Wasiovaa nguo za heshima kanisani waonywa

WAAMINI wakristo nchini wameaswa kuvaa mavazi ya heshima wawapo katika ibada ama katika jamii ili kuondoa fikra potofu kwa jamii inazowazunguka.
Padri Kalole wa Kanisa la Kitope lililopo Kaskazini Unguja ameyasema hayo katika ibada ya jumapili ya tatu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Mt. Joseph.
Amesema endapo waamini watakuwa na heshima katika mavazi yao basi wataondosha fikra mbaya kutoka kwa jamii inayowazunguka na pia itasaidia waamini wengine kusali kwa amani bila kuwahukumu wenzao kutokana na mavazi yao.
Padri Kalole amesisitiza kuwa ni busara kuvaa vizuri kwa sababu hakuna dini inayoruhusu kuvaa mavazi yasiyo ya heshima hususani katika ibada huku akisema kuwa hali hii inapaswa kuwa kwa kipindi chote na siyo kipindi cha Kwaresima tu.
Naye Katibu wa vijana wa parokia ya Mjini Methew Mathoyo amesisitiza kuwa vijana ni  viongozi wa kuvaa mavazi yasiyokuwa na adabu na heshima, hivyo wajirekebishe la sivyo watakuwa hawaruhusiwi kuingia kusali kwa sababu watakuwa wanasababisha usumbufu kwa wenzao wanapokuwa katika ibada.
Baadhi ya vijana wakitoa mchango wao kuhusu baadhi ya vijana wenzao kuvaa mavazi yasiyokuwa na heshima wameshauri litengenezwe bango litakaloonesha mavazi ya kuingilia kanisani na yale yasiyokubalika ambapo vijana wote wameliafiki wazo hilo.
Pia wameshauri zitafutwe khanga kwa wageni wanaokuja Zanzibar kutalii ambao mara nyingi huvaa mavazi ambayo hayajazoeleka kwa jamii ili waweze kusitiriwa na khanga hizo zitakazonunuliwa na vijana hao na kuvaliwa wakati wa ibada.
Hata hivyo vijana wa parokia ya Mjini walimalizia kwa kusema kuwa ni vyema kuwa na ubunifu katika kutafuta ajira kwa upande wao na siyo kusubiri kuajiriwa hasa kwa kuanzisha mradi wowote ili uweze kuwasadia katika michango midogomidogo ya kuliwezesha Kanisa na kuwasadia  watu wengine wasiojiweza.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU