UNYENYEKEVU NA USIKIVU KATIKA KUUJENGA UFALME WA MUNGU


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 25 Oktoba 2016 amesema kwamba, waamini wanapaswa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu na usikivu ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani. Anakumbusha kwamba, miundo mbinu na mashirika mbali mbali yana mchango kidogo sana katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwani huu ni Ufalme ambao daima unatembea na wala haujaganda na kusimama kama maji mtungini!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, heri wale wanaotembea katika Sheria ya Bwana, ambayo waamini wanapaswa kuisoma, kuitafakari, lakini zaidi kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yao kwa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, daima wakiwa katika hija ya maisha. Mwenyezi Mungu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, ili kwa njia ya maisha yao waweze kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaoendelezwa na kudumishwa na waamini wote kila siku ya maisha. Ufalme wa Mungu haufumbatwi kwa Sheria ngumu, bali ni katika unyofu wa moyo kwa kumsikiliza na kutekeleza mapenzi ya Mungu. Baba Mtakatifu anauliza swali la msingi, itamfaa nini mtu kupata ulimwengu wote na hatimaye, kuangamia kwenye moto wa milele. Yesu katika Injili ya siku anazungumzia mambo ya kawaida kabisa yanayoweza kuchachua na kuumua mkate na kuwa ni chakula kwa wengi. Mbegu isipopandwa ardhini haiwezi kuota na kuzaa matunda yanayokusudiwa. Hata mambo madogo madogo yanaweza kusababisha mchakato wa mabadiliko na mageuzi katika maisha na ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ili Ufalme wa Mungu uweze kukua, kukomaa na kuzaa matunda ya haki, amani, upendo na mshikamano, kuna haja kwa waamini kujikita katika unyenyekevu kwa kuwa wasikivu kwa Roho Mtakatifu anawakirimia waamini nguvu ya kufanya mageuzi katika maisha na baadaye Ufalme huu unakuwa ni kwa ajili ya wote. Waamini wenye fadhila ya unyenyevu ni zawadi kubwa kwa jirani zao, ni chachu ya matumaini katika mchakato wa kuelekea kwenye utimilifu wa maisha ya uzima wa milele.
Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka waamini kuondokana na shingo ngumu na moyo wa jiwe, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, kwani ugumu wa moyo unawafanya waamini kuwa tasa na yatima. Ufalme wa Mungu ni kama Mama anayejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wake. Waamini wawe na ujasiri wa kumwomba Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia fadhila ya unyenyekevu na usikivu, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu hapa duniani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI