‘Tafsiri ya ndoa na talaka inapotoshwa’ Ask Rwoma

n  Na Pascal Mwanache
KATIKA kipindi hiki Kanisa Katoliki Tanzania Bara linaposherehekea Yubilei ya miaka 150 ya uinjilishaji, tathmini ya utume wa walei nchini imetolewa huku changamoto zinazoukabili ukristo zikiwekwa bayana.
Akizungumza na gazeti Kiongozi katika mahojiano maalum ya kufanya tathmini ya utume wa walei nchini katika kipindi cha miaka 150, Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Desderius Rwoma amesema kuwa ndoa na talaka ni baadhi ya mambo yanayokosa tafsiri sahihi kwa waamini wengi, hali inayosababisha changamoto mbalimbali katika utume wa walei.
Amesema kuwa maandalizi ya kuingia katika Sakramenti ya ndoa yamegubikwa zaidi na hisia za kimwili kuliko maandalizi ya kiroho, hali inayopelekea  neno ‘kusubiri’ kuwa msamiati kwa wachumba wengi wanaotarajia kufunga ndoa.
“Katika Kanisa kuna ongezeko la waamini wanaofunga ndoa, jambo hili ni la kupongezwa. Lakini hoja ya msingi siyo kufunga ndoa, bali namna ya kudumu katika ndoa. Tunashuhudia kukithiri kwa ndoa ambazo siyo ‘fresh’, ambazo unakuta wahusika wameshaishi pamoja kwa muda mrefu ndipo sasa wanaamua kufunga ndoa. Sasa kwa nini watu waingie kwanza kwenye dhambi halafu ndipo wafunge ndoa?” amehoji Askofu Rwoma.
Ameongeza kuwa watu wanaoingia katika ndoa baada ya kuishi pamoja kwa muda mrefu husababisha hata watoto wao wanaowapata katika mahusiano hayo kucheleweshwa kubatizwa na hivyo kuwakosea haki zao. Aidha amebainisha kuwa kukosekana kwa  subira kwa wachumba wanaojiandaa kuingia katika ndoa hupelekea kukithiri kwa dhambi na wachumba kuachana kabla ya kutimiza azma yao.
“Kila mtu anapokutana na mwenzake wa jinsia tofauti bila kufunga ndoa, anakuwa ametenda dhambi. Sasa hebu jiulize, kama wachumba hawa wakikaa zaidi ya mwaka mmoja katika hali hiyo watakuwa wametenda dhambi mara ngapi?” amehoji.
Ametaja changamoto nyingine inayowakabili vijana wanaojiandaa kufunga ndoa kuwa ni kutotenga muda wa kutosha wa kuchunguzana na kufahamiaka, badala yake wanaharakisha katika kutenda dhambi. Ameongeza kuwa vijana wengi hawatafuti ushauri wa wazazi, viongozi wa dini na watu wa mfano katika ndoa pale wanapojiandaa kufunga ndoa, hivyo kutetereka kirahisi wanapokutana na changamoto mbalimbali.

Ndoa mseto
Akielezea kuhusu wachumba wanaotaka kufunga ndoa huku wakiwa katika dini tofauti, Askofu Rwoma amesema kuwa ni kweli Kanisa linaruhusu ndoa za namna hiyo iwapo tu kuna sababu maalum na za kweli za kufanya hivyo.
Hata hivyo ameweka wazi kuwa ndoa za namna hiyo zina changamoto zaidi kuliko ndoa za kawaida, huku changamoto kubwa ikiwa ni kugawanyika kwa watoto na kukosa msingi mmoja.  Amewataka vijana kujipa muda wa kutosha wa kujitathmini kabla ya kuingia kwenye ndoa kwa kuwa wengi huangukia kwenye ndoa mseto kutokana na kukosa muda wa kutosha wa kujitathmini.
“Nashindwa kuelewa, yaani unakuta kijana anaomba kufunga ndoa na mtu wa dini tofauti. Ukimuuliza sababu anakuambia eti siku chache kabla ya kufunga ndoa ndiyo amejua kuwa mwenza wake ni wa dini tofauti. Hii ni dalili kwamba vijana hawapati muda wa kutosha wa kuchunguzana” amesema.

Vipaumbele na maandalizi ya ndoa
Askofu Rwoma ametahadharisha juu ya hali inayoendelea kushamiri kila kukicha ambapo vijana wengi huingia kwenye mahusiano kwa kuangalia viashiria vya nje kama vile mali, fedha, ajira na umbile, badala ya kujikita katika vipaumbele vya kiroho.
“Wasichana wengi sasa unakuta wanatafuta wanaume wenye ajira, yaani ukishakuwa na ajira tu basi wanakuja wenyewe. Hapo mbio mbio utasikia wakiharakisha ndoa” ameeleza.
Kwa upande wa maandalizi ya ndoa amewataka vijana kutenga muda wa kutosha kujifunza katekesi ya ndoa badala ya kuishia kwenye maandalizi ya zimamoto. Amewataka watafute fursa za kuijua katekesi ya ndoa kupitia semina mbalimbali za ndoa, kuwatafuta mapadri, kujisomea vitabu na matini yanayoelezea katekesi hiyo.

Mafanikio utume wa walei nchini na changamoto
Akielezea mafanikio ya utume wa walei nchini, Askofu Rwoma amesema kuwa kwa kiasi kikubwa waamini wamelinda imani katoliki inayodhihirika katika ongezeko la waamini. Pia amesema kuwa waamini wakatoliki ni wengi zaidi, kama dhehebu linalojitegemea kwa upande wa wakristo.
Amepongeza vyama vya kitume ambavyo vinafanya kazi nzuri, huku akitoa mfano wa chama cha wakristo wanataaluma (CPT) ambacho hujikita katika kuelimisha watu wajiandikishe kupiga kura na kuhamashisha upigaji na upigiwaji kura kwa wananchi katika nyakati za kampeni.
Pia amepongeza kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha walei cha Idori Bakanja, ambacho kimejengwa kwa nguvu za walei wenyewe.
“Tunawapongeza pia kwa kuchagiza miito hasa ya utawa na upadri, ndiyo maana tunaona mafanikio makubwa ya ongezeko la vijana wanaojiunga na seminari kuu” amesema.
Akielezea changamoto za utume wa walei, Askofu Rwoma amesema kuwa kuzama katika malimwegu kuliko kuyatakatifuza ni moja ya changamoto hizo, hivyo kuwataka waamini wajikite katika maisha ya kiroho zaidi.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI