"FANYENI KAZI POPOTE" ASK NDIMBO




MAPADRI wametakiwa kuwa tayari kufanya kazi ya uinjilishaji katika mazingira yoyote na kuifanya kazi hiyo kwa uaminifu.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Mbinga Mhashamu John Ndimbo Septemba 29, 2016 katika sherehe za kutimiza miaka 50 tangu Parokia ya Mikalanga ianzishwe.
Askofu Ndimbo amewataka mapadri kuwa tayari kuinjilisha katika mazingira ya aina yoyote yale kutokana na ukweli kuwa baadhi ya mapadri hawatoi huduma ipasavyo katika vigango vya parokia zao eti kwa kukosa usafiri wa magari.
“Mapadri hao wanapoombwa wapewe pikipiki badala ya magari wanasema kuwa hawawezi kutumia pikipiki kwa sababu wana matatizo ya mgongo. Lakini mapadri hao hao wanaonekana mjini Mbinga wamebebwa na bodaboda wakati wanapofuatilia miradi yao ya binafsi” amesema Askofu Ndimbo.
Aidha Askofu Ndimbo ametoa wito kwa waamini wa Parokia hiyo ya Mikalanga kuacha tabia ya kuoa wake wengi kwa visingizio kwamba kitendo hicho kinawarahisishia shughuli za kilimo cha kahawa.
“Visingizio hivi kwa kweli havina mashiko kwa wakati huu kwa sababu kahawa sasa imeingiliwa na ugonjwa, na mapato yako chini sana lakini mitara bado inaendelea kushamiri” ameeleza.
Pia amewakumbusha waamini hao kuwa na moyo wa kusaidia kanisa na utoaji wa zaka. Amesema kuwa waamini wa Mikalanga si wepesi katika masuala ya kusaidia kanisa na katika utoaji wa zaka, kiasi kwamba kuna majengo ya vigango vya kanisa yaliyoanza kujengwa miaka ya huko nyuma  na bado hayajakamilika hadi sasa.

Historia fupi ya Parokia ya Mikalanga.
Uinjilishaji wa eneo la Mikalanga: Eneo la Mikalanga liliinjilishwa na Wamisionari Wabenediktini wakitokea Litembo. Mwanzoni waliichukua Mikalanga kama sehemu ya Parokia hiyo. Maguu ilipoanzishwa Parokia, Mikalanga ilikuwa inahudumiwa kama sehemu ya Parokia ya Maguu.
Padri Joseph Damm, Paroko wa Maguu, alianza kupiga zamu Mikalanga mwaka 1943 akisaidiwa na Mapadri Adelgoth OSB na Pirmin OSB. Mwaka 1946 wakristo wa maeneo hayo mwalijenga kanisa dogo eneo la Mkegeto na kupaita mahali hapo “Mikalanga”.
Mapadri wengine walikuja kuhudumia baadae hapo Mikalanga. Waamini walipoongezeka, lilihitajika kanisa kubwa. Mwaka 1960 tofali zilifyatuliwa chini ya usimamizi wa Pd.Beda OSB. Mwaka 1961 kanisa lilijengwa na kutabarukiwa.  
Kuanzishwa kwa Parokia ya Mikalanga na mbio za uinjilishaji katika eneo hili:
Kutangazwa kwa Parokia, na Paroko wa kwanza wa Mikalanga: Baada ya kifo cha Pd. Michael aliyekuwa Paroko wa kwanza wa Mikalanga,  Jimbo la Peramiho chini ya Askofu Abate Eberhard Spiess OSB lilihakikisha kwamba Parokia ya Mikalanga inahudumiwa ipasavyo.
Mapadri waliopelekwa walikuwa ni Pd. Gottfried Rhein (1968 -1969). Pd.Gottfried alifanya uchungaji Mikalanga akitokea Maguu ambako ndiko alikuwa akiishi.     Jimbo la Songea lilipoanzishwa mwaka 1968, Askofu wa Songea ndiye aliyebeba dhamana ya uinjilishaji.
Mapadri wamisionari waliendelea kutumwa Mikalanga. Mathalani, mapadri: Daud OSB (1969 – 1984), Osmund Kastner OSB (1977 – 1984) kama Padri msaidizi, Basil Fetz (1982 – 1983) na Erich OSB (983 – 1985) walitoa huduma huko.
 Mapadri wazalendo wainjilisha Parokia ya Mikalanga: Mapadri wazalendo walianza kuhudumia Parokia ya Mikalanga kuanzia mwaka 1985. Kuanzia mwaka huo mpaka leo, ni mapadri wazalendo wanaoendeleza kazi ya uinjilishaji Mikalanga.
Mpaka sasa Parokia hiyo imehudumiwa na mapadri wazalendo wafuatao: Pd. Lukas Komba (Liberatus) Paroko (1985), Pd. Vitus Kapinga (1986 – 1987), Joseph Ngahi (1987), Pd. Erasmo Mhagama (1987 – 1989), Pd. Theodos Thilia (1989 – 1990).
 Pd. Theophor Henjewele (1990), Pd.Sales Mapunda (1990 – 1993) ambaye alikuwa na mapadri wasaidizi akina Pd. Osmund Nchimbi na Pd. Emeran Kihwili kwa nyakati tofauti tofauti. Mapadri wengine ni: Pd. Amon Nchimbi (1993 – 1995), Pd. Bruno Ndunguru (1995 – 1996), Pd.Alex Nombo (1996 – 2001), Pd. Moses Haule (2001 – 2007), Pd. Erick Kamchatika (2007 – 2013) na Pd. Severin Njako 2013 mpaka sasa).

 Na Philip Komba, Mbinga

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI