“Himizeni watoto wasome seminari” mapadri waaswa
Askofu wa jimbo Katoliki
Kahama, Mhashamu Ludovick Minde amewataka mapadri kuhakikisha wanawasaidia
watoto kutoka kila parokia wajiunge katika seminari ya Ushirombo iliyopo
jimboni hapa kwa lengo la kukuza miito ndani ya Kanisa.
Askofu Minde ametoa wito huo alipokuwa akibariki na kufungua rasmi shule
na nyumba ya watawa katika parokia ya Mtakatifu Fransisko wa Sale, Isaka
jimboni hapa na kutoa wito kwa mapadri kuwasaidia watoto wenye nia wasome
seminari.
Amesema katika kila parokia wamekuwepo watoto wenye nia ya kujiunga kusoma
seminari lakini wamekuwa wakikosa msaada hivyo amewataka mapadri kwa
kushirikiana na wazazi na walezi kuwasaidia kuhakikisha wanakwenda kusoma
seminarini hapo.
Askofu Minde amesema parokia zote
23 zilizopo jimboni Kahama zihakikishe zinakuwa na watoto wanaojiunga kusoma
katika Seminari hiyo iliyopo katika Parokia ya Mama Bikira Msaada wa Daima,
Ushirombo kwa kuwasaidia mapadri.
“Elimu ni moja ya zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, hivyo lazima wazazi na
walezi kwa kushirikiana na Kanisa kuhakikisha watoto wanapewa elimu na malezi bora na kuwasaidia wakue katika
maadili mema,” amefafanua
Askofu Minde amesema elimu ni
sehemu ya uchungaji, ni lazima mapadri wawasaidie watoto katika kila parokia
wenye nia ya kwenda kujiunga katika shule hiyo ya seminari kusoma hapo kwa
lengo la kukuza miito mbalimbali ndani ya Kanisa.
Parokia ya Fransisko wa Sale, Isaka imepata watawa wa shirika la Masista wainjilishaji wa Bikira Maria
watakaofanya kazi ya utume hapo baada ya kukamilika kwa nyumba yao na pia watakuwa
walezi na kuwafundisha watoto katika shule ya mwenye heri Askofu Fulton Sheen
English Medium Primary School.
Katika mahubiri yake aliyoyatoa wakati wa misa baada ya kubariki na
kufungua rasmi shule na nyumba ya
watawa, Askofu Minde amewataka watawa watakaofanya kazi ya utume wao hapo
kufanya kazi kwa furaha na
matumaini huku wakimkazia macho Yesu
Kristo kwa upendo na jamii yote.
Comments
Post a Comment