NAMWUNGAMIA MUNGU MWENYEZI NANYI NDUGU ZANGU
Kuhani na wahudumu wakishafika mbele ya madhabahu huinama sana mbele ya Msalaba, lakini kama kuna Ekaristi Takatifu hupiga goti, kisha kuhani huenda kubusu altare. Altare ni meza ya kumtolea Mungu sadaka, lakini ni pia ishara ya Yesu Kristo.Tendo la kubusu altare ni ishara ya kuisalimu na kutoa heshima kwa Kristo.
Ndivyo kila mkristo anavyotakiwa kuinamia
Msalaba aingiapo kanisani. Iwapo mbele
imehifadhiwa Ekaristi anatakiwa kupiga goti ishara ya kumwabudu Yesu katika
tabernakulo; lakini kama hakuna Ekaristi Takatifu, anatakiwa kuinama sana ndipo
kwenye benchi na kusali.
Tafakari
haitolewi
Baada ya kufika mahali pa kuanzia
Adhimisho la Ekaristi, kuhani huanza Adhimisho kwa Ishara ya Msalaba na kisha
huwaamkia Wakristo kama tulivyoeleza katika makala iliyopita. Hapo mwongozo
katika Kanuni ya Misa unasema hivi: Kuhani, au shemasi, au mhudumu mwingine anaweza kuwaeleza waamini nia maalum ya Misa
ya siku hiyo kwa maneno machache kabisa.
Baadhi hutumia nafasi hiyo kutoa
tafakari ya masomo ya Misa ya siku hiyo. Binafsi ninashangaa na kujiuliza:
utaratibu huo umeanzia wapi? Mwongozo unasema ni nafasi ya kuwaeleza waamini nia
maalum ya Misa. Haisemi chochodte kuhusu Masomo ya Misa. Hiyo siyo nafasi
ya kutoa tafakari ya Masomo wala kueleza maisha ya mtakatifu ambaye hukumbukwa
siku hiyo kwamba alizaliwa wapi, mwaka gani, aliishi vipi, karama zake na kadhalika. Kufanya vile ni kinyume cha
mwongozo.
Tafakari fupi ya Masomo hata kama
ingekuwa ya sentensi mbili au tatu hutolewa
baada ya kutangaza Injili. Nafasi hiyo ni ya kuwaeleza waamini nia
maalum ya Misa na aina ya Misa
inayoadhimishwa siku hiyo tena kwa maneno machache sana. Tukumbuke
waamini huwa wamesimama na katika hali hiyo si vema kusikiliza tafakari au historia
ya maisha ya mtakatifu wa siku. Mara nyingi mtoa tafakari hupata kishawishi cha
kuaendelea kutoa tafakari waamini wakiwa wamesimama. Inatupasa sote kujitahidi
kufuata Uongozi wa Kanisa unavyoelekeza, na siyo kufuata matakwa yetu katika
kuadhimisha Liturujia.
Tukiri
dhambi zetu
Kisha kueleza nia ya Misa, Kuhani
huwaalika waamini wote waweze kukiri kwamba ni wakosefu na waweze kusali kwa pamoja sala ya kumwungamia
Mungu na kila mmoja. Tafsiri tuliyoizoea ilisema: Tujute dhambi zetu tupate
kujiweka tayari kutoa sadaka takatifu. Tafsiri hiyo imeachwa na badala yake kuhani husema: Ndugu
zangu, tukiri dhambi zetu ili tupate kustahilishwa kuadhimisha mafumbo
matakatifu. Kuna tofauti kubwa kati ya tafsiri hizo mbili.
Tofauti ya kwanza ni katika uchaguzi
wa maneno. Badala ya neno Tujute
sasa kuhani anasema Tukiri.Neno kujuta linaendana zaidi na
Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Tunapoadhimisha Sakramenti hiyo tunafanya liturujia
ya majuto kisha tunakwenda kuungama dhambi kwa kuhani. Kila Mkristo lazima aziungame
dhambi kubwa zote katika Sakramenti ya
Kitubio na Upatanisho.
Tafsiri mpya inasema: tupate
kustahilishwa kuadhimisha mafumbo matakatifu. Maneno hayo ni muhimu
pia. Ni Roho Mtakatifu anayetuwezesha
kuadhimisha mafumbo matakatifu. Katika
kutenda yale yanayotupasa mbele ya Mungu, daima ni Mungu mwenyewe hutangulia
kwa neema yake kutuhimiza na tufanye na kutuwezesha au kutusindikiza kufanya
vizuri. Mwaliko huo sasa umekaa vizuri zaidi kuliko ule wa mwanzo.
Tufahamu vizuri tendo tunalolifanya
mwanzoni mwa Misa ni la kujiweka tayari kwa Adhimisho la Ekaristi. Mwaliko
anaotoa kuhani anaposema: “Tukiri dhambi zetu ...” unadhihirisha kwamba tendo hili ni
tofauti na lile tunalolifanya katika Sakramenti ya Kitubio na Upatanisho. Tunakaa
kimya kitambo kifupi kutafakari hali yetu ya dhambi. Nafasi hiyo ya unyamavu nayo
ni muhimu sana.
Katika ukimya kila mmoja ajione yupo
mbele ya Mwenyezi Mungu, hujinyenyekea na kujiona yu mkosefu. Hata iwapo Mkristo hana dhambi kubwa, katika unyamavu
huo, kabla ya kuadhimisha mafumbo hayo matakatifu, ajione ni mkosefu. Wakristo huwa wamesimama, na kuhani anaposema “Tukiri
dhambi zetu...” ndipo waamini hupiga magoti na kutafakari.
Kwa bahati mbaya sana, pengine nafasi
hiyo haitolewi kwani wakishapiga magoti,
kuhani huanza mara: “Namwungamia Mungu mwenyezi...” Tunawaomba
makuhani watoe nafasi ya unyamavu hata robo dakika tu na waamini wafahamu
umuhimu wa unyamavu huo ni wa kila mmoja kutafakari dhambi zake, na hali yake
ya dhambi. Mababa wa Mtaguso wamehimiza nafasi hizo zizingatiwe (Hati ya Lit. 30).
Baada ya unyamavu huo kwa pamoja waamini
hukiri mbele ya Mungu na waamini wote waliopo kanisani kwamba ni wakosefu.
Kuhani anaanza: “Namwungamia Mungu mwenyezi.”
Waamini wote huendelea kusali sala hiyo ya kukiri dhambi. Tafsiri ya zamani
ilisema: Nakuungamia Mungu mwenyezi. Kwa kuwa ni tendo la kukiri dhambi
pamoja Sala inaanza “Namwungamia Mungu mwenyezi.”
Tendo ni la kukiri kwamba tu wakosefu; siyo la kuadhimisha Sakramenti ya
Kitubio na Upatanisho. Sakramenti ya Ekaristi haipo kwa ajili ya kuondoa dhambi
kubwa ndivyo tunavyofundishwa katika Katekisimu Katoliki.
Tunasoma hivi: “Ekaristi hutukinga tusitende
dhambi za mauti... Ekaristi haipo kwa lengo la kuondolea dhambi za mauti.
Kuondolea dhambi za mauti ndiyo kazi hasa ya Sakramenti ya Upatanisho. Ekaristi
ni hasa Sakramenti ya wale walio katika ushirika kamili na Kanisa.” Basi tendo
tunalolifanya mwanzoni mwa Misa ni tendo la kukiri dhambi na kujiweka tayari
kwa Adhimisho la Ekaristi.
Kila Mkristo inampasa kusali sala
hiyo ili kukiri mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya waamini wote waliopo kwamba
ametenda dhambi. Mkristo ambaye hufumba
mdomo na hasali tunapasa kumwuliza: Je,
mwenzetu umefika kanisani kufanya nini?
Tuzingatie Matini ya Liturujia.
Kwamba kuhani anaweza kubadili
maneno sehemu mbalimbali katika
kuadhimisha Liturujia ni fursa inayoelekezwa sehemu mbalimbali katika Adhimisho
lenyewe. Hata hivi tuzingatie matini, na kuelewa nini tunaelekezwa. Kwa nafasi
hii kuhani alisema zamani: Tujute dhambi zetu... kumbe sasa anatakiwa
kusema: Tukiri dhambi zetu.
Baba Askofu Salutaris Libena, Askofu
wa Jimbo la Ifakara na msimamizi wa Idara ya Liturujia kitaifa alipotoa mada
katika Kongamano la kitaifa la Ekaristi kule Mwanza aliwasihi makuhani
kuzingatia matini ya tafsiri hii mpya katika kuadhimisha Ekaristi. Kwa namna ya
pekee aliwaomba kuzingatia jambo hilo hapo mwanzoni ambapo mabadiliko ya
tafsiri hayajazoeleka kwa Wakristo wengi,
ili nao wanapofuata katika vijitabu vile ambavyo vimeandaliwa kwa ajili yao
waweze kufuata vizuri.
Kwa nafasi hii basi turudie wito ule
aliotoa Baba Askofu na kwa kweli ndivyo inavyotakiwa kusema kadiri ya tafsiri
na maana ya tendo tunalolifanya. Tukiri dhambi zetu na siyo Tujute
dhambi zetu.
Na Padri Paul Chiwangu
Comments
Post a Comment