" TUVITHAMINI VYOMBO VYA HABARI VYA KANISA" ASKOFU NZIGILWA
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu
Katoliki Dar es Salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa amekemea waamini wanaopenda
kufuatilia vyombo vya habari vya kidunia kuliko vya kanisa na hivyo kufanya kazi
ya uinjilishaji kuwa ngumu, kwani kanisa hutumia vyombo vyake kuinjilisha huku
wakristo wengi wakipitwa na fursa hiyo.
Ameeleza
hayo hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya
Kipaimara katika Parokia ya Teresia wa Mtoto Yesu, Mafia
Ambapo
takribani vijana 30 walipokea Sakaramenti hiyo, idadi ambayo haijawahi kufikiwa
katika kisiwa hicho cha Mafia, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wake ni
waislamu.
“Wangapi
mnasikiliza redio za kanisa? Hamsikilizi kwa sababu mnapenda mambo ya kidunia”
amehoji Askofu Nzigilwa.
Aidha amesema kuwa Yesu aliwaagiza watu waende
ulimwenguni kote wakatangaze Injili, hivyo hawapaswi kupinga agizo la Mungu, na
kwamba atakayemuonea aibu naye atamuonea aibu mbele ya Baba yake.
Amewaasa
vijana waliopata Sakramenti ya Kipaimara kuwa hata wao wanatumwa kuitangaza
Injili, na kuwataka waitangaze Huruma ya Mungu bila uwoga kwai huu siyo wakati
wa kujificha.
“Wazazi
msiwalee watoto kwa kuzingatia usafi wa kimwili pekee, bali fanyeni hivyo pia
kwenye usafi wa kiroho. Tusiwalee watoto kwa kuwafanya wapende kitu bali utu,
kwani kitu huchakaa na hutupwa, ninyi mkizeeka watawakataa kwa kuwa mtakuwa hamna kitu” amesisitiza Askofu
Nzigilwa.
Baada ya Adhimisho
hilo la Misa Takatifu ilifuata halfa iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali na
wa dini mbalimbali, huku kwa upande wa serikali Mkurugenzi Mtendaji Mafia Erick
Chrisantus Mapunda amemuomba Askofu Nzigilwa afikishe
salamu kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuwa wapo tayari kutoa eneo ili
ijengwe shule ya Sekondari kidato cha
tano na sita.
Pia
ameongeza kuwa Serikali wilayani humo ipo tayari kutoa kiwanja kingine kwa
Kanisa ili kuunga mkono juhudi za Kanisa katika kutoa huduma za afya.
“Tupo
tayari kutoa eneo jingine ili kujenga kituo cha afya. Japo itakuwa mali ya
kanisa tunafahamu kuwa watakaonufaika ni watanzania wote”
TEC
Comments
Post a Comment