Mwalimu Mkuu asakwa akituhumiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi Mbeya
Thompson Mpanji, Mbeya
JESHI la Polisi mkoani Mbeya linamsaka Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Msingi Matwiga iliyopo katika Kijiji na Kata ya Matwiga,
Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya Scola Mwasaga [38] kwa tuhuma za kusababisha
kifo cha mwanafunzi wa darasa la kwanza baada ya kudaiwa kumfungia katika kasiki ya
kutunzia mitihani.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi Dhahiri Kidavashari amesema tukio
hilo limetokea Mei 8 majira ya saa 4:30 asubuhi katika Kata ya Matwiga, Tarafa
ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya ambapo mwanafunzi aliyefahamika kwa jina la Daud Kaila [11]
alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa katika Zahanati ya Matwiga.
Kamanda
Kidavashari amesema kuwa awali inadaiwa
kuwa marehemu alifikishwa shuleni hapo majira ya saa 4:00 asubuhi na baba yake
mzazi aitwaye Jordan Kaila [43] Mkazi wa Matwiga kutokana na kuwa mtoro kwa
mwezi mmoja na nusu na ndipo Mwalimu
huyo alimuamuru Baba wa mwanafunzi huyo amchape viboko vitatu makalioni na alitekeleza adhabu hiyo.
Kamanda
huyo amefafanua kuwa mara baada ya adhabu hiyo, Mwalimu Mkuu alimfungia
mwanafunzi huyo pamoja na mwanafunzi mwingine ambaye ni mtoro aliyefahamika kwa
jina la Felix Samweli [13] mwanafunzi wa darasa la 4 kwenye kasiki ya kutunzia
mitihani iliyopo ofisini kwake.
“Baada ya
muda mfupi kupita na kasiki kufunguliwa, mwanafunzi huyo wa darasa la kwanza
alikuwa hawezi kupumua vizuri pamoja na mwenzake hali iliyosababisha kukimbizwa
katika Zahanati ya kijiji kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini ilibainika kuwa
Daud amepoteza maisha,” amefafanua
Kamanda huyo.
Naibu
Kamishna wa Polisi Kidavashari
amebainisha kuwa Mwanafunzi mwenzake alipata huduma ya kwanza na kurejea
katika hali yake ya kawaida ambapo
kutokana na tukio hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Scola alikimbia na msako
unaendelea na kwamba chanzo cha kifo ni kukosa hewa na upelelezi unaendelea.
Kamanda
Kidavashari ametoa wito kwa walimu, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuepuka
kutoa adhabu kali kwa watoto wadogo kwani zinaweza kusababisha madhara makubwa
ikiwa ni pamoja na kifo na kushauri kutoa adhabu zitakazowafundisha watoto na
kuwajenga katika misingi na ustawi mzuri katika makuzi yao huku akiomba jamii
kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili wakamatwe na kufikishwa
katika vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
Wakati huo
huo, Jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 43 raia kutoka
nchini Ethiopia wakiwa kwenye gari lenye
namba za usajili T.155 AZU aina ya Toyota Canter, wilayani Mbarali, mkoani
Mbeya na kwamba dereva wa gari lililowabeba raia hao aliyefahamika kwa jina la Zakayo Elias, mkazi
wa Makambako alikimbia baada ya tukio hilo na juhudi za kumtafuta zinaendelea
Katika
tukio jingine, Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa
jina la Julius Mathias [28] Mkazi wa Uyole akiwa na Bhangi kete 11 sawa na
uzito wa gramu 55.
Kamanda
Kidavashari amesema tukio hilo limetokea Mei 8 mwaka huu majira
ya saa 4:00 usiku huko Stendi Kuu ya Uyole, Kata ya Igawilo, Tarafa ya Iyunga,
mkoani Mbeya baada ya askari kufanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa
huyo ambaye amedai ni muuzaji na
mtumiaji wa bhangi na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi
kukamilika.
Comments
Post a Comment