Hija nchi Takatifu 2017 yafana
θ Mapadri wahamasishwa kushiriki kwa wingi
ASKOFU, mapadri 51, watawa na walei wamefanya safari ya Hija katika nchi
Takatifu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Padri
mzalendo wa kwanza kupewa daraja hilo Tanzania Bara.
Kundi hilo lililokuwa na mahujaji zaidi ya 90 kutoka majimbo 15 nchini
lilianzia safari yake nchini Misri likiwa limedhamiria kuifuata njia ya Wana wa
Israel kutoka Misri kwenda nchi ya ahadi.
Kundi hilo liliambatana na Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa Mhashamu
Bernadini Mfumbusa ambaye pamoja na mapadri wengine 19 mwaka huu wanaadhimisha
Jubilei ya miaka 25 ya utumishi katika shamba la Bwana.
Mahujaji hao waliowasili nchini Misri tarehe 9 April 2017 waliweza
kutembelea Kanisa la Familia Takatifu ambapo kwa mujibu wa mapokeo Yesu, Bikira
Maria, na Mtakatifu Yosefu waliishi hapo kwa miaka 3 kama wakimbizi kufuatia
tishio la Mfalme Herode kutaka kumwua mtoto Yesu.
Aidha mahujaji hao waliweza kubadilishana mawazo na wakristo wa madhehebu
ya Kikoptic ambao wamekuwa ni kielelezo cha mateso ya wakristo karne hii katika
nchi yao yanayotokana na imani yao. Mahujaji hao waliweza kutembelea piramidi
za mjini Kairo zilizo Gaza nchini humo ikiwa ni moja ya vielelezo juu ya mateso
waliyoyapata Waana wa Israeli wakati wakiwa utumwani Misri.
Kundi hilo la Mahujaji lilisafiri kuelekea Mlima Sinai ikiwa ni hatua ya
pili katika safari hiyo ambapo pamoja na kupanda Mlima Sinai waliweza
kutembelea Monastery ya Mtakatifu Katarina.
Mapokeo yanaeleza kuwa hapo ni mahali ambapo Musa aliweza kushuhudia
kichaka kinachowaka moto bila kuteketea. Wakiwa njiani waliweza kusimama mahali
ambapo pia kwa kadri ya mapokeo ndipo ambapo Mungu aliwavusha Waisrael katika
bahari ya Shamu.
Pamoja na kutembelea mji wa kihistoria wa Petra nchini Yordani mahujaji
waliweza kuona mlima Nebo mahali ambapo Musa kadri ya maandiko alionyeshwa Nchi
Takatifu, nchi ya ahadi kabla ya kufa.
Nchini Israel mahujaji hao walipiga kambi katika mji mdogo wa Bethlehemu,
mahali ambapo Kristo alizaliwa. Sehemu hiyo ya tatu ya ziara iliwafikisha
sehemu zote kuu katika historia ya maisha ya Yesu kadri ya maandiko tangu
kuzaliwa, kufundisha, kufanya miujiza, kuteswa hadi kifo chake.
Padri Wenceslaus Kayera wa Jimbo
Katoliki Ifakara, mmoja wa Wajubilei wa miaka 25 ya utumishi anakumbuka jinsi
alivyoweza kusubiri kwa zaidi ya masaa matatu ili aweze kulifikia Kaburi la
Yesu kutokana na uwingi wa watu kwenye foleni.
Mahujaji hao walipata bahati ya kuadhimisha sadaka ya Misa Takatifu
katika mlima ujulikanao sasa kama Mlima wa Heri (Beatitudes –Mt 5:1-12) na
baadhi ya mahujaji walipata pia nafasi ya kurudia ahadi zao za ndoa mjini Kana
mahali ambapo Kristo alifanya muujiza wake wa kwanza.
Siku ya mwisho kabla ya kurudi nyumbani mahujaji hao waliweza kutembelea
mlima Sayuni, mahali ambapo panaaminika kuwa ndipo Hekalu la kwanza lilijengwa.
Hekalu hilo kwa sasa halipo na mahali pake pamejengwa Msikiti ujulikanao
kama Dome of the Rock. Wayahudi hujikusanya na kusali wakielekea moja ya kuta
za uzio wa Hekalu zilizosalia wakisali na wakiamini kuwa siku moja Hekalu lao
litajengwa tena.
Baadhi ya mahujaji walizungumza na gazeti hili walionyesha furaha yao
hasa kutokana na mlinganisho wa yale waliyokuwa wakisoma katika maandiko na
uhalisia wake waliouona katika safari hiyo. Aidha waliomba kuwa iwepo mipango
maalumu kwa Wakatoliki kuwa wanatembelea maeneo hayo mara kwa mara kadri ya
nafasi.
Naye Askofu Bernadini Mfumbusa katika kuhitimisha ziara hiyo alisema kuwa
ingekuwa ni jambo jema kama mapadri wengi wanapata nafasi ya kutembelea nchi
hizo tatu, ikiwa ni kukamilisha yale ambayo wamejifunza wakiwa mashuleni.
Safari hii iliandaliwa vyema na
kampuni ya Cordial Tours ya mjini Dar es Salaam na kuratibiwa na Mapadri
Wanajubilei wa miaka 25 nchini.
Comments
Post a Comment