MIAKA 25 YA PAROKIA YA FAMILIA TAKATIFU
Waamini wa parokia
ya Familia Takatifu jimboni Sumbawanga wanamshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 25
tangu kupandwa kwa mbegu ya imani parokiani hapo.
Wakizungumza katika
sherehe za jubilei hiyo wananchi na waamini wa parokia ya Familia Takatifu
wamesema kuwa kanisa katoliki ni nguzo ya maendeleo kwa waamini na wananchi kwa
ujumla kwa maeneo mbalimbali.
"Miaka 25 ya
parokia ya Familia Takatifu ni ukomavu wa huduma za kiroho na kimwili kwa
waumini wake na wananchi kwa ujumla kwani kwa muda huu kumekuwa na shughuli za
kijamii ambazo ni msaada kwa watu wote wakatoliki na wasio wakatoliki kama vile
shule ya chekechea, mashine za kusaga na kukoboa hali kadhalika kupata mapadri
na watawa ni matunda ya parokia hii". amesema ndugu Nolasco Kalikwenda
katibu wa parokia.
Akiongoza maelfu ya waamini
waliohudhuria misa ya jubilei ya miaka 25 ya parokia ya familia takatifu Askofu
wa jimbo katoliki Sumbawanga Mhashamu Damian Kyaruzi amesema kuwa katika mwaka
huu wa huruma ya Mungu na jubilei ya parokia, ni vema kuziishi fadhila za
kimungu yaani Imani, Matumaini na Mapendo kama ilivyokuwa katika familia ya Nazareti
ya Yesu, Maria na Yosephu.
"Ili kuhusisha
maisha wa somo wa parokia hii yaani familia ya Yesu ,Maria na Yosephu na
kupitia makuzi ya miaka 25 tangu kupandwa kwa mbegu ya imani katika parokia hii
ni vema kuziishi fadhila za kimungu yaani imani, matumaini na mapendo. Na kwa
kufanya hivyo mtaweza kulea watoto wenu katika maadili yanayokubalika kama
ilivyokuwa kwa mtoto Yesu ambapo itafanya watoto wawaheshimu na kuwasikiliza
wazazi wao na kwa namna hiyo jamii ya Sumbawanga na Tanzania nzima hatutakuwa
na watoto vibaka, wapiga nondo, wavuta bangi, wahuni na hata walioshindikana
hata kwa wazazi wao" Amesema Askofu Kyaruzi.
Aidha Askofu Kyaruzi
ameongeza kuwa jina la parokia hiyo ya familia takatifu limesababisha kiasi cha wengi kushindwa
kutambua jina la asili la sehemu ile na kila mtu awe wa imani gani ukimuuliza
unakwenda wapi, hana cha kutaja zaidi ya Familia takatifu kwahiyo ni vema
familia za kikristo zikalienzi jina hilo pamoja na parokia yao kwa kuhudumia
jamii inayozunguka kwa kuyaishi maisha ya familia ya Nazareti.
Parokia ya
Familia Takatifu ilianza mwaka 1990 na kuwekwa wakfu tarehe 13 Mei 1990 na
Mhashamu Askofu Tarcicius Ngalalekumtwa.
Katika kipindi cha miaka 25 Parokia
hii imeongozwa na Mapadri mbalimbali na kwa vipindi tofauti ambao ni Paroko na
mwanzilishi Padri Luka Ville akifuatana na Paroko Hugo, Maparoko hao
walisaidiwa na Mapadri Peter Durie, Padri Baisloji na Padri Alois Monsiwenga na
Brother Sikeleni.
Walifuatiwa na Maporoko Peter Vander
Pass Simchile, Emil Luwaga, Joachim Sangu na sasa anayeongoza ni Padri Leonard
Teza akisaidiwa na Padri Gaudensi
Sindani.
Mapadri wengine waliofanya kazi ya utume Parokiani hapo ndani ya miaka 25 nao ni Padri
Demetrius Kazonde, Padri John Chiwalala, Padri Boniface Nyama na Padri Charles
Kasuku.
Na Emmanuel Mayunga, Sumbawanga
Comments
Post a Comment