Wataliki na watalakiwa hawajaruhusiwa kupokea Ekaristi
KUMEKUWEPO na uvumi katika mitandao ya kijamii kuwa
Baba Fransisko kupitia waraka wake wa Furaha ya Upendo (Amoris Laetitia)
ameruhusu wataliki na watalikiwa ambao wameshafunga ndoa nyingi (mfano ya
kiserikali), kupokea Ekaristi.
Uvumi huo sii kweli. Baba Mtakatifu amesisitiza kuwa watu hao wanapaswa
kusaidiwa na Kanisa ili waweze kufahamu mpango wa Mungu juu yao.
Hayo yamefafanuliwa na Tume ya Tume
ya Sheria za Kanisa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania T.E.C.
Mwenyekiti wake akiwa Askofu Rogathy Kimaryo, Makamu Mwenyekiti Askofu Michael
Msonganzila na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Padri Henry Mchamungu mwalimu
katika Seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga Segerea jijini Dar es Salaam.
Tume hiyo imefafanua kwa waamini wote pamoja na makleri kuelewa kuwa, Baba
Mtakatifu katika nyaraka hiyo alisema; “Katika kuangalia namna ya kukabili
uchungaji kwa watu waliofunga ndoa za kiserikali, kwa wale waliopeana talaka na
kuingia katika mkataba mpya wa ndoa au kwa wale wanaoishi pamoja bila ndoa,
Kanisa lina wajibu wa kuwasaidia kuelewa mbinu za kimungu za kuwajulisha neema
katika maisha yao na kuwapa msaada ili waweze kufikia utimilifu wa mpango wa
Mungu juu yao.” (Rejea Amoris Laetitia, n. 297).
Baba Mtakatifu amesisitiza kuwa wakristo waliopeana talaka halafu
wakafunga ndoa ya kiserikali wana haja ya kujumuika kikamilifu zaidi katika
jumuiya za kikristo kwa namna mbalimbali zinazowezekana, mradi isilete makwazo
kwa wengine.
Kushiriki kwao kunaweza kudhihirishwa katika ibada mbalimbali za Kanisa.
“Watu hawa wanahitaji kujisikia siyo kama wanakanisa waliotengwa, bali kama
wanakanisa walio hai, wanaoweza kuishi na kukua ndani ya Kanisa na kuliona kama
Mama anayewakaribisha daima, anayewatunza kwa upendo na kuwatia moyo katika
mapito ya maisha na ya Injili.” (Rejea Amoris Laetitia, n. 299).
Baba Mtakatifu amewasihi mapadri kuwasindikiza na kuwasadia wanandoa
waliopeana talaka na kuingia katika mkataba mpya wa ndoa, ili waweze kuelewa
hali yao kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa na mwongozo wa Askofu. Wanandoa
hawa wasaidiwe kujichunguza na kujichunguza huku kuwaongoze kufikia ufahamu wa
hali yao mbele ya Mungu. Ieleweke kuwa uchunguzi huu hauwezi kamwe kuthubutu
kwenda nje ya matakwa ya Injili ya ukweli na ukarimu kama inavyopendekezwa na
Kanisa (rejea Amoris Laetitia, n. 300).
Kuendana na mafundisho ya Kanisa, mwanandoa ambaye amejikuta katika talaka
na akabaki mwenyewe (single), yaaani bila ya kuingia kwenye muungano mwingine,
na anaishi vizuri maisha yake ya kikristo, huyo hazuiliwi kupokea sakramenti.
Lakini yule ambaye baada ya talaka amejiingiza kwenye muungano au mkataba mpya
wa ndoa, ni vigumu kupokea Ekaristi. Kwa maneno mengine, inakuwa vigumu kwa mtu
huyo kupokea Ekaristi kwa sababu hali yake ya maisha inapingana na umoja wa
upendo kati ya Kristo na Kanisa unaojidhihirisha katika Ekaristi (rejea John Paul II, Familiaris Consortio, n. 84).
Furaha ya upendo ya familia ni wosia wa kitume uliotolewa na Baba
Mtakatifu Fransisko kuhusu injili ya Familia na kuchapishwa rasmi tarehe
19/03/2016 katika sikukuu ya Mt. Joseph mume wa Bikira Maria sanjari na
kumbukumbu ya miaka mitatu ya Upapa wake kama khalifa wa Mt. Petro. Wosia huu
ni matunda ya maadhimisho ya sinodi za Maaskofu kuhusu familia za mwaka 2014 na
2015.
Katika wosia huo wa kitume Baba mtakatifu amefafanua kwa namna ya pekee
umuhimu wa sadaka katika maisha na utume wa familia.
Wosia wa furaha ya Upendo ndani ya Familia umegawanyika katika sura tisa
zinazoelezea mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa sinodi ya Familia. Hivyo,
Baba Mtakatifu analitaka kanisa lililo familia ya Mungu lichukue muda kusoma na
kutafakari wosia huu kwa uvumilivu na kufanya utekelezaji kadri ya mazingira
husika kwa kuzingatia mafundisho ya Mungu na kanisa lake.
Comments
Post a Comment