Wanadiplomasia wa Vatican ni madaraja kati ya Papa na Makanisa mahalia
Taasisi ya Kidiplomasia ya Kanisa Katoliki ni mahali ambapo wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia wanafundwa ili kuwa ni madaraja muhimu kati ya Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia. Hawa kimsingi ni wawakilishi wa Baba Mtakatifu kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Ijumaa, tarehe 26 Mei 2019, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea Taasisi ya Kidiplomasia ya Kanisa na kushiriki pamoja na familia hii katika sala, tafakari, chakula pamoja na kushirikishana furaha, matumaini na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu.
Jumuiya hii ambayo kwa mwaka huu inaundwa na Mapadre 33 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, imeonja kwa namna ya pekee, utu na ubinadamu; ukristo na upendo wa kibaba kutoka kwa Papa Francisko anayewachangamotisha daima kujiandaa kuwa kweli ni madaraja, mashuhuda na vyombo vya majadiliano kati ya watu wa Mataifa! Wanapaswa kutambua kwamba, wao ni madaraja muhimu sana kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia; Jamii za watu pamoja na Jumuiya ya Kimataifa. Ziara hii ya Baba Mtakatifu ilikuwa ya kawaida kabisa iliyoandaliwa na Askofu mkuu Giampiero Gloder, viongozi wakuu wa Jumuiya hii pamoja na watawa wanaotoa huduma ya kutukuka kwenye Jumuiya hii.
Baba Mtakatifu ameshiriki kuongoza masifu ya jioni na baadaye, akatumia fursa hii kusalimiana na kila mwanajumuiya aliyeshiriki katika Ibada hi ina baadaye, wakati wakisubiri chakula cha usiku, waliweza kujadiliana masuala mbali mbali yanayogusa maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu; huduma ya kidiplomasia inayotolewa na Kanisa sehemu mbali mbali za dunia; matatizo na changamoto zilizopo na kwamba, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa Kanisa kuwa kama “Hospitali kwenye uwanja wa mapambano”, ili kuganga na kuponya majeraha ya watu kutokana na sababu mbali mbali za maisha.
Baba Mtakatifu amewaambia wazi Mapadre hawa kwamba, watatakiwa kushirikisha uozefu na mang’amuzi yao yanayobubujika kutoka katika maisha na wito wao wa Kipadre; watatakiwa kuwa ni mashuhuda na vyombo utajiri mkubwa wa maisha ya Kanisa unaobubujika kutoka kwa watakatifu, wafiadini na waungama imani. Ameonya kwamba, dunia mambo leo iko kwenye Vita Kuu ya tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande, ili watengenezaji, wafanyabiashara na watumiani wa silaha waendelee kujinufaisha kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Huu ndio mfumo wa uchumi usiojali utu, heshima na haki msingi za binadamu na badala yake watu wanaendelea kujikita katika sera na mikakati ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.
Waathirika wakubwa wa mfumo wa uchumi kama huo ni wazee, wanawake na watoto! Matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, mambo yanayodhalilisha na kunyanyasa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kuna athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi. Katika matatizo na changamoto zote hizi, Mama Kanisa anapaswa kuwa mstari wa mbele ili kutibu na kuganga madonda haya kwa roho ya kimama inayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu. Kwa upande mwingine, Diplomasia ya Vatican inajikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.
Baba Mtakatifu anaonya kwamba, kamwe Kanisa haliwezi kustawi kwa kufanya wongofu shuruti. Kumbe, Kanisa litaendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; katika ukweli na uwazi; unyofu na upole; kwa kusikiliza kwa makini na kumwilisha imani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawaonya Mabalozi wa Vatican kwa siku za usoni kutambua kwamba, dhamana iliyoko mbele yao ni kubwa na ina changamoto zake, kwani daima watakuwa ni watu wenye masanduku mikononi, tayari kutumwa sehemu mbali mbali za dunia.
Wawe makini kwani wasipoangalia wanaweza kujikuta wakimezwa na malimwengu na hivyo kuanza kufilisika kiroho! Hatari kubwa kwa maisha na utume wao kama madaraja kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia! Katika maisha na utume wao, daima wawe ni watu wa sala, wenye kufanya tafakari za kina, ili kuwa na mang’amuzi mapana zaidi katika maisha na utume wao; wawe ni watu wapole, wanyenyekevu, watu wenye kiasi, lakini zaidi kama wachungaji wema wanaoitwa na kutumwa na Mama Kanisa: kuongoza, kutakatifuza, kufundisha; lakini zaidi wanahamasishwa kusikiliza kwa makini na kuandamana na familia ya Mungu katika hija ya maisha yaoìke hapa duniani!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa daima litaendelea kuhakikisha kwamba, Jumuiya hii pamoja na wanadiplomasia wake wanaangaliwa kwa jicho la upendeleo. Wawe ni mashuhuda amini wa maisha na wito wa Kipadre. Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Jumuiya ya Taasisi ya Kidiplomasia ya Kanisa Katoliki yamedumu kwa takribani saa moja na nusu. Amefafanua mambo msingi katika mwanga wa Mapokeo ya Kanisa na Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment