Ajali ya wanafunzi Arusha
Mapadri, Masheikh, wachungaji watahadharisha
θ Waongoza ibada katika eneo la ajali
Na Sophia Fundi, Karatu.
MAELFU
ya wananchi wa wilaya ya Karatu mkoani Arusha wamejitokeza katika ibada maalumu
iliyofanyika katika eneo ilipotokea ajali na kuua wanafunzi 33, walimu 2 na
dereva mmoja.
Ibada hiyo ilishirikisha waamini wa dini
mbalimbali wilayani Karatu ikijumuisha mapadri wa Kanisa Katoliki, masheikh na
wachungaji, wote wakiwa na lengo la kumwomba Mungu azipokee roho za marehemu na
kuondoa balaa la ajali kama iliyotokea katika eneo hilo na katika wilaya nzima.
Mkuu wa wilaya ya Karatu ambaye ni Mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Bi. Theresia Mahongo amewashukuru
viongozi wa dini na waamini kwa pamoja kwa kushirikiana katika ajali iliyotokea
kwa kuwasaidia majeruhi pamoja na marehemu kuwapeleka wanapostahili.
Amesema serikali inatoa shukrani zake kwa
wote walioshiriki kwa hali na mali katika tukio zima, wakati ilipotokea ajali
hadi kusafirisha majeruhi na maiti.
Akizungumza katika ibada hiyo mwakilishi
wa Askofu Jimbo Katoliki Mbulu ambaye ni Makamu Msimamizi wa Kitume wa Jimbo
Katoliki Mbulu Padri Urbano Sulle amewaomba waamini kuwa na ushirikiano bila
kuangalia itikadi za dini kwani watu wote ni wana wa Mungu.
Amelaani vitendo vya madereva kutofuata
alama za barabarani na kusababisha ajali ambapo Malaika wa Mungu ambao ni taifa
la kesho na waliokuwa na ndoto zao za baadaye wamekatishwa ndoto hizo.
Kwa upande wake mwakilishi wa Kanisa la
KKKT jimbo la Karatu Mchungaji John Safari amewaomba waamini kwa ujumla wao
kuwa na roho ya toba kila wakati wakiinua macho yao kwa Mungu na pia kukemea
roho ya ajali iliyotawala katika maeneo yote na kumwomba Mungu kutakasa eneo
ilipotokea ajali kwa damu ya Yesu
aliyekufa msalabani.
Ajali hiyo ilitokea Mei 6 mwaka
huu katika eneo la Marera kijiji cha Rhotia wilayani Karatu ambapo wanafunzi 33
wafariki, walimu 2 pamoja na dereva wa gari baada ya gari NO.T.871BYS COSTA
kupinduka na kutumbukia kwenye korongo.
Comments
Post a Comment