‘Tutapata kila kitu kupitia Maria’ Katibu Mkuu TEC
WAAMINI nchini wameaswa kusali, kujikabidhi na kujiweka wakfu kwa moyo Imakulata wa Bikira Maria kama njia pekee ya kutafuta amani ya mtu binafsi, familia, jumuiya, Kanisa na Taifa.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padri Raymond Saba katika homilia
aliyoitoa wakati wa adhimisho la kilele cha Yubilei ya miaka 100 tangu Bikira
Maria alipowatokea watoto wa Fatima, Lucia, Fransisko na Yasinta, adhimisho
lililofanyika katika Parokia ya Msimbazi, Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam.
Padri Saba amesema kuwa ikiwa Mungu
alimuona Maria kuwa njia ya kuwafikia wanadamu ulimwenguni, kwa nini wanadamu
wasimtambue na kujikabidhi kwake ili awapeleke mbinguni, huku akiwataka waamini
kutoona aibu kusali sala ya Rozari Takatifu.
“Salini rozari kwa kuwa ni chombo
kitakacholeta amani duniani. Tusali rozari kila siku amani itarudi duniani,
amani inayoanzia kwenye nafsi zetu. Kama malaika alitoka mbinguni akasema
‘Salamu Maria’ kwa nini mimi na wewe tuone aibu kusali” amehoji Padri Saba.
Aidha ameeleza kuwa moja ya maagizo ya
Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima aliwataka kufanya malipizi kwa ajili
ya dhambi za dunia, hivyo ametumia fursa hiyo kuwakumbusha waamini kuwa tayari
kujitoa sadaka kwa ajili ya wadhambi na kuziombea roho nyingi zinazoenda motoni
kwa kukosa waombezi.
Amewaasa waamini kuwa imara katika
imani kwa kuwa watu wengi wanaacha ukatoliki na kwenda kuhangaika kwenye
madhehebu mengine wakitafuta uponyaji, huku akisema kuwa teolojia ya mateso na
msalaba imepoteza maana yake kwa waamini wengi.
“Bikira Maria aliwataka watoto wale
wafanye malipizi pale alipowauliza. ‘Je mpo tayari kujitoa ili mpate mateso ya
kila aina kwa ajili ya kulipia dhambi zenu na ulimwengu na moyo Imakulata
unaodhalilishwa?’ Watoto hawa wadogo kabisa walikubali. Kwetu sisi teolojia ya
msalaba hatuipendi hata sisi wakatoliki. Ndiyo maana tunaacha ukatoliki kwa
kutafuta uponyaji. Tungependa kuwa na Pasaka bila Ijumaa Kuu,” ameeleza Padri
Saba.
Kwa nini Mama Maria atokee duniani tena
1917?
Akielezea nia ya kufanya Yubilei hiyo
Padri Saba amesema kuwa waamini wanaalikwa kumrudishia Mungu shukrani kwa
kuwapatia Bikira Maria ambaye haoni fahari tu kukaa mbinguni wakati huku
duniani mambo hayaendi sawa, na hivyo anashuka kuwasaidia waamini wafuate njia
iendayo kwa Mungu.
Pia ameeleza kuwa mwaka 1917 ambao Mama
Maria alitokea huko Fatima, ni mwaka wenye sifa ya pekee katika historia ya
ulimwengu, ambapo ni katika mwaka huo waprotestanti waliadhimisha miaka 400
tangu Martin Luther alipoanzisha uprotestanti uliosisitiza kuwa imani peke yake
inatosha.
“Bikira Maria anapotokea anaagiza watu
wasali, wafunge, wafanye toba na hija, na hivi anathibitisha kinachosemwa na
Yakobo kwamba imani bila matendo ni bure. Lakini pia mwaka 1917 ndipo
Freemasons walikua wanaadhimisha miaka 200 tangu waanze shughuli zao huko
London Uingereza,” amesema.
Aidha ameongeza kuwa mwaka 1917 ndipo
mapinduzi ya Urusi yalifanyika na hapo ukomunisti ukashika hatamu na kuteketeza
imani ya kikristo, hapo ndipo makanisa yakavunjwa, mapadri na maaskofu
wakafungwa. Pia amebainisha kuwa, mwaka 1917 ndipo Taifa la Marekani
lilipoingia katika vita kuu ya kwanza ya dunia, na kushuhudia mvutano mkali
baina ya Urusi na Marekani.
“Ni katika mazingira haya ndipo Bikira
Maria anakuja na kutoa ujumbe kwamba watu wasali ili amani irudi duniani,”
ameongeza.
Comments
Post a Comment