CARITAS Mbeya watakiwa kuwa mfano katika kuitumikia jamii
WAFANYAKAZI wa Idara ya Caritas na Maendeleo, Jimbo
Katoliki Mbeya wametakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kutenda na kuyaishi
maisha mema katika jamii kama wanavyoonekana katika maeneo yao ya utendaji
kazi.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa
Idara ya Caritas na Maendeleo, Jimbo Katoliki Mbeya, Edgar Mangasila wakati wa
hafla fupi ya kukabidhi zawadi na kuwapongeza wafanyakazi 9 wa vitengo
mbalimbali vya Caritas na maendeleo iliyofanyika katika kituo cha malezi ya
vijana cha Knorr Bremse cha St.Alamano, Parokia ya Shewa jimboni Mbeya.
Mkurugenzi Mangasila amesema kuwa maendeleo na mafanikio katika maeneo yao ya utume yanaanzia katika ngazi ya familia, jumuiya ndogo ndogo
na hatimaye katika jamii kwa ujumla, hivyo amewaalika kuyaishi kwa vitendo yale
yanayoonekana katika maeneo yao ya utume
mathalani, unyenyekevu, upendo, ushirikiano, haki na amani huku
wakimtanguliza Mungu.
“Ninawapongeza kwa kuzaliwa upya leo kwa
kusheherekea siku zenu za kuzaliwa, kumbukeni kufikia hapa leo siyo kwa mipango
yenu bali kwa mipango ya Mwenyezi Mungu, kupitia siku hii ya leo nawaalika
kutafakari kutenda yanayompendeza jirani yako,”amesema.
Ameongeza kuwa mafanikio katika utume wao
kazini yanatokana na kutekeleza majukumu
yanayowakabili kwa unyenyekevu,
ukweli na kujituma pasipo kujibakiza kwa ajili ya jamii ya wahitaji kadri ya
upendo na huruma.
Kwa upande wake mmoja wa wafanyakazi,
Praxeda Killian akizungumza kwa niaba ya
watumishi walioadhimisha siku ya kuzaliwa amemshukuru Mungu kwa kufikia
siku hiyo huku shukrani za pekee
zikienda kwa wazazi waliowalea na
uongozi wa Caritas kwa kuendelea katika makuzi mema ya kifamilia.
“Kwa niaba ya wenzangu tuliozaliwa leo tusisahau kuomba na kusali
muda wote ili Mungu aweze kutujalia kuwahudumia wahitaji kwa upendo, haki,
usawa na kujituma bila kujibakisha na tusisahau kuwakumbuka na kuwatembelea
wahitaji,”amesisitiza.
Comments
Post a Comment