Papa Francisko anawashukuru wote waliofanikisha hija yake ya kitume!
Falsafa ya neno asante ni kuomba tena! Kama ilivyo kawaida kwa Baba Mtakatifu Francisko kabla na baada ya hija zake za kitume kwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma, Jumapili, tarehe 14 Mei 2017 alfajiri na mapema, Baba Mtakatifu Francisko amekwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na kukaa mbele ya picha ya Bikira Maria afya ya Warumi katika hali ya ukimya kwa kitambo cha dakika ishirini na baadaye kurejea tena Vatican kuendelea na shughuli zake!
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima nchini Ureno, kuanzia tare 12 hadi 13 Mei 2017, akiwa njiani kurejea mjini Vatican, amewatumia wakuu wa nchi ya: Ureno, Hispania, Ufaransa na Italia, ujumbe wa matashi mema wakati alipokuwa anapita kwenye anga la nchi zao. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno kwa mapokezi na ukarimu wa ajabu waliomwonesha wananchi wa Ureno wakati wa hija yake nchini humo. Anapenda kuwaombea wananchi wote, amani, baraka na furaha!
Baba Mtakatifu alipokuwa anatinga kwenye anga za Hispania, amemtumia salam na matashi mema Mfalme Felipe VI, akiwahakikishia wananchi wote wa Hispania sala zake. Alipoingia kwenye anga la Ufaransa, Baba Mtakatifu amemtumia salam na matashi mema Rais Francois Hollande kwa niaba ya wananchi wote wa Ufaransa, akiwahakikishia sala na maombezi yake.
Alipowasili kwenye anga za Italia, Baba Mtakatifu amemtumia salam na matashi mema Rais Sergio Mattarella wa Italia, akimwelezea kwamba, anarejea kutoka katika hija ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, ambako amebahatika kukutana pia na wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi kulikuwepo na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Italia. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kutekeleza hija hii kama hujaji wa matumaini na amani. Anapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza wasamaria wema wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na wanaoteseka nchini Italia. Anapenda kuwahakikishia wananchi wa Italia sala na sadaka ili kweli Italia iweze kupata ustawi na maridhiano. Amewapatia wananchi wote wa Italia baraka zake za kitume!
Comments
Post a Comment