Askofu Minde awataka waamini Kahama kuombea miito

Na Patrick Mabula, Kahama,


WAAMINI wa Jimbo Katoliki Kahama wametakiwa kuombea miito mitakatifu kwa Mwenyezi Mungu ili kupata mapadri na watawa kutoka kwenye familia zao kwani wanahitajika ndani ya Kanisa.
Wito huo umetolewa na Askofu wa jimbo Katoliki Kahama, Mhashamu Ludovick Minde katika misa takatifu  iliyofanyika hivi karibuni ya Mchungaji Mwema  na kuombea miito katika parokia ya Familia Takatifu, Kagongwa jimboni hapo.
Amesema kila muamini anapaswa kujiunga katika vyama vya kitume vilivyopo  ndani ya Kanisa vinavyowasaidia waamini kuishi kwa imani kiroho, sala na maadili mema juu ya kusaidia kupata miito ya Upadri na Utawa toka kwenye familia zilizo bora kiimani.
 Askofu Minde amewaalika waamini kusali siku zote kuombea miito mitakatifu ya Upadri na Utawa kwa neema ya Mungu inayopatikana kwenye familia zao kutokana na kuhitajika ndani ya Kanisa.
“Miito ya Upadri na Utawa inapatikana kwenye familia za imani za sala, matumaini, maadili mema ya kiinjili, lazima tuwape malezi bora watoto wetu na kuwatengenezea mazingira ya kupata miito hiyo,” Amesisitiza.
“Kuunda miito  mitakatifu  tunahitaji   sala  na kutengeneza mazingira  bora  ya  kiinjili  toka  kwenye familia za  waamini  kwa kusali na kuomba neema ya Mungu atujalie kupata Mapadri na Watawa kwa umuhimu wao ndani ya Kanisa.”
 Amesema malezi mema ya imani, kiroho, sala na matumaini katika familia zetu kwa  kushirikiana na  Kanisa  yanapaswa kuwa endelevu kwa sababu kutasaidia kupata miito mitakatifu, makatekista na viongozi bora kwenye  parokia  na  miongoni mwa jamii. 
Aidha katika misa hiyo ilikwenda sambamba na harambee ya maendeleo ya Jimbo Katoliki Kahama ya kiroho na kimwili  katika kufanikisha ujenzi wa chuo cha makatekista cha jimboni hapo ambapo jumla ya shilingi milioni 86 zilipatikana kwa lengo la kufanikisha kazi hiyo.  


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI