MAKALA: MWAKA WA HURUMA YA MUNGU UNA UMUHIMU GANI?


Baba Mtakatifu alitangaza na kuzindua Mwaka wa Pekee wa Jubilei ya Huruma ya Mungu kwa ajili ya Kanisa zima na ulimwengu. Katika Kanisa letu la Milenia ya Tatu na katika ulimwengu huu wa nyakati zetu hizi tendo hili lapaswa kutazama kama tukio-kiongozi la matukio yote makuu.
A. KWA NINI MWAKA WA HURUMA YA MUNGU?
Tunasoma katika Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko sababu ya kutangaza Maadhimisho ya  Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu:
“1. Yesu Kristo ni uso wa huruma ya Baba. Katika neno hili upo ufupisho sahihi wa fumbo zima la imani ya kikristo. Huruma imepata kuwa hai na yenye kuonekana katika Yesu Mnazareti, na hata ikafikia kilele chake katika Yeye. Baba “aliye mwingi wa rehema” (Efe 2:4), baada ya kumfunulia Musa jina lake kuwa ni “Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kut 34:6), hakuwahi kuacha hata mara moja kuonyesha hali yake ya kimungu katika nafasi zote za historia. “Ulipowadia utimilifu wa wakati” (Gal 4:4), kila kitu kilipokuwa kimepangwa kadiri ya utaratibu wake wa ukombozi, alimtuma duniani Mwanae pekee ili kutufunulia upendo wake katika ukamilifu wake. Aliyemwona Yeye, amemwona Baba (Rej. Yn 14:9). Yesu Mnazareti, kwa neno lake, matendo yake na kwa nafsi yake yote anaifunua Huruma ya Mungu.
2. Tunahitaji kulitafakari tena na tena fumbo la huruma. Ni chemchemi ya furaha, ya utulivu na ya amani. Ni sharti la wokovu wetu. Huruma ni neno linalotufunulia Utatu Mtakatifu wenyewe. Huruma ni tendo la juu na kuu kabisa ambalo kwa njia yake Mungu anatujia sisi. Huruma ni sheria ya msingi ambayo ipo katika moyo wa kila mtu anayemwangalia kwa unyofu wa macho ndugu anayemkuta katika safari ya maisha. Huruma ni njia inayowaunganisha Mungu na binadamu, na kuufungulia moyo mlango wa matumaini ya kupendwa daima, licha ya hali yetu ya dhambi.
3. Katika nyakati hizi tunaitwa kuitazama kwa makini sana huruma ili tuweze kuwa ishara wazi kabisa ya utendaji wa Baba katika maisha yetu. Kwa sababu hiyo nimeitangaza Jubilei ya Pekee ya Huruma, kama wakati maalum kwa ajili ya Kanisa, ambapo ushuhuda wa waamini unakuwa wenye nguvu zaidi na wenye kuzaa matunda mengi zaidi.“ (Uso wa Huruma)
Kimsingi, Baba Mtakatifu amekusudia Mwaka wa Jubilei kama wakati muafaka kwetu wa kujiuliza kwa pamoja na kila mtu katika nafsi yake - ‘Mungu ni nani?’ Ukisoma vizuri Bula ya kutangaza Mwaka wa Huruma, utagundua kwamba Papa anajibu tayari swali hili yeye mwenyewe kwa mapana na marefu.
Mtakatifu Yohane Paulo II naye katika ensiklika yake - Dives in Misericordia (Tajiri wa Huruma) - alitupatia changamoto iyo hiyo - tugundue upya Mungu ni nani! Swali la kimsingi na muhimu kabisa - kuliko hoja, malumbano ndani ya Kanisa, tofauti za kiteolojia - tujiulize Mungu ni nani? Tukishagundua Mungu ni nani, papo hapo pia tutafahamu sisi tunapaswa kuwa nani, kila mmoja wetu katika maisha yake binafsi  - maana tuliumbwa kwa sura na mfano wake - na tunapaswa kuweje kama Kanisa katika utume wake kwa wanadamu.

B. KWA NINI SASA?
Turejee tena Bula ya kutangaza Mwaka wa Huruma:
“4. Nimechagua tarehe 8 mwezi Desemba kwa sababu ya umaana wake katika miaka ya karibuni ya historia ya Kanisa. Kwa kweli, nitaufungua Mlango Mtakatifu siku tunapoadhimisha miaka hamsini tangu kuhitimishwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano. Kanisa linahitaji kulikumbuka daima tukio hilo. Kwa Mtaguso huo Kanisa liliingia katika upeo mpya wa historia. Mababa wa Mtaguso walitambua kwa dhati kwamba ni pumzi ya kweli ya Roho Mtakatifu hitaji la kumwongokea Mungu kwa binadamu (wake kwa waume) wa nyakati hizi kwa njia ya wazi zaidi. Kuta ambazo kwa muda mrefu zililifanya Kanisa liwe kama ngome ziliangushwa chini, na wakati ulifika wa kutangaza Injili kwa mtazamo mpya. Ni njia mpya ya uinjilishaji uleule uliokuwepo tangu mwanzo. Lilikuwa ni jukumu jipya kwa wakristo wote kutoa ushuhuda wa imani yao kwa ujasiri mkubwa zaidi na kwa msimamo zaidi. Kanisa lilipata kuwa makini zaidi kwamba kazi yake ni kuonyesha kwa dhati zaidi upendo wa Baba ulimwenguni. (…) Mtaguso umeupatia ulimwengu wa sasa ujumbe wa kutia moyo badala ya ule unaokatisha tamaa, badala ya utabiri wa kutisha, ujumbe wa matumaini.” (Uso wa Huruma)
Baba Mtakatifu alitangaza Mwaka wa Huruma ya Mungu kwa ajili ya kuenzi Jubilei ya Miaka 50 ya kumalizika kwa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican - 8/12/1965. Papa Fransisko anaamini kabisa kwamba siku Mtaguso wa Pili wa Vatikano ulipomalizika, Kanisa Takatifu la Kristo liliingia katika awamu mpya kabisa ya historia yake.
Wakati Mtaguso huo ulipoanza, watu wengi duniani walikuwa wanaona Kanisa Katoliki kama jumuiya ya kidini iliyolazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, kama taasisi iliyopitwa na wakati, isiyokuwa na kauli ya maana wala hoja yoyote ya maana tena katika ulimwengu wa kisasa. Kwa upande mwingine, Kanisa nalo lilizidi linajijenga zaidi na zaidi ndani yake na kujielewa kama ngome dhidi ya mambo mapya mabaya yaliyokuwa changamoto kwake. Mtaguso ulipomalizika, hali hiyo ilibadilika ghafula.
Baba Mtakatifu Paulo VI katika yatokanayo ya Mtaguso wa Pili wa Vatican aliandika ujumbe kwa makundi manane ya watu mahsusi duniani wakiwemo watoto, wanawake, wanasayansi, wanasiasa, wasanii na wengineo na kuwaambia kama ifuatavyo: “Mtaguso wa Pili wa Vatikano umemalizika na kutoka pande zote za dunia sauti zinasikika zikituuliza - mna neno lolote la kutuambia sisi? mnao ujumbe maalum kwa ajili yetu?
Kanisa ambalo lilikuwa limekwishazikwa katika fikra na mitazamo ya wengi linahojiwa sasa kama sauti yenye hoja muhimu na kauli nzito katika dunia ya kisasa - “Mna neno lolote kwa ajili yetu?” All of a sudden, everybody started to pay attention to the Church again and what the Church had to say on various matters!
Hilo ndilo analotaka kutuambia Baba Mtakatifu Fransisko. Hilo ndilo analosimamia kwa dhati katika Upapa wake tangu mwanzo. Kanisa la Baba wa Huruma lililozaliwa ubavuni mwake Yesu Msalabani kwa hulka yake ni Kanisa la kiPentekoste. Ni Kanisa linalotoka nje kutafuta kwa huruma kondoo waliopotea na watu waliotupwa na kudharauliwa na kuonewa katika jamii. Kanisa linalotangaza Injili kwa ushujaa, kwa furaha, kwa upyaisho wa kiroho na wa kifikra. Kanisa linalojielewa kama Kanisa la kitume. Kanisa linalong’aa Uso wa Huruma wa Baba katika nafsi ya Kristo wa Huruma, Mchungaji Mwema mwenye Huruma. Kanisa lenye Huruma KAMA BABA!
Baba Mtakatifu Paulo VI alisema kwamba endapo tunatafuta namna ya kujumlisha yatokanayo na Mtaguso wa Pili wa Vatican katika ujumbe mmoja, katika kauli moja, katika sura moja, basi, anaona kwamba - muhtasari sahihi wa Mtaguso ni Simulizi la Msamaria Mwema. Basi, turejee sasa matini ya Simulizi hilo.
Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang'anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang'anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” (Lk 10:25-37)
Kuhani na Mlawi walinukia harufu ya ubani wakati walipopita kando ya Mwisraeli mwenzao majeruhi wakiwa wanatelemka kutoka Yerusalemu kurudi nyumbani. Maana walitoka katika huduma takatifu ya Hekalu la Mungu Yerusalemu. Wameshindwa kuunganisha uchaji wa Mungu hekaluni na uchaji wa Mungu katika maisha ya kawaida ya kila siku. Huenda kwa hofu ya kunajisiwa kadiri ya Sheria ya Musa.
Barabara iliyokuwa inaunganisha Yerusalemu na Yeriko ina urefu wa karibia kilometa 30 na inapita katika bonde hatari la Wadi Qelt. Yerusalemu imejengwa katika mwinuko wa futi 2,461 juu ya usawa wa bahari wakati Yeriko iko futi 1,312 chini ya usawa wa bahari. Kumbe, barabara kutoka Yerusalemu ni mtelemko mkali na ndiyo maana simulizi la Yesu linaeleza kwamba walikuwa wakitelemka kutoka Yerusalemu kuelekea Yeriko.
Msamaria Mwema ambaye alikuwa hana habari hata na Hekalu la Yerusalemu maana Wasamaria hawakulitambua Hekalu la Yerusalemu kama Hekalu la Mungu, tunavyojua, alisimama, alimwinamia adui wake Mwisraeli majeruhi na kumhurumia.
Alichokifanya yeye ni sawa na matendo ya kiibada waliyokuwa wanafanya makuhani katika Hekalu la Yerusalemu - alizitia majeraha ya Mwisraeli majeruhi mafuta na divai. Tazameni jambo hili! Msamaria aliyanyunyizia majeraha ya Mwisraeli kwa kutumia divai - sawa na Makuhani waliokuwa wananyunyizia sadaka na kafara zilizokuwa zinatolewa Hekaluni kwa kutumia divai vilevile. Kumbe, Msamaria amekuwa Kuhani wa kweli aliyeona Hekalu la Mungu katika mwili wa majeruhi huyo. Na akaunganisha imani yake na huduma iliyojaa huruma kwa majeruhi huyo ambaye alikuwa wa kabila la maadui zake.
Siku moja kabla ya kuuawa kwake, Martin Luther King Jr. alitoa hotuba yake juu ya Msamaria Mwema. Katika tafakari yake alisema yafuatayo: “Swali la kwanza alilojiuliza Kuhani, swali la kwanza alilojiuliza Mlawi lilikuwa hili - ‘Nikisimama na kumsaidia mtu huyu, nitakuwaje (what will happen to me)?’ Na Msamaria Mwema alipofikia mahali pale akajiuliza swali tofauti - ‘Nisiposimama na kumhudumia mtu huyu, atakuwaje (what will happen to him)?’”
Tunaweza kuongeza swali la tatu hapo - ‘Nitakuwaje (what will happen to me), nisiposimama na kumhudumia majeruhi katika maisha yangu?’
Kumbe, ndugu zangu, sisi pamoja na waamini wenzetu kila wakati tunapotoka kanisani baada ya Misa kila siku au hata siku za Dominika tu, tukumbuke kwamba majeruhi na wenye shida mbalimbali daima wamelala daima kando ya njia yetu ya kurudi nyumbani. Wapo daima! Tukitaka tu kutazama kwa jicho la huruma, tutawaona! Swali tunalopaswa kujihoji - je, tutawapita kwa hofu ya kutoka katika ulimwengu tuliozoea na kukutana na mambo mapya katika maisha yetu na Ukristo wetu; au tutawainamia na kuwahurumia na kuwahudumia kimatendo kama Msamaria Mwema aliyejihoji - nisiposimama na kumhudumia majeruhi huyo atakuwaje?
Jibu analo kila mmoja wetu. Tutagusia hitaji hili la kuunganisha uchaji wetu kanisani na maisha yetu ya matendo ya huruma na uinjilishaji wa ulimwengu katika mada zetu hatua kwa hatua.
Mpasuko huo uliopo kati ya uchaji wetu Kanisani na maisha yetu ya kila siku ndio alioufikiria Baba Mtakatifu Paulo VI aliposema kuwa muhtasari wa Mtaguso wa Pili wa Vatikano ni simulizi la Msamaria Mwema; na ndicho anachofikiria Baba Mtakatifu Fransisko kwa kutangaza Mwaka wa Huruma kwa kuheshimu Jubilei ya Miaka 50 ya Mtaguso huo - na kurudia ujumbe wake kwamba Kanisa la sasa linatakiwa kuwa Kanisa la Msamaria Mwema anayewaona Majeruhi na kuona ndani mwao Hekalu la Mungu Aliye Hai na kuwahudumia kwa huruma. Kanisa ambalo limeunganisha upya Ibada Takatifu Hekaluni na huduma ya huruma na upendo kwa watu wenye taabu mbalimbali duniani. Kanisa linaloitikia kauli ya Mtume Yakobo:
Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu. Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii - kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.” (Yk 1:21-27)
Baba Mtakatifu aliuita mwaka huu kuwa Jubilei ya Huruma, maana tunahitaji sote kusoma upya Sura ya Baba wa Huruma, tunahitaji kugundua upya kwamba Mungu si mwingine bali ni Huruma yenyewe. Jina la Mungu ni HURUMA. Na kwa kusoma Sura ya Baba wa Huruma na kutambua uhusiano wake na watoto wake, sisi wenyewe tuweze kubadilika, kuongoka na kuwa na huruma sisi kwa sisi na kwa wahitaji wote - KAMA BABA.
Tunaishi katika ulimwengu ambao hatua kwa hatua husahau huruma ni nini. Baba Mtakatifu anasema kama binadamu haoni dhambi, basi atawezaje kuhitaji Huruma ya Mungu? Kadiri ulimwengu unavyozidi kusahau huruma na kushindwa kuielewa, kadiri iyo hiyo Mungu ataka kutuonyesha kwamba Yeye ni mwingi wa Huruma na kwamba anatupenda kwa upendo na huruma kamili kabisa. Tukishagundua Mungu ni nani na sisi ni akina nani, basi, tutagundua vilevile Kanisa lapaswa kuweje na sisi ndani yake vilevile. Maana Kanisa lina utume mmoja tu - kujinafasi katika uhusiano huo wa Mungu na wanadamu. Endapo Kanisa lingejikuta limo nje ya mahusiano hayo, basi litageuka kuwa taasisi ya ajabu isiyoeleweka.
Ili Mwaka huu wa Jubilei ya Huruma ulete kweli tija na mafanikio yanayotarajiwa na Baba Mtakatifu, unatakiwa uanze kwanza katika nafsi zetu sisi wenyewe.
Sisi kwanza tunapaswa kujiuliza - Mungu ni nani kwangu? Mungu ninayemtangaza na kumhudumia katika Ukristo wangu ni nani? Katika Ukristo wangu ninadhihirisha Uso gani wa Mungu? Kweli, watu wanaona katika maisha yangu na huduma yangu ya kikristo Uso wa Huruma wa Baba? Mdomo wangu ni Lango la Huruma au handaki ya mashetani? Moyo wangu ni Lango la Huruma lililo wazi kwa wahitaji wa kila namna wanaonizunguka ama ni pango la wanyang’anyi?
Kama Yesu kweli ni Umwilisho wa Huruma ya Baba, kama Yeye kweli ni Uso wa Huruma wa Baba, sisi nasi je? Hatupaswi pia kuelewa, kufahamu na kuliishi fumbo la Ukristo wetu kama Umwilisho wa Huruma ya Mungu, kama Uso wa Huruma wa Baba!
Na Padre Wojciech Adam Koscielniak.
Kituo cha Hija Kiabakari,
Jimbo Katoliki Musoma.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI