Malezi mabaya kwenye familia yanaua miito ya Upadri

Na Sarah Pelaji

BAADA ya Vatikani kutoa ufafanuzi juu ya mwongozo mpya wa malezi ya kipadri, baadhi ya viongozi wa Kanisa na waamini wamesisitiza malezi ya watoto katika familia kuwa ndiyo utajiri wa Kanisa.
Akizungumza na Gazeti Kiongozi, Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila amesema kuwa, ni vyema Kanisa likaangalia baadhi ya changamoto ambazo Kanisa linapata katika nyakati hizi ili kupata viongozi wema, bora, wenye imani thabiti ya kuliendeleza Kanisa.
“Ni kweli lazima kuangalia malezi ya vijana katika seminari zetu ili kuwafinyanga wawe mapadri waaminifu kwa kondoo wa Mungu kwani kazi ya Padri kutakatifuza watu, mwenye sura ya Kristo, baba Mchungaji mwema.
Jambo muhimu la kuzingatia ni malezi katika familia kwa sababu padri anatoka kwenye familia hivyo chimbuko la kwanza Kanisa ni familia.
Tupeleke nguvu zetu kwenye familia ili watoto wapate malezi bora, miito yao ichochewe kwa kuwaandaa kuwa mapadri, watawa na walei walio na maadili, imani na ukomavu wa kiimani. Tusipozingatia malezi ya watoto tunalea kizazi ambacho hakitaweza kuwajibika kwa lolote kama wazazi, mapadri, watawa na viongozi wa jamii hapo baadaye,” amesema Askofu Msonganzila.
Aidha amezitaja baadhi ya changamoto katika malezi ya vijana kuwa mapadri ukiwemo mwingiliano wa tabia mbalimbali ambazo vijana hao wamekuwa nazo.
“Kwa bahati mbaya kama mzazi alizembea tabia fulani kama wizi, mahusiano ya jinsia moja, kiburi nk. inawezekana Kanisa likapata wakati mgumu wa kumbadilisha kijana huyu. Wizi ukianzia nyumbani utaingia Kanisani, ushoga ukianzia nyumbani na kulelewa utaingia Kanisani, kadhalika uvivu nk.
Mila pia ziangaliwe kwani kijana akienda na mila za ukoo ama kabila lake kwenye seminari, inakuwa vigumu kumbadilisha, hivyo kuleta changamoto zaidi katika malezi yake ya upadri ama utawa.
Kinachotakiwa ni wazazi kuwa karibu na watoto wao, kufuatilia mienendo yao ili watambue pale palipo na changamoto ili kuwasaidia,” amesisitiza Askofu Msonganzila.
Ametaja muda wa kusomea upadri kuwa pia ni changamoto kwani kijana baada ya kusoma elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, badala ya kwenda chuo kikuu inamlazimu ajiunge na malezi ya upadri kwa takribani miaka 9.
“Atasoma falsafa  miaka mitatu, Teolojia miaka minne, aende mwaka wa kichungaji baadaye shemasi kisha padri. Wakati akimaliza Teolojia anaona wenzake aliosoma nao wameoa, wanaendesha magari, wana kazi nzuri na mishahara mikubwa wakati yeye anasubiri pesa za kupewa tena na Kanisa. Hapo anaona amepoteza muda. Ndiyo maana idadi kubwa ya waseminari katika seminari zetu ndogo wakimaliza kidato cha sita, wanajiunga na vyuo vikuu na kupotelea huko hawarudi tena.”
Changamoto nyingine ni gharama za kusomesha waseminari. Ameeleza kuwa, kijana akishamaliza elimu ya kidato cha sita, akiitikia wito wa kuwa Padri itamlazimu asome katika seminari kuu falsafa na Teolojia. Gharama hizo ni za Kanisa.
Zamani palikuwa na wafadhili wa kuzisaidia seminari hizo lakini kwa sasa wafadhili hawapo inabidi kila Jimbo kuwasomesha waseminari wake.
“Tulianza kuchangia kwa kila mseminari laki nne, baadaye ikapanda laki nane, sasa milioni 1.2. Kama Jimbo lina waseminari wengi gharama zake pia ni kubwa.
Ukiwaambia waamini wasaidie kuwasomesha waseminari hawa wanaona ni mzigo kwao. Ukimwambia mzazi achangie anaona ameshatimiza wajibu wake wa kulea na kusomesha hadi kidato cha sita sasa kazi kwa Askofu,” ameeleza.
Baadhi ya changamoto nyingine ni uhuru wa mitandao ya kijamii ambayo imetoa uhuru wa kupata taarifa zozote mwanadamu anazozitaka yakiwemo mambo yaliyo kinyume na maadili. Vijana wanakuwa huru kutumia mitandao hiyo tangu udogo wao, wakiwa wakubwa wapo seminarini wameshazoea tayari baadhi ya tabia ambazo kimsingi hazipaswi kukuzwa kwa kijana anayetarajia kuwa padri kwani Kanisa linahitaji padri mwenye maadili.
Ikumbukwe kuwa Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki Tanga alishawahi kuzungumzia masuala haya ya malezi akisema kuwa, zipo baadhi ya changamoto kwa sasa ambazo hazifai kufumbia macho kama kuwafuatilia vijana kuona kama wana maadili.
“Ukampa kijana ambaye ana dalili za mahusiano ya jinsia moja, (ambapo kwa sasa hatutegemei kwamba wapo ) unatengeneza padri atakayewaumiza waamini, kuwakwaza na kulisaliti Kanisa.
Ukimpa upadri kijana mwenye majivuno anayejiona bora kuliko wenzake, huyo hatakuwa na nafasi ya kuwachunga kondoo wa Bwana kwa ukarimu,” alibainisha Askofu Banzi.

Gombera wa seminari anasemaje kuhusu changamoto hizo?
Gazeti la Kiongozi limefika kwenye seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Segerea iliyopo katika Jimbo Kuu Dar es Salaam ambapo vijana wanaotaka kuwa mapadri wanalelewa.                                                                 
Gombera katika Seminari hiyo Padri Tobias Ndabhatinya amesema kuwa, kwa sasa Kanisa lina changamoto mbalimbali ikiwemo, kutoeleweka kwa mafundisho. Mafundisho hayajaelezwa vizuri kwa watu. Waamini wamekuwa wanafuata maisha ya Kikristo na Ukatoliki lakini kimsingi “kila mmoja” anaamini vyake.

Mifano mibaya ya maisha ya mapadri kuwa kikwazo kwa waamini, dini mbalimbali na ushawishi mkubwa kiasi cha kuwatikisa waamini kiimani (injili ya mafanikio), ushirikina (kuchanganya imani), idadi ndogo ya wachungaji (Mapadri) ukilinganisha na uhitaji, kuporomoka kwa maadili katika familia ambayo ni Kanisa dogo, mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watu hata wale wanaojiita Wakristo! Harambee nyingi makanisani kuliko ufundishwaji wa Imani.
Ubinafsi unaosababishwa na utandawazi. Watu wanawasiliana kwa urahisi na watu walio mbali kwa mtandao kuliko na walio karibu nao.

Kwa sasa Kanisa linahitaji mapadri wa aina gani?
Ilizoeleka enzi za wamisionari mapadri walikuwa ni wazungu, kama ni waafrika walikuwa wanapata misaada kutoka katika nchi zilizoendelea. Hivyo wakati wa kuinjilisha walikuwa wanawapatia waamini zawadi kama nguo, fedha, chakula, parokia zilikuwa zinapewa magari, zinasaidiwa kujenga makanisa nakadhalika.
Kwa sasa wamisionari ni waafrika wazalendo ambao wanahitaji kujituma ili kuliendeleza Kanisa kwa michango yao ya ndani.
Ndiyo maana Gombera Padri Tobias Ndabhatinya anasema, Kanisa lipo katika ulimwengu wa utandawazi hivyo linahitaji mapadri wabunifu ili kutatua changamoto hizo.
“Kanisa kwa sasa linahitaji mapadri wenye mtazamo chanya kuhusu maisha, wenye kuishi maisha ya ushuhuda yaani kuishi maisha yenye taswira ya Kristo katika kondoo wao wanaowachunga.
Wenye kuishi maisha ya sala, kwani sala ndiyo nguvu ya padri. Asali kwa ajili yake mwenyewe na kondoo wake. Padri awe na mbinu mpya za uinjilishaji kwani nyakati zinatofautiana hususani uinjilishaji kwa vijana pamoja na muingiliano wa madhehebu mbalimbali.
Kanisa pia linahitaji padri mwenye kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia kwa kujiwezesha kitaaluma. Wenye bidii ya kutafuta utakatifu.
Pia Kanisa linahitaji vijana wanaotaka kuwa mapadri wawe tayari kupokea malezi katika misingi yote: kiroho, kiutu, kiakili na kichungaji.

Je, Kanisa linahitaji mapinduzi gani katika kulea (formation) ya waseminari?
Gombera Tobias Ndabhatinya ameeleza baadhi ya mapinduzi katika kuwalea waseminari.
Mafunzo maalum ya malezi yatolewe kwa wale wanaoteuliwa kuwa walezi...katika ngazi zote za malezi kuwasaidia waseminari kuwa na picha halisi ya upadri na hivyo kupambanua kama kweli wameitwa.
Kutilia mkazo katika mwaka wa malezi unaomsaidia kijana kutambua kama kweli kaitwa na kumpa malezi ya msingi mintarafu upadri. Pawe na uwazi na ukweli (kuaminiana).
Kuwa na ubunifu mpya wa mara kwa mara ili kuendana na nyakati mbalimbali za vijana.
Walezi na walelewa kushiriki pamoja katika shughuli za kila siku kama kazi za mikono na michezo. Pia kuchochea roho ya mazungumzano miongoni mwa walezi na walelewa.
Kuongeza idadi ya walezi ili wawe karibu zaidi na walelewa hasa katika zoezi la maongozi ya kiroho.
Vijana wajifunze na kupenda maongozi ya kiroho katika hatua zote za malezi.
Kuwe na ubadilishanaji wa taarifa juu ya Mseminari kati ya seminari na Jimbo au shirika anakotoka.
Waseminari wawe tayari kupokea taarifa hasi juu yao na kuwa tayari kubadilika. Taarifa hasi isionekane kama hatari kwa kufukuzwa bali kama mwaliko wa mabadiliko.

Je, walei wana mtizamo gani juu ya hilo?
Kwa kuzingatia umuhimu wa walei katika Kanisa ambao wana nafasi kubwa ya kulijenga na kuliendeleza Kanisa, Gazeti hili limefanya mazungumzo na baadhi ya walei ambao wamesisitiza malezi kuanzia ngazi ya familia.
Baadhi yao wamesema kuwa, ni vyema wazazi wakawalea watoto wao katika misingi ya imani na wakawa kichocheo cha miito tangu utotoni.
Dkt. Fredrick Kigadye amefafanua kuwa, wazazi wanao wajibu wa kuchochea miito lakini wasiwalazimishe kujiunga na miito ambayo itawatesa vijana wao kwani hawana wito huo.
“Wapo wazazi wanawashawishi watoto kwenda seminari ili wawe mapadri wapate sifa kama familia lakini wanafahamu wazi kuwa kijana wao ana wito wa ulei.
Wengine wanawashawishi wakawe watawa ili wapate sifa. Kuitwa mzazi wa padri au sista kusiwe ni sifa ya kujipatia kipato, kupata heshima na mtoto kuishi maisha mazuri yenye uhakika!La hasha! Iwe ni sadaka ya kweli kwa Mungu na imani thabiti kwa Mungu na si sifa.
Tusipoangalia changamoto hii tunaweza kupata matatizo mbalimbali ya kiimani na kubaki kulaumiana ama kupoteza waamini. Kijana asaidiwe kuishi wito alioitiwa na Mungu na si mwanadamu kwa ajili ya maslahi binafsi,” amesema Dkt. Kigadye.
Wapo pia baadhi ya vijana ambao wamesema kuwa, nyakati hizi lazima Kanisa liangalie changamoto za kiimani bila kuogopa. Litumie busara kuangalia malezi kwa waseminari watakaokuwa mapadri hapo baadaye kwani inawezekana baadhi wana changamoto za kimaadili, imani na mengine lakini wanaonewa huruma na kupata Daraja hilo Takatifu lakini wanaongeza changamoto zaidi ndani ya Kanisa.
“Nimependa kauli ya Askofu Banzi aliyosema kuwa, kama kuna kijana ana dalili ama ameshaanza tabia za mahusiano ya jinsia moja, aondolewe maana yuko kinyume na maadili ya Kanisa. Changamoto zilizo kwa vijana za ushoga, usagaji, wizi, ubinafsi nk. zinaweza pia kuwa katika vijana wanaojiunga na seminari zetu ili wawe mapadri ama wasichana wanaojiunga na utawa. Kanisa liangalie haya kwa makini,” amesema Yohanes Mkrimwene wa Parokia ya Kristo Mfalme Tabata.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU