“Majimbo yote yawe na tovuti”
KURUGENZI ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) imeshauriwa kuhimiza matumizi ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano katika majimbo yote ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na
kupanua wigo wa Mawasiliano.
Akizungumza na wakurugenzi wa Mawasiliano Jamii
kutoka baadhi ya majimbo Katoliki Tanzania katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Augustino (SAUT) kwenye Semina juu ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(Tehama), pia mbinu za Mawasiliano, Mratibu wa Mawasiliano Jamii wa Umoja wa Wanachama
Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) Padri
Chrisantus Ndaga amesema Kanisa Katoliki bado lina changamoto katika matumizi
ya mitandao ya kijamii hususani tovuti za majimbo.
Padri Ndaga ameyashauri majimbo yote Katoliki nchini
Tanzania kufungua tovuti na mitandao mingine ya kijamii ili kutanua wigo wa
Mawasiliano ndani na nje ya majimbo wakati akiwahimiza wakurugenzi wa Idara za
Mawasiliano Jamii majimboni kuwaendeleza kitaaluma wasimamizi wa Idara hizo ili
waendane na teknolojia ya kisasa katika upashanaji habari.
Padri Ndaga amesema kuwa majimbo mengi ya Kanisa
Katoliki Tanzania hayajazama katika matumizi ya tovuti (website) na baadhi ya
majimbo yamefungua tovuti hizi lakini hayana wataalamu wenye weledi wa
kuzisimamia tovuti hizo pia kuweka habari zinazoendana na muda.
Aidha amesema AMECEA na TEC wamejipanga kuwaelimisha
mapadri, watawa na walei walio katika tasnia ya habari ili wapate maarifa
yatakayowawezesha kutumia mitandao yote ya kijamii ikiwemo ‘whatsap’,
‘facebook’, tweeter’, ‘instagram’ na blogu ambapo kwa sasa kuna jamii kubwa ya
watanzania hususani vijana ambao wanaweza kuinjilishwa katika uinjilishaji
mpya.
Wakichangia maoni yao katika semina hiyo, washiriki
toka majimbo mbalimbali wameipongeza AMECEA na TEC kuona hitaji la
kuyahamasisha majimbo kutumia Tehama na redio kwani wapo watanzania wengi
hawaendi kanisani lakini wanasikiliza sana redio na kufuatilia mitandao ya
kijamii.
Semina hiyo imeandaliwa na Idara ya Mawasiliano ya
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa udhamini wa AMECEA na
kuhudhuriwa na wakurugenzi wa Mawasiliano kutoka majimbo ya Dar Es Salaam,
Mwanza, Shinyanga, Geita, Njombe, Arusha, Tanga, Tabora, na baadhi ya
wawezeshaji kutoka Chuo Kikuu cha
Nairobi.
Aidha Mratibu wa Mawasiliano wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania Bw. Bernard James ameshangazwa na baadhi ya wasimamizi wa
Mawasiliano majimboni kushindwa kuandika habari zinazowagusa wakristo na
wananchi na hivyo kufanya habari za jitihada mbalimbali nzuri zinazofanywa na
majimbo kuisaidia serikali kutoa huduma za kijamii hasa elimu, afya, maji na
ujenzi wa miundombinu kutoifikia jamii.
Bwana Bernard amewaomba wakurugenzi wa Mawasiliano
kutoka majimboni kuhamasisha habari toka majimboni ziandikwe kwa wingi, na
kuunda mfumo mzuri wa usambazaji ili kuliwezesha gazeti hili lifike katika kila
Parokia ili waamini wengi wanufaike na gazeti hilo.
Na Salvatory Magangila na Veronica Modest, Mwanza
wazo zuri sana websites hizo ziwe na matukio yote ya jimbo na pia wakumbuke ku update hizo websites kila siku maana ukiingia website ya jimkoo la dsm ni kituko yani ni kaka imekufa na wana idara ya teknolojia habari na mawasiliano
ReplyDeletesawa kabisa
ReplyDelete