Mapinduzi makubwa kwenye muziki mtakatifu kufanyika
Na Pascal
Mwanache, Dar
θ Katiba ya kwaya Taifa mbioni kukamilika
θ Bodi ya walimu wa muziki wa Kanisa kuundwa
Katika jitihada za kutunza hadhi ya muziki
mtakatifu wa kanisa, mapinduzi makubwa yanatarajiwa kufanyika ikiwa ni pamoja
na uundwaji wa katiba ya kwaya ya taifa, uundwaji wa bodi ya muziki wa Kanisa
na uwepo wa tovuti maalum kwa ajili ya kukusanya nyimbo zilizopitishwa kwa
ajili ya matumizi ya kiliturujia.
Hayo ni baadhi ya maazimio ya Kamati ya
Taifa ya Muziki Mtakatifu kupitia Kamati ya Taifa ya Liturujia, ambapo kwa muda
mrefu zimekutana kutathmini hali ya kupungua kwa hadhi ya muziki mtakatifu
kutokana na watunzi na wanakwaya kuwa na uelewa mdogo wa teolojia na elimu ya
muziki huo.
Katika mkutano wao hivi karibuni, wajumbe
wa kamati ya muziki mtakatifu wamepitia rasimu ya katiba ya kwaya ya taifa,
ambayo ndani yake inataja uundwaji wa bodi ya walimu wa muziki ya Taifa ambayo
pamoja na mambo mengine itahusika kuratibu mambo yanayohusu walimu na ualimu wa
muziki wa Kanisa.
Kiini cha mapinduzi hayo
Akifungua rasmi mkutano huo, Askofu wa
Jimbo Katoliki Ifakara na Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania, Mhashamu Salutaris Libena amesema kuwa muziki mtakatifu kama
moja ya nguzo 10 za liturujia umevamiwa kiasi cha kuhatarisha utakatifu wake,
hivyo ni lazima jitihada za makusudi zifanyike kuunusuru muziki huo.
“Muziki wetu ni lazima uwe mtakatifu kwa
sababu ni sehemu ya liturujia. Tangu zamani mafundisho mengi yamewekwa kwenye
muziki. Hii itukumbushe kuwa sisi tumeitwa na kutumwa kuinjilisha na
kutakatifuza, tuweze kuwagusa watu ili wamgeukie Mungu. Lakini kwa sasa uwanja
wa muziki mtakatifu umevamiwa sana, ikiwa ni mbinu za shetani kushambulia
yaliyo mema. Lazima vita hii tuishinde” amesema Askofu Libena.
Aidha Askofu Libena ambaye aliongoza
mkutano huo, ametaja baadhi ya changamoto zinazoukabili muziki mtakatifu kwa
sasa kuwa ni pamoja na wanakwaya kutoelewa ni nini utume wao, wanakwaya
kutoshiriki kikamilifu Sakramenti mbalimbali hasa Ekaristi Takatifu, kuimba
nyimbo kwa nia ya kuburudisha badala ya kuinjilisha.
“Biblia ina maneno mengi na mazuri, lakini
ajabu watunzi wanatumia maneno ya mtaani, ninyi watunzi maneno yenu mnayatoa
wapi? Mnatunga nyimbo zenu mkiwa katika hali gani na mkiwa wapi? Unafika muda
wa kukomunika wanakwaya wamekaa tu wanaimba. Tunapomtumikia Mungu vizuri
tunatekeleza kile alichotuitia, ole wetu tusipoihubiri Injili” ameongeza.
Katika jitihada za kuepukana na changamoto
zinazoukabili muziki mtakatifu, Kamati ya Muziki Mtakatifu ya Taifa iliazimia
kuandaa rasimu ambayo itakuwa katiba na kutumika kwa kwaya zote nchini.
Mchakato wa kuandaa rasimu hiyo ulianza mwaka 2016 ambapo kamati maalum
iliyojumuisha watafiti, wataalamu wa muziki wa Kanisa, Wanasheria wa Kanisa,
mapadri na watawa na wataalamu wa sayansi ya jamii iliundwa na kuanza kazi
yake.
“Rasimu pia inapendekeza kuundwa kwa Bodi
ya walimu wa Muziki wa Kanisa, ambayo itafanya kazi ya kuratibu masuala
yanayohusu walimu na ualimu. Pamoja na kazi nyingine, bodi hiyo itaamua ili mtu
aitwe mwalimu wa muziki wa Kanisa anatarajiwa awe namna gani. Pia itahusika
kuratibu na kuandaa madarasa ya Muziki Mtakatifu kadiri ya silabasi ya Baraza
la Maaskofu” ameeleza Bernadin Mukasa, mmoja wa wajumbe walioshiriki kuaandaa
rasimu hiyo.
Rasimu hiyo inapendekeza kuwa na Utume wa
Kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA), huku ikipendekeza somo wa utume huo akiwa
ni Mtakatifu Sesilia, na salamu itakayotumika ni ‘Tumwimbie Bwana: Katika Roho
na kweli’.
Swahili Music Notes kuwa mali ya Kanisa
Katika hatua nyingine ya kuendelea kuupa
hadhi yake muziki mtakatifu, kamati ya muziki pia imeafikiana kuifanya tovuti
yenye mkusanyiko wa nyimbo mbalimbali za kanisa inayojulikana kama Swahili
music notes, kuwa chini ya usimamizi wa kanisa, ili kuboresha yanayofanywa na
tovuti hiyo.
Askofu Libena ameeleza kuwa utayari wa
mwanzilishi wa tovuti hiyo kuikabidhi kwa Kanisa utasaidia uhakiki wa kila
wimbo utakaoingizwa katika tovuti hiyo pamoja na zile zilizopo ili kuepusha
makosa ya kiteolojia yaliyomo.
Kwa upande wake mwanzilishi wa tovuti
hiyo, Bw. Terence Silonda amesema kuwa analikabidhi Kanisa tovuti hiyo ili kazi
ya uinjilishaji kupitia muziki mtakatifu ifuate mtiririko wa kiliturujia
unaokubalika na Kanisa Katoliki.
Nawapongeza sana kwa utayari huo wa kuanziasha mapinduzi katika MUZIKI MTAKATIFU,
ReplyDeletemaana wanakwaya wengi hujiimbia tuu waonavyo inafaa.
Vyema sana. Muhimu ni kuwa maendeleo haya yasifunge milango kwa kizazi cha wanamuziki wanaojifunza kiwapa nafasi ya kukua.
ReplyDeleteMungu atubariki