SHULE KADHAA ZAFUTWA

Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imezifuta shule nyingine za awali na msingi nchini ambazo hazijasajiliwa zaidi ya 10 kuanzia Desemba mwaka jana. Aidha, shule tano kati ya 40 zilizokuwa zimefutiwa usajili zimekamilisha taratibu na kurejeshewa usajili wake.


Kaimu Mkurugenzi wa Usajili wa Shule katika wizara hiyo, Khadija Mcheka amesema mpaka sasa bado wanaendelea na ukaguzi kubaini shule ambazo hazijasajiliwa.

Alizitaja shule ambazo zimefutwa kwa kutosajiliwa kuwa ni Mwandai Junior Academy, shule ya msingi DACETE, shule za msingi Malaika na Fares Kisingo (FK) za wilaya ya Kinondoni. Nyingine ni shule ya msingi The Unity, shule ya sekondari Jotac iliyopo eneo la Kipunguni, Verena iliyopo eneo la Pugu zote wilaya ya Ilala, Exodus iliyopo Kigamboni na Havard Junior ya wilaya ya Temeke.

Alisema shule nyingine zilizofutwa kabisa ni shule ya sekondari ya Kahe ambayo imefutwa kutokana na wamiliki kushindwa kuiendesha na pia majengo yake yamebadilishiwa matumizi. 

Alisema shule nyingine za Deogrolius International School iliyopo Kitunda, Desinity na Almustakim zote za jijini Dar es Salaam nazo zimefutiwa usajili. Alisema awali yalitolewa majina ya wamiliki.

Mcheka alisema pia shule mbili hazitakiwi kuwa za bweni ambazo ni Heritage iliyopo Banana Ukonga na Hellens iliyopo Kinondoni.

Akizungumzia shule zilizorejeshewa usajili, alisema ni Gisera, Rose Land, Conerstone na Grace za jijini Dar es Salaam na Must Lead na Qunu zilizopo mkoani Pwani huku shule ya Fountain Gate ikifutiwa usajili wa kuendesha shughuli za bweni.

Akifafanua kuhusu shule ya Coner Stone alisema baada ya ukaguzi na kufutiwa usajili kuanzia mwezi Julai zipo shule ambazo zilikamilisha utaratibu na kurejeshewa usajili, na kwamba hakuna shule iliyoelezwa kufutiwa usajili kwa uongo.

“Kuhusu shule zinazolalamika kutangazwa kimakosa si kweli isipokuwa jambo lililofanyika baada ya kuwapelekea barua kuwataka kutawanya wanafunzi baada ya kufutiwa usajili walikamilisha utaratibu ndipo wakasajiliwa,“ alisisitiza.

Alisema ukaguzi huo wa shule unaendelea katika mikoa yote nchini kwa kuwatumia wakaguzi wa Kanda na watakaobainika watafutwa mpaka watakapokidhi vigezo vinavyotakiwa. 

Hivi karibuni Mcheka alisema kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, waligundua kuwepo kwa shule 35 zisizosajiliwa na kuzifuta na baadaye walizifungia shule nyingine 12. 

Mcheka alisema shule zinaweza kufutwa kwa sababu mbili zikiwamo zilizosajiliwa, lakini zikakiuka vigezo ambapo zikitimiza vigezo zinaweza kuomba upya usajili na kupewa.

“Lakini aina ya pili ni zile ambazo hazijasajiliwa na zinaendeshwa kinyume cha sheria ambazo nazo zikifuata taratibu zikatimiza vigezo zinaweza kupewa usajili,” alifafanua Kaimu Mkurugenzi huyo wa Usajili wa Shule.

Alisema katika kipindi hicho mpaka Agosti mwaka huu baada ya tangazo la kuwataka kusajiliwa shule za awali nne, zile za awali na msingi 105 na sekondari 19, walifika wizarani kwa ajili ya kupata taratibu za usajili ambapo zipo zilizosajiliwa na nyingine kupewa vibali.

Alisema katika usajili, wapo waliokidhi viwango na wengine walipatiwa maelekezo na kupatiwa vibali vya kutumia majengo yaliyopo huku wengine wakipewa vibali vya kujenga majengo ya shule kabla ya kupata usajili. 

Alisema kwa shule walizozifungia, waliwaandikia barua za kuwafungia na kuwataka kuhakikisha wanawatawanya wanafunzi katika shule zilizosajiliwa kwa gharama zao bila kuwaathiri wanafunzi.

Alitaja shule zilizofungiwa kwa kuendesha shughuli zake bila usajili kuwa ni shule ya awali na msingi Must Lead ya mkoa wa Pwani, kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam ni Brainstorm, Pax, Lassana, Grace, Rose Land, Julius Raymod, St Thomas, Mary Mother of Mercy, Noble Sinkonde, Immaculate Heart of Mary, St Columba, Corner Stone, Dancraig, Mwalimu Edward Kalunga, Edson Mwidunda, Gisela, Kingstar, St Columba, Bilal Muslim, Thado, Hocet , Elishadai, Lawrance Citizen, Comrade, Dar Elite Preparatory, Golden Hill Academy na Hekima.

Nyingine ni Pwani Islamic, St Kizito na Rwazi Encysloped za Kagera, Dancraig na Qunu za Pwani, Hellen’s ya Njombe, Joseph ya Arusha, Samandito na Maguzu za Geita. Alizitaja shule za sekondari zilizofungiwa kwa sababu hiyo kuwa ni Hananasif, Elu, Hocet, Safina za Dar es Salaam na Namnyaki ya Iringa.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI