parokia hiyo.

Askofu Kasala amesema kuwa tabia za kupiga ramli kwa waganga wa kienyeji ambao wengi huishia kuwa wachonganishi, zimekuwa kichocheo kikubwa cha mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi ambao wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa ya kuuawa na watu wanaodaiwa kutafuta utajiri kwa kukatisha maisha ya wengine.

Aidha Askofu Kasalla ameiomba Serikali kuangalia upya Leseni za uganga walizozitoa kwa waganga hao, ambazo zimewapa uhalali wa kupiga ramli na kuhatarisha maisha ya wengine.

"Ndugu zangu wapendwa natumia fursa hii kuiomba serikali kuangalia upya leseni za waganga hawa wanaojiita wa tiba asilia, kwani wanarudisha nyuma jitihada zetu sisi viongozi wa dini kuwaelimisha watu kuacha kufikiri kuwa kila ugonjwa ni wa kurogwa. Naisihi serikali isaidieni sana kuokoa maisha ya watu kwa kuwadhibiti waganga hawa ambao ni hatari kwa ustawi wa watu kimwili na kiroho” ameeleza.

Pia Askofu Kasalla amewahimiza watu wote kuzitumia hospitali zilizo kwenye maeneo yao ili wapate vipimo na tiba sahihi za afya zao,  badala ya kukimbilia kwenye ramli ambazo zinazidi kuwajaza watu ujinga wa ushirikina. Ameonya hali hiyo isipodhibitiwa vizazi hata vizazi vitaendeleza dhana hizo za kishirikina na kuishia kuuana bila hatia yoyote.

Askofu Kasalla amekemea vikali utoaji mimba kwa akina mama akisema kuwa kitendo hicho ni kiovu na dhambi kubwa mbele ya Mungu. Ametoa wito kwa waamini wa namana hiyo kuiendea haraka Sakramenti ya Upatanisho ambapo amewaalika kwake wote waliowahi kutoa mimba ili wakajipatanishe na Mungu na kuwekwa huru na kifungo hicho cha mauaji.


Katika kuhakikisha kuwa Jimbo la Geita linazidi kutoa huduma muhimu za Kijamii Askofu Kasalla amesema anakusudia kuanzisha kituo kikubwa cha Afya ambacho baadaye kitaendelezwa na kuwa Hospitali kubwa ya kuwafaa watu wengi, pia shule ya sekondari ya mchanganyiko itakayoanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ambapo hatua za awali zimeanza.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI