MISAADA YA KIGENI ITUSAIDIE KUWA KANISA LA KUJITEGEMEA
NAANZA
Makala haya kwa maneno ya Hayati Mwalimu Nyerere aliyesema kwamba: “Itatufaa zaidi kutumia muda katika vijiji
tukiwaonesha watu namna ya kuleta maendeleo kutokana na juhudi zao wenyewe
kuliko kufanya safari ndefu na za gharama kubwa kwenda ng’ambo kutafuta fedha
ya maendeleo”.
Maendeleo waliyoleta
wamisionari ni mengi sana na mpaka leo wanazidi kutuendeleza. Lakini bado
hatujafikia lengo letu jingine la kulijenga Kanisa la Kitanzania
linalojitegemea. Kwa nje inaonekana kama Kanisa letu linajitegemea kiuchumi
lakini tuko mbali kabisa na lengo hilo.
Maendeleo ya Parokia
zetu yasidhaniwe kuwa ni maendeleo ya Kanisa. Kujitegemea kwa wamisionari wa
kwanza si kujitegemea kwa wakristo wa Tanzania. Si jambo la ajabu kumsikia mmisionari
akishangaa kama mapadri waafrika watapata wapi wataalamu na fedha za kuendeleza
shughuli zote zilizoko Parokiani hivi sasa.
Hii ni kwa sababu kile
wanachokitoa wakristo wengi kwa kusaidia Kanisa lao hakitoshi kuendesha shughuli
zote tulizonazo hivi sasa maparokiani na majimboni.
Leo tunapata matatizo
kupata zaka ya kanisa sababu parokia zetu zina vitu ambavyo kwa watu ni alama
ya utajiri. Mahali pengine ni kweli kuna vitu vingi lakini hivyo havikuletwa na
wakristo wa Tanzania au wakristo mahalia bali wa ng’ambo, ndiyo maana wakristo
wetu inawapasa waanze toka sasa kujifunza kutoa zaidi kwa ajili ya kanisa lao
kama vile hao ndugu wa huko Ulaya na Marekani.
Namna nyingine baadaye
watakapoondoka kabisa watafikiri kuwa Kanisa letu hapa linajitegemea kiuchumi
kumbe sivyo, bali ni kiutumishi tu.
Watu
walizoea kupata bure:
Kanisa ambalo ni mahali
pa ibada, ni kitu kimojawapo kati ya vile vya maana sana ambavyo wakristo
wanahitaji kwa ajili ya ibada na mambo ya liturujia.
Toka mwanzo ingekaziwa
sana kwamba wakristo lazima watoe kiasi fulani kwa ajili ya ujenzi wa makanisa.
Lakini inasikitisha kwamba makanisa makubwa na majumba kadhaa yamejengwa bila
wakristo kutoa hata senti moja mahali pengine. Si lazima watoe sehemu kubwa
hasa kama hawana chochote.
Lakini kiasi kidogo
wangeweza kutoa, bora tu kama wanashirikishwa katika ujenzi wake. Tuanze
polepole kuondoa mawazo ya kwamba makanisa na majumba ya mapadre yatajengwa
daima na maaskofu bila wakristo kusaidia.
Wakatoliki wengi katika
sehemu fulani hawakuzoea kulipa kitu kwa ajili ya ujenzi wa makanisa, nyumba za
mapadre, ghrama ya mahitaji ya kanisa na safari ya kichungaji ya mapadre katika
vigango.
Ndiyo maana mahali
pengine wanaona kama ni fundisho jipya kutoa zaka ya kanisa na michango mingine
kwa ajili ya kujenga kanisa au kutoa posho ya makatekista wo. Wanafanya hivyo
si kwa sababu ya ubishi, bali ni kwa sababu hawafahamu wajibu wao kutokana na
mazoea waliyopata toka mwanzo.
Kama wangefahamu mapema
bila shaka wangetoa. Wakati fulani wakristo tangu mwanzo walipewa misaada bila
maelezo kwamba nia ya misaada hiyo ni kutaka baadaye wajitegemee.
Mwalimu Nyerere alisema
kwamba: “Kuna njia moja tu tunayoweza kutumia kuwafanya watu wajiletee maendeleo
yao wenyewe. Njia yenyewe ni kuwaeleza na kuwaongoza”.
Kwa njia hizo watu
wanaweza kusaidiwa wakaelewa shida zao na mambo yanayoweza kufanya kumaliza
shida hizo. Kwa hiyo inatupasa kuwaonesha watu njia ya maelezo kwamba ingawaje
wanaona majengo mazuri, bado kanisa haliwezi kujengwa na mambo hayo, isipokuwa
waamini wenyewe wanashughulika kuinua hali ya Kanisa la Tanzania.
Misaada ya ndugu zetu
wa ng’ambo iwe tu ni ya kuendeleza kile ambacho tunacho au kutafuta kingine kwa
mtaji wa kutoka nje. Kama wataelewa maelezo hayo sina shaka wakristo wengi
watakuwa tayari kulipa zaka na michango yao ya kulijenga Kanisa.
Wakristo waelezwe kwa
mafundisho ya kina kuhusu matumizi na namna ya zaka na michango mbalimbali ya
Kanisa kabla ya kutiliwa mkazo utoaji wake. Kama watu wameelewa ndipo hapo
wanaweza kuanza kutilia mkazo utoaji wake.
Waamini waelezwe kwamba
zaka ya Kanisa hutumika kwa kuendeshea shughuli zote za Kanisa. Zaka ya Kanisa
ni kwa ajili ya mahitaji ya Parokia, Jimbo na Kanisa lote kiujumla.
Kutoa Zaka si jambo
jipya, ni Amri pia ya 5 ya Kanisa. Hata mababu zetu Abrahamu Mw. 14:20, Mw.
28:22, kumb. 14:22-28, 26:12-15 na Hes. 18:21-22, walitoa Zaka na walifundishwa
na Musa. Hata Wafarisayo walikuwa waamini katika kutoa zaka Mt. 13:23,
Lk.11:42. Ni mazoea na ya kufaa ambayo humnyunyizia mafaa juu ya mlipa zaka,
Parokia na Kanisa lote ulimwenguni.
Wakati wowote wa kulipa
zaka, mambo yafuatayo daima yakumbukwe, yaani ni lazima nitoe zaka kwa sababu:
1)
Nampenda Mungu na jirani yangu.
2)
Nataka kuona kanisa linaendelea.
3)
Mungu anadai, na
4) Malipo yake ni mara mia zaidi kwa
mtumishi mwaminifu.
Na
Syllvanus Kayanda
Mwandishi
ni Padri wa Kanisa Kuu,
Jimbo
Katoliki Kigoma
P.O.Box
71 KIGOMA.
Comments
Post a Comment