AGIZO LA RAIS MAGUFULI KWA MABALOZI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, jana
tarehe 07 Oktoba, 2016 amekutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania
katika nchi mbalimbali duniani ambapo pamoja na mambo mengine ametaka
utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utiliwe mkazo katika uwekezaji
kwenye sekta ya viwanda.
Katika
Mkutano huo uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa, Rais Magufuli aliyehutubia na kuongoza majadiliano juu ya
masuala mbalimbali ya shughuli za mabalozi, alisema Tanzania imeweka
dhamira ya kuikuza sekta ya viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 hadi
kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2021 na kuzalisha ajira kwa asilimia
40.
“Sasa
nimeona niwaite waheshimiwa Mabalozi ili tuelewane, mjue mwelekeo
tunaoutaka na mjue ni namna gani mtakavyoshiriki kuhamasisha uwekezaji
wa viwanda.
“Nataka
badala ya kubaki mmejifungia ofisini, mtoke mwende mkawatafute
wawekezaji waje wawekeze katika viwanda ili nchi yetu inufaike kwa watu
wetu kupata ajira, Serikali kukusanya kodi na tuinue maendeleo yetu” alisema Rais Magufuli.
Maeneo
mengine ambayo Rais Magufuli ametaka Mabalozi wayafanyie kazi ni
kutangaza na kuwavutia watalii kuja hapa nchini, kufanyia kazi fursa
zote zenye manufaa kwa Tanzania katika nchi wanakowakilisha, kulinda
mali za nchi zilizopo katika nchi hizo na kufuatilia utekelezaji wa
mikataba ya biashara na uwekezaji inayofanywa kati ya Tanzania na nchi
wanakowakilisha.
Pia
Rais Magufuli aliwataka waheshimiwa Mabalozi wote kufanya kazi kwa
juhudi, kuondoa kasoro za utendaji kazi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa
katika ofisi zao na kubana matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima.
Dkt.
Magufuli aliitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kujipanga na kudhibiti mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha
za umma ambazo zimekuwa zikitumika katika safari za nje ya nchi na
matumizi mengine yasiyo ya lazima, pamoja na kuhakikisha watumishi wote
ambao wapo katika ofisi za ubalozi kwenye nchi mbalimbali bila sababu za
msingi wanarejeshwa nchini ili kupunguza mzigo wa gharama kwa Serikali.
“Kuna
wafanyakazi wapo kwenye Balozi zetu wakati hata sifa za kuwa katika
nafasi wanazoshikilia hawana, ilifika mahali mtu akiharibu hapa nyumbani
anapangiwa ubalozini.
“Wakati
mwingine unakuta ubalozi wa Tanzania kwenye nchi fulani una idadi kubwa
ya wafanyakazi kuliko mahitaji ya ubalozi huo, haiwezekani” alisisitiza Rais Magufuli.
Hata
hivyo Dkt. Magufuli aliwapongeza Mabalozi wote wa Tanzania kwa kazi
wanazozifanya kwenye nchi wanazowakilisha na amewahakikishia kuwa
Serikali ina matumaini nao na inawategemea kuwa wataendelea kuiwakilisha
na kuitangaza vizuri Tanzania.
Mkutano
huo pia ulihuduriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu
Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa vyombo vya
ulinzi na usalama, Viongozi wa Taasisi mbalimbali na Wakurugenzi wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Comments
Post a Comment