Talaka Kanisa Katoliki hapana
Na Sarah Pelaji
TUME ya Sheria za Kanisa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) imefanya ufupisho wa Barua ya Kitume Mitis Iudex Dominus Iesus (The Gentle Judge, Our Lord Jesus) ya Baba Mtakatifu Fransisko ya Agosti 15 mwaka 2015 ambayo ilifanya mabadiliko katika kanuni zinazohusiana na mwenendo wa kesi za utangazaji batili wa ndoa
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Katibu
Mtendaji wa Tume hiyo Padri Henry Mchamungu, mwalimu katika Seminari
ya Mtakatifu Karoli Lwanga Segerea jijini Dar es Salaam ambaye ni mjumbe katika
Tume ya Sheria za Kanisa nchini akieleza kuwa mabadiliko katika kanuni
zinazohusiana na mwenendo wa kesi za utangazaji batili wa ndoa ni vyema
Maaskofu pamoja na Mavikari Hakimu (Judicial Vicars) kufahamu ili waweze
kushughulikia kesi za ndoa ipasavyo.
Aidha Tume hiyo inayoongozwa na
Mwenyekiti wake Askofu Rogathy Kimaryo na Makamu Mwenyekiti Askofu Michael
Msonganzila, wameoanisha baadhi ya mambo ya kimsingi ya kuzingatia katika barua hiyo kuwa ni pamoja
na Hukumu moja ya ubatili wa ndoa inayotolewa na mahakama ya ngazi ya mwanzo
inajitosheleza. Haihitaji tena kufanyiwa mapitio na mahakama ya ngazi ya pili
na mengine.
Kutokana na Barua hii ya kitume ya Papa
Fransisko, haimaanishi kuwa Baba Mtakatifu ameruhusu talaka, bali amefanya
marekebisho kidogo kwenye kanoni zinazohusiana na mwenendo wa kesi za
utangazaji batili wa ndoa. Kanoni ambazo Baba Mtakatifu amezifanyia
marekebisho, zimekuwepo tangu Mkusanyo wa Sheria Kanoni (Code of Canon Law)
ulipotangazwa na Baba Mtakatifu Yohani Paulo II mwaka 1983.
Amenipa, Kanisa linatambua waziwazi
uwezekano wa kuwepo ndoa ambazo zinafungwa kibatili, na ndiyo maana limeweka
kanoni zinazotawala mchakato wa kutangaza batili ndoa hizo. Ili ndoa iwe
halali, lazima mambo makuu matatu yazingatiwe: a) Ubadilishanaji wa Ukubali wa
Ndoa kati ya Wafunga ndoa wenyewe, b) Kutokuwepo kwa Kizuizi cha Ndoa, na c)
Uzingatiaji wa Utaratibu Kanoni.
Amesema kuwa, endapo ndoa itafungwa
huku mmojawapo wa wafunga ndoa hayupo au mwakilishi wake ili kubadilishana
ukubali wa ndoa, au kuna kizuizi cha ndoa na hakikuondolewa na mtawala mahalia,
au utaratibu kanoni hauzingatiwi, basi ndoa hiyo huwa ni batili.
Kanisa limeweka utaratibu wa kutangaza
batili ndoa kama hizo. Ndoa inapotangazwa batili ina maana kuwa ndoa
inatangazwa kuwa haikuwepo tangu mwanzo, na wala haimaanishi Hakimu mmoja chini
ya mamlaka ya Askofu: Katika ngazi ya mwanzo, Askofu ndiye mwenye mamlaka ya
kumteua hakimu ambaye anapaswa kuwa mklero.
Mkusanyo
wa Sheria Kanuni unaeleza kuwa kesi inayohusu utangazaji batili wa ndoa
iamuliwe na jopo la mahakimu watatu (rejea Kan. 1425, §1 na Mitis Iudex Dominus
Iesus, Kan. 1673, §3). Hakimu ambaye ni mklero lazima asimamie jopo hili,
lakini mahakimu wengine wanaweza kuwa walei. Katika jopo hili la mahakimu, kura
ya wengi inahitajika ili ndoa ipate kutangazwa batili.
Hata hivyo kutokana na upungufu mkubwa
wa wanasheria kanuni na hivyo kuwa vigumu kuanzia mahakama yenye jopo la
mahakimu watatu, Baraza la Maaskofu linaweza kumruhusu Askofu aaminishe kesi za
ndoa kwa hakimu mmoja, ambaye anapaswa kuwa mklero (rejea MSK, kan. 1425, §4).
Kwa kuwa mchakato wa kesi za utangazaji
ubatili wa ndoa mara nyingi umechukua muda mrefu, ndiyo maana Baba Mtakatifu
Fransisko amefanyia mabadiliko kanoni husika, ili mchakato uende kwa kasi
zaidi.
Kwa mfano, hukumu inayotolewa na
mahakama ya ngazi ya mwanzo inajitosheleza, haihitaji tena kufanyiwa mapitio na
mahakama ya ngazi ya pili. Kwa namna hii, mchakato umefupishwa.
Aidha, Baba Mtakatifu ameyataka
Mabaraza ya Maaskofu yawasaidie maaskofu kuangalia ni jinsi gani ya kuchangia
gharama za mahakama ili kupunguza mzigo kwa waamini wenye kesi za ndoa, na pale
inapowezekana michakato ya kesi za ndoa ifanyike bila ya kuwatoza chochote
wenye kesi.
Comments
Post a Comment