Wengi wanaopewa madaraka Tz ni dhaifu
Rais Magufuli: Vita ya uchumi ni mbaya
Askofu: Tunabadilishiwa dhahabu kwa bangili
Mwamalanga: Wabunge waliombeza Rais wasikanyage bungeni
KITENDO cha Serikali kuzuia makinikia (mchanga wa dhahabu)
uliopo kwenye makontena katika Bandari ya Dar es Salaam na sehemu nyingine
nchini usisafirishwe kwenda nje ya nchi na hatimaye kuchunguzwa na kubainika
kuwa na madini yanayotoroshwa, ni funzo kwa Watanzania; Wamesema watu
mbalimbali wakiwamo wasomi na viongozi wa dini huku Askofu Kilaini akisema,
Watanzania wasishangilie kutumbuliwa kwa Profesa Muhongo.
Kutokana na hali
hiyo, Rais John Magufuli, amesema Tanzania iko kwenye vita, huku akisistiza,
“Vita ya uchumi ni mbaya.”
“Kwa ajili ya kazi
hii muhimu ilibidi wajumbe watafutiwe ulinzi maalumu, lakini wapo watu
waliojitokeza kutaka kuingilia uchunguzi huu na majina yao tunayo na wengine tunawajua,”
alisema rais Magufuli muda mfupi baada ya kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda
kuchunguza makontena ya mchanga huo zaidi ya 270 yaliyokuwa yasafirishwe kwenda
nje ya nchi.
Akaongeza, “Kuna
mwingine anajiita profesa wakati yeye ni daktari; alipewa hela mbele ya kamera.
Ninachotaka kusema kwa Watanzania ni kuwa, tupo kwenye vita na vita ya uchumi,
ni mbaya sana.”
Uchunguzi wa gazeti
hili kupitia mazungumzo na vyanzo mbalimbali umebaini kuwa, uchunguzi, ripoti,
mapendekezo na hatua za awali zilizochukuliwa na Rais Magufuli dhidi ya
walioshiriki kufanikisha hujuma hiyo dhidi ya uchumi wa Watanzania, pia vimetoa
fundisho kuwa katika masuala yenye maslahi ya taifa, tofauti za itikadi za
kidini na kisiasa lazima ziwekwe pembeni ili kujenga taifa imara.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti, watu hao wamesema miongoni mwa mambo ambayo ni fundisho kubwa
kwa Watanzania ni kuwa, umaskini wa Watanzania ni wa kujitakia kwa kuwa
miongoni mwa watu wanaofanikisha utajiri wa Watanzania kuibwa na kuliwa na
mkampuni ya wawekezaji wa nje, wamo
Watanzania.
Imebainika kupitia
Ripoti ya Kamati aliyoiunda Rais John Magufuli kuchunguza makontena hayo ya
mchanga wa dhahabu kuwa, madini mengine ya mabilioni ya fedha, yamekuwa pia
yakitoroshwa kutoka Tanzania bila kujulikana.
Kwa mujibu wa
Mwenyekiti wa Kamati hiyo iliyoundwa na kufanya uchunguzi huo, Profesa
Abdulkarim Mruma, madini mengine yaliyokuwa hayajulikani yenye thamani ya kati
ya shilingi bilioni 129.5 na shilingi bilioni 261yalibainika katika makontena
227 yaliyokuwa yasafirishwe kwa mwezi mmoja kabla Rais hajazuia usafirishaji
huo ambao baadhi ya watu waliubeza kuwa utatishia na kuwafukuza wawekezaji.
Askofu Msaidizi wa
Jimbo Katoliki Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini, amesema kuwa ingawa
aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kabla ya Rais kumuondoa madarakani,
Profesa Sospeter Muhongo ameondoka madarakani kwa kuwajibika kwa mujibu wa
nafasi yake, hapaswi kubezwa kwa kuwa naye aliikuta mikataba hiyo.
“Profesa Muhongo
ametumbuliwa kuwajibika, lakini mikataba hiyo aliikuta hivyo, kutumbuliwa kwa
Muhongo sio jambo la kushangilia na badala yake, tunapaswa kuibadili na hapa
Rais ana kazi kubwa kuirekebisha maana tulishajifunga ipo kazi ngumu
kwelikweli, lakini najua Rais yuko makini,” alisema Mhashamu Kilaini.
Alisema fundisho
kubwa analoliona kwa Watanzania kutokana na sakata hili, ni kwamba Watanzania
wengi wanaopewa madaraka ni dhaifu kiasi cha kudanganywa na kutumiwa kwa
manufaa ya mataifa ya nje huku, wakiangamiza taifa lao jambo linalohitaji
maombi zaidi kwa taifa lipate watu waadilifu na wenye uzalendo.
“Tuwe na uzalendo
na tuandae watu wetu kwa ujuzi na maarifa; hii itatusaidia kuepuka watu
wanaotoka Ulaya kutuletea bangili ili sisi tuwape almasi na dhahabu,” alisema.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii
ya Madhehebu ya Dini Tanzania, Askofu William Mwamalanga, alisema moja ya
mafunzo makubwa wanayoyapata Watanzania ni kwamba Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015,
umewapa Rais ambaye ni jemadari jasiri katika kutetea wanyonge na kulinda
rasilimali za nchi.
“Ndipo tunajifunza
kuwa ziara nyingi za nje ya nchi kwa viongozi wakuu wa nchi sio kuwa zinaleta
faida, bali mara nyingi ni hasara maana wengi wanapokwenda huko, wanakutana na
magenge ya wawezekezaji wahuni yanayowapofusha na kuwafanya watumike kuroga
uchumi wa nchi zao,” alisema Mwamalanga.
Ametaka Watanzania
wamuunge mkono na kumtia moyo kwa kufanya maandamano ya kitaifa huku
wakimwombea na kumpa tuzo.
“Rais amesisitiza
kabisa na ndiyo ukweli kwamba, hii ni vita kubwa kati ya madude makubwa ya
uhalifu ambayo ni zaidi ya ujambazi,” alisema.
Kiongozi huyo wa
kiroho alisema kukimbiakimbia kwenda nchi za nje na kujidanganya kwa misaada,
ni kuzidi kuliangamiza taifa kwa kuwa kinachotolewa na baadhi ya mataifa au
wahisani, ni sehemu ndogo kati ya rasilimali wanazolipora taifa.
“Tujifunze
kutokwenda nje kuomba misaada kwa kuwa ukienda, wanakupa sehemu moja kati ya
100; na 99 inayobaki, wanakupora,” alisema na kuongeza, “Huyu ni Rais wa Kwanza
tangu tupate uhuru, kusimamia kwa dhati uchumi wa nchi na hapa, tunapaswa kumpa
tuzo ili hata watoto wetu wajifunze maadili na kuthubutu kulitetea taifa kama
anavyofanya Rais.”
Alisema kutokana na
hali hiyo, mawaziri na watendaji wote waliopita katika wizara hiyo tangu mwaka
1998, wachunguzwe na kuchukuliwa hatua hususani watakaobainika kuhusika au
kuzembea na kulisababishia taifa hasara.
“Hata vyama vyetu
vyote vya siasa visiwe chaka la kuwaficha majambazi wanaoliangamiza taifa na
ninashukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwa ameanza kukisafisha chama
chake,” alisema.
Alisema anatamani
kampuni zote zilizobainika kukiuka makubaliano katika mikataba na kufanya
hujuma kwa taifa, ziondolewe nchini haraka kwa kuwa ni hatari kwa taifa.
“Ninatamani kuona
hata wanasiasa waliokuwa wakibeza uamuzi wa Rais wa kuzuia usafirishaji wa
mchanga wa dhahabu huku wakijua wanatumikia rushwa ili kukandamiza maslahi ya
taifa, wajipime wenyewe kama wanastahili kuendelea kuingia katika Bunge la
Tanzania kwani wamedhihirisha walikuwa wanatetea usaliti na maangamizi kwa
taifa,” alisema.
Akasema, “Wapo
wabunge walikomaa kabisa kumlaumu Rais kuwa uamuzi wake kuzuia mchanga
utaliathiri taifa kwa kulitia hasara na kufukuza wawekezaji… Hao, naomba hata
Bunge kupitia kwa Spika, Job Ndugai, liwajadili na viundwe vyombo vya kuwachunguza
walikuwa wanatetea maslahi gani kama sio kutumikia rushwa.”
“Hapa ninasema kwa
nguvu kabisa kwamba, wale waliotaka kulishawishi Bunge kumuona Rais kama
aliyekosea katika uamuzi wke, wajitoe au watolewe wasiendelee kuingia bungeni
maana walikuwa wanafanya usaliti wanaoujua na wanaojua namna wanavyofaidi
usaliti huo dhidi ya Watanzania wenzao. Nitashangaa sana kama wabunge hao
wataendelea kuwa bungeni.”
Mbunge wa Kigoma
Mjini, Kabwe Zitto alinukuliwa jana akiunga mkono matokeo yaliyobainishwa na kamati
iliyoundwa na rais kuchunguza mchanga wa dhahabu na kusema matokeo ya utafiti
huo ndio rejea sahihi kwa sasa.
“Utafiti unapingwa
kwa utafiti. Kwa sasa Kamati ya Mruma (Profesa Abdulkarim Mruma- Mwenyekiti wa
Kamati) ndio rejea sahihi kwenye suala la mchanga na hivyo nakubali mapendekezo
yaliyomo,” alisema mbunge huyo wa upinzani aliyewahi kuwamo katika moja ya Tume
za kuchunguza mikataba ya sekta ya madini nchini.
Naye Askofu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na
Pwani, Dk Alex Malasusa alisema ripoti hiyo inapaswa kuwafumbua macho
Watanzania katika sekta mbalimbali.
Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana kwa upande wake anasema, funzo
tunalopata Watanzania ni ukweli kwamba tumekuwa tukiwanyenyekea wawekezaji huku
wakitunyonya na alichokifanya Rais ni jambo jipya na la manufaa na linalopaswa
kuungwa mkono na Watanzania wote.
Comments
Post a Comment