Kijana akaa kitandani miezi 9 akikisubiri kifo
“Natamani hata siku moja
niweze kukaa au kutambaa hata kujigeuza mwenyewe kitandani, sina fedha ya
matibabu wala ndugu wa kunisaidia, Watanzania nisaidieni.”
Ni sauti ya kijana
Ayubu Julias inayoibua hisia za huzuni na masononeko juu ya maisha yake anavyoteseka kitandani kwa kukosa
matibabu na kupoteza matumaini na ndoto
zake baada ya kupatwa na ajali iliyosababisha kupooza mwili na kukosa matibabu.
Ayubu ni kijana
mwenye umri wa miaka 30 anaishi katika kijiji cha Baibo, kata ya Msua Manispaa
ya Sumbawanga na anapaza kilio chake kwa watanzania aweze kusaidiwa kutokana na
kukosa pesa za matibabu baada ya kuteguka uti wa mgongo na amekuwa mtu wa
kulala kitandani na kugeuzwa kwa zaidi ya miezi 9 sasa.
Gazeti la kiongozi
limemtembelea Ayubu nyumbani kwao na kufanya nae mazungumzo ambapo kwa
masikitiko makubwa Ayubu anaeleza
historia ya maisha yake na kuomba msaada kwa watanzania na watu wote walio na
moyo wa kumsaidia. Na anaanza kwa kusema:
“Ndugu yangu,
nasubiri miujiza ya mungu tu!! Maana kama aliweza kuyatenda haya kwa Ayubu wa
nchi ya Usi niliebatizwa kwa jina lake ambaye alikuwa mkamilifu na kumcha
Mungu.”
“Naitwa Ayubu
Julias Simchindo, nina umri wa miaka 30 nimezaliwa wilayani Chunya mkoani
Mbeya. Nimelelewa zaidi na baba yangu mzazi kwani mama yangu alifariki nikiwa
na umri wa miaka miwili tu hivyo sikuweza kuyashiba mapenzi na malezi ya mama
katika utoto wangu.” Anaeleza kijana huyu.
“Baba yangu alikuwa
akijihusisha na ujasiliamali wa kufanya biashara ndogondogo zaidi alijishughulisha
na uvuvi wa samaki ambapo alikuja Mkoani
Rukwa kuvua na kupeleka samaki Mbeya ambapo mnamo mwaka 1995 alituhamishia
makazi katika mji wa Tunduma ambapo alitupangia nyumba mimi pamoja na dada
yangu na tukawa wakazi wa Tunduma kwa muda ambapo baba alikua akija kutuona kila baada ya mwezi
mmoja au zaidi.
Mnamo mwaka 1996 ilikuwa ndio ukomo wa baba
yetu kuja kutuona na ikawa ni mwisho
wetu kuiona sura ya baba machoni petu maana mpaka leo hii simjui baba wala
hatujui ni wapi alipopotelea, ni mzima au marehemu sijui ila limebaki ni fumbo
lisilo na majibu.
Namshukuru mama
mwenye nyumba tulipokuwa tukiishi ambapo alitambua kama tumetelekezwa na
akaamua kutufanya ni wanae na kuanza kuishi kama watoto wa pale na si wapangaji
tena ambapo mama huyu aliamua kututafutia ndugu zetu na kubaini kuwa asili ya
baba yetu mzazi ni Rukwa maeneo ya
Karuko ambapo aliweza kumpata baba yetu mkubwa na kutukabidhi kwake ingawa dada
yangu alibaki Tunduma kwani aliolewa huko ndipo nilipotambua ukoo wetu.
Haikupita muda mrefu
baba yangu mkubwa alifariki dunia lakini mwanae mkubwa ambaye ni kaka yangu
alinichukua na kuanza kuishi nae maeneo ya Majengo Manispaa ya Sumbawanga
ambapo nikiwa na miaka 13 mnamo mwaka 2000 aliniandikisha shule ya msingi
Jangwani ambapo baadaye waliigawa shule zikawa shule mbili nyingine ikiitwa
Kiweru hivyo nilihitimu katika shule ya msingi Kiweru.
Nilihitimu, nikafaulu na kuchaguliwa kujiunga
na elimu ya sekondari katika shule ya Kizwite Sekondari Manispaa ya Sumbawanga
ambapo nilihitimu kidato cha nne mwaka 2010, hata hivyo sikuweza kufanya vizuri
katika masomo yangu ambapo nilianza maisha mapya ya utafutaji.
Baada ya kuhitimu
elimu ya sekondari, nilianza kuishi na mama yangu mkubwa ambaye baba yangu
mkubwa alimuacha na kuanza kumsaidia baadhi ya kazi na mahitaji madogomadogo
kwani amekuwa hajiwezi.
Nilianza kujishughulisha na biashara ya kuuza
karanga na baadaye kuuza picha kubwa za ukutani kama vile za Yesu, wasanii,
timu za mpira na nyinginezo ambazo ziliweza kuniingizia kipato na kuweza
kuendesha maisha yangu.
Nilianza kupeleka
bidhaa zangu za picha katika maeneo ya minada mbalimbali ambapo mafanikio
yalizidi kunitia faraja na nilianza kujikimu mimi na mama yangu mkubwa na
nikaanza kufikiri maisha ya kutafuta mwenza wa maisha yangu.
“Looo! Mipango si
matumizi na binadamu unapanga lako kumbe Mungu nae ana makusudi juu yako,
ilikua ni tarehe 17/ 07 /2016 ambapo ndoto zangu za maisha zilizima na mpaka
sasa najiozea huku najiona.” Anaeleza Ayubu huku machozi yakimbubujika.
Tulikuwa tukitokea
kipande Sumbawanga Manispaa tunaelekea wilayani Nkasi kijiji cha Kirando
tulipopatwa na ajali mbaya sana ya gari ambapo binafsi nilipoteza fahamu na
baada ya kurejea katika hali ya kujitambua nikiwa hospitali ya mkoa wa Rukwa nilijikuta siwezi kuinuka, kutembea,
kutambaa, kukaa wala kujigeuza kwani sehemu ya mwili wangu kuanzia miguuni hadi kiunoni hakukuwa na
mawasiliano tena mpaka leo ambapo nasubiri miujiza ya Mungu na katika ajali ile
mmoja wetu alipoteza maisha palepale na 40 tulikuwa majeruhi ingawa mimi ndio
nilikuwa muathirika mkubwa zaidi.
Mganga Mkuu wa
hospitali ya mkoa wa Rukwa alisema kuwa hakuna uwezekano wa kimatibabu wa
kunisaidia kurejea katika hali ya
kawaida na kushauri nipelekwe Muhimbili
ambapo nawashukuru wafanyabiashara wa mnadani waliweza kunichangia nauli
na kufanikisha kupelekwa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
Baada ya kufika
kule nilipigwa xray, na sitscanner ambapo sikuweza kufanyiwa upasuaji wowote
kwani kuna kidonda ambacho kipo maeneo ya uti wa mgongo na badala yake kupumzishwa
wodini na kutakiwa kuponesha vidonda ndipo nifanyiwe upasuaji kwa baadaye na
wakanitaka nirudi nyumbani mpaka tarehe 28/11/2016 kwa ajili ya kufanyiwa
upasuaji na matibabu mengine.
Sijaweza tena
kurudi kwenye matibabu wala upasuaji kwa sababu sina fedha wala mama yangu hana
fedha ya kunisafirisha kwenda Muhimbili hata masharti ya chakula niliyopewa
imekuwa ni changamoto maana hana uwezo
wa kunihudumia naye anasumbuliwa na ugonjwa wa Athma kwa muda sasa wala hana
uwezo wa kuzalisha anasubiri misaada ya watu na ndugu ndipo anihudumie, na
wakati mwingine nadhani Mungu atende analoliweza juu yangu,” Anasema Ayubu na
kuongeza kuwa;
“Natamani hata siku
moja niweze kukaa au kutambaa hata kujigeuza mwenyewe kitandani lakini nahisi
ni ndoto za mchana kwani gharama za matibabu na nauli ya kunifanikisha kufika
Muhimbili ni zaidi ya 2,000,000 ambapo sina hata ndugu mwenye uwezo wa
kunisaidia, hivyo nipo naoza bila kujua hatima ya maisha yangu ingawa najihisi
vichomi sehemu ya miguu yangu tofauti na nilivyokuwa mwanzo.”
Kijana Ayubu anahudumiwa na mama yake mkubwa ambaye
naYe amekwisha kuzeeka huku naye akisumbuliwa na Athma wakishirikiana na dada
yake.
Na anahitaji msaada
wa hali na mali ili kuweza kumsaidia kupata matibabu angalau aweze hata kukaa
au kujigeuza mwenyewe na kujihudimia katika huduma za haja, kwani kwa zaidi ya miezi 9 sasa amekuwa ni mtu wa
kulala kifudifudi tu na hajui hatima yake katika kupata matibabu.
Kwa
maelezo au msaada wowote wasiliana na dada yake kwa simu namba. 0758216017
Comments
Post a Comment