Asiyemheshimu Bikira Maria hapangiki namba

TUMEINGIA mwezi Mei tena, mwezi mmojawapo kati ya miezi mitatu ambapo Wakatoliki huwa tunajitahidi kumwalika Bikira Maria katika shughuli zetu za kujikuza katika utakatifu ili hatimaye tukajiunge na Mungu mbinguni kwa maisha ya umilele. Nawakumbusheni miezi mingine ni Agosti na Oktoba.
Twendeni polepole: Ndugu zanguni, kumwabudu Mungu siyo suala la “mitulinga”. Kwa nini nasema hivyo? Nitakumbusheni. Kuhusu kumwabudu Mungu, Yesu alituzuia kubwatabwata na kumwabudu kana kwamba tu wendawazimu. Mimi huwa nashangaa sana. Sijui kwa nini hatuyaheshimu maneno ya Mwalimu wetu na Maandiko Matakatifu.
Alisema, “Tena msalipo, msiwe kama wasiomjua Mungu; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia: wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Nanyi mkiwa katika kusali, msipayukepayuke, kama watu wa mataifa, maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi, msiwaige hao, maana Baba anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba” (Mt 6:5-11).
Zaidi ya hayo, tumeagizwa tumwabudu Mungu kwa akili yetu pia, yaani siyo kwa juhudi na “mtulinga tu”. Tunasoma jambo hili katika Mt 22:37-40. Ndipo kwa haki, Kanisa Katoliki huwaalika waamini wake wawe na utaratibu wa kusali kila mwezi na kila siku. Ndiko kusali kwa akili huko!
Kumbe, niwakumbusheni tena jinsi miezi ilivyoratibiwa kwa akili na Mama Kanisa. Miezi imepangwa itumiwe ifuatavyo: Januari- Jina la Yesu, Februari- maisha ya wakfu, Machi – Mt. Yosefu, Aprili – Mateso ya Yesu, Mei – Bikira Maria, Juni – Moyo mtakatifu wa Yesu, Julai –Damu azizi ya Yesu, Agosti – Moyo mtakatifu wa Bikira Maria, Septemba – Malaika watakatifu, Oktobea – Rozari takatifu, Novemba – Roho za marehemu, Decemba- Kuzaliwa kwa Yesu.
Aghalabu, nawakumbusheni jambo lingine. Siku zimepangwa kwa akili zitumiwe ifuatavyo: Jumapili – Waamini wote au Utatu Mtakatifu, Jumatatu – Roho Mtakatifu au Malaika watakatifu, Jumanne- Mitume watakatifu, Jumatano – Mt. Yosefu, Alhamisi – Ekaristi takatifu, Ijumaa – Moyo mtakatifu wa Yesu, Jumamosi – Bikira Maria.
Sasa nakuja kwenye mada ya leo. Inatoka kwenye maswali kuhusu Mama Bikira Maria. Kifupi, maishani mwangu nimewahi kubandikwa maswali mengi kuhusu Mama Bikira Maria. Maswali hayo hujirudiarudia kama yanavyojirudia majira ya kiangazi na masika.
Kumbe, leo nisikilizeni vizuri. Kwanza kabisa, nakusihini wote myaelewe vizuri mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu Bikira Maria. Isiwe kila siku tuhuma na kubwatabwata tu kana kwamba sisi sote tumelewa “kimpumu”.
Ni hivi, mafundisho makuu ya Kanisa Katoliki kuhusu Mama Bikira Maria ni matano tu: kukingiwa dhambi ya asili, ubikira wa daima, umama wa Mungu, kupalizwa mbinguni na ushenga wake.
Kumbe, maswali kadhaa huulizwa katika maeneo haya pasipo mpangilio mahususi. Hapo hapo, huja maswali kadhaa kuhusu ibada kwa Bikira Maria. Ndipo huulizwa kama ni halali au ni sawa kufanya ibada kwa heshima yake na vile vile kuwa na sala kama Salamu Maria, memorale, Malaika wa Bwana na kadhalika. Sawia huulizwa kama ni halali kusali rosari na kuiadhimisha kwa heshima yake miezi ya Mei na Oktoba na kadhalika.
Mwishowe, huwapo maswali madogo madogo kuhusiana na vyama vya kitume vilivyozaliwa kwa ajili ya kumheshimu, hususan, Legio Maria na Utume wa Fatima. Wapendwa wangu, katika mada hii nayashughulikia maswali mawili tu ili mwezi huu tuuadhimishe kwa uelewa mpevu.
Hivi nakuleteeni muhtasari wa majibu mawili maarufu, mosi kwa nini Bikira Maria anaheshimiwa na pili kwa nini tunamtumia katika kuomba badala ya kila siku kumwomba Mungu moja kwa moja.
Swali la kwanza: Heshima kwa Bikira Maria
Leo, kama siku zote, namjibu anayetuuliza kwa heshima (1Pet 3:15). Kwa nini Bikira Maria anaheshimiwa na Wakatoliki? Jibu ni kwa sababu ANA NAFASI YA PEKEE KATIKA UKOMBOZI WETU.
Sikilizeni. Popote wanapopigana vita vya ukombozi, washiriki wote hata wale waliowaletea askari maji na biskuti, au hata bisi na mihogo, au hata uyoga na matunda, hukumbukwa na kuheshimiwa, sembuse aliyemlea na kumkuza kiongozi wa mapambano! Bikira Maria ndiye mama wa kiongozi wa mapambano aliyoyaendesha Yesu Kristo dhidi ya shetani na silaha zake za mauti na dhambi.
Ni mama wa jemedari wetu. Mwenye sababu kwa nini asiheshimiwe atoe! Tusisahau. Yesu Kristo, Mwokozi wetu, alifanyika mwanadamu mwenye mwili na damu kwake yeye Bikira Maria. Mwili na damu alivyopata toka kwa Bikira Maria ndivyo vilivyomwezesha kutoa sadaka ya ukombozi wetu (Ebr 10:5-7). Bila nyama na damu Yesu asingeliweza kutoa sadaka ya kutokomboa sisi. Angelitoa nini? Roho haitoleki sadaka.
Lakini siyo haya tu. Kuna suala la kumhudumia na kumtunza kwa hali na mali. Kumbe, Bikira Maria ndiye aliyemkuza tumboni mwake kwa miezi tisa. Ndiye aliyemzaa. Ndiye aliyemnyonyesha na kumlisha akue na kuwa mtu kamili. Ndiye aliyekesha naye usiku na mchana. Ndiye aliyemkimbizia usalamani huko Misri. Ndiye aliyemfundisha kutambaa, kutembea na kusema. Ndiye aliyempeleka hekaluni kumkomboa na kazi za kikuhani.
Ndiye aliyemfundisha sala na ibada kwa Mungu. Ndiye aliyemhifadhi usalamani huko Nazareti. Ndiye aliyempikia chakula alipokuwa akifanya kazi yake ya useremala. Ndiye aliyemfundisha kufanya ibada katika kabila lake la Kiyahudi. Ndiye aliyemfundisha heshima kwa watu na kadhalika. Soma mwenyewe Lk 1-2.
Haya yote yanampa Mama Bikira Maria mahali pa juu pa heshima kati ya wote wanaokiri wamekombolewa na mtoto wa tumbo lake. Asiyeliona jambo hili atuambie kwa nini halioni. Kwa sababu hii asiyemheshimu Bikira Maria hatuna mahali pa kumweka. Hapangiki namba kabisa.
Sikilizeni. Mchezo unapochezwa wachezaji hupangwa namba kadiri wanavyofaa katika nafasi mbalimbali. Kumbe, katika shughuli za kiroho, mtu asiyemheshimu Bikira Maria hapangiki popote. Tulia, nitakueleza sasa hivi!
Mosi, hapangiki namba kati ya watakatifu. Mtu asiyemheshimu Bikira Maria hawezi kuwa mmoja watu watakatifu na hivyo lazima awe kinyume na watakatifu. Kwa nini? Kwa sababu malaika mtakatifu kama Malaika Gabrieli alisema Maria amejaa neema na Bwana yu pamoja naye. Sasa asiyeyakubali maneno ya malaika Gabrieli atakuwaje mtakatifu vile vile? La hasha, lazima awe mtu tofauti na malaika.
Tazama, tunasoma habari na maneno ya Mtakatifu malaika Gabrieli ifuatavyo: “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya kwa msichana mmoja bikira aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu wa ukoo wa Daudi. Malaika alimwendea, akamwambia, ‘Salamu ewe uliyeneemeshwa na Mungu, Bwana yu pamoja nawe’.
Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza, maneno hayo yanamaanisha nini? Malaika akamwambia, ‘Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujaza neema. Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiune; nawe utampa jina Yesu. Yeye atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, baba yake. Kwa hiyo atautawala ukoo wa Yakobo hata milele na ufalme wake hautakuwa na mwisho’.
Maria akamjibu, ‘Yatawezakanaje hayo, hali mimi ni bikira?’ Malaika akamjibu, ‘Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu Mwana wa Mungu.
Ujue pia kwamba hata Elizabeti, jamaa yako naye amepata mimba ingawa ni mzee na huu ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu’. Maria akasema, ‘Mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyosema’. Kisha yule malaika akaenda zake’ (Lk 1:28-38).


Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI