Umuhimu wa kuwa na ibada kwa Mama Bikira Maria (2)
SALA:
Sala ya Malaika wa Bwana ni sala ya jadi ya kimapokeo inayotumika kwa
kumbukumbu ya Mama Bikira Maria Kupashwa Habari ya kuzaliwa Bwana.
Sala hii inasaliwa mara tatu kwa siku:
alfajiri, mchana na magharibi. Wakati wa kipindi cha Pasaka, sala ya Malkia wa
Mbingu husaliwa badala ya ile ya Malaika wa Bwana, Sala ambayo imekuwa ikisaliwa tangu karne ya 10 au ya 11.
Sala zingine za Mama Bikira Maria ni sala ya Rozari Takatifu na sala ya Litania
ya Loretto. Litania ya Loretto hujulikana na kupendwa zaidi.
Maandamano: Wakristo mara nyingi wamekuwa
wakiandamana kwa kuonyesha heshima zao kwa Mama Bikira Maria. Maandamano kama
haya yamekuwa yakifanywa na wakatoliki na waothodoksi kuanzia karne ya 16.
Kwa mfano katika mji wa Los Angeles kule
Marekani kulikuwa na utaratibu wa kuandamana kwa heshima ya Mama Bikira Maria
kila mwaka kwa miaka 100 ya kwanza baada ya kuanzishwa kwa mji huo hapo mwaka
1781. Utaratibu huu uliokuwa unafanywa kwa kumbukumbu ya uanzishwaji wa mji huo
ulirudishwa tena mwaka 2011 baada ya kuachwa kwa miaka mingi.
Ibada zingine: Ibada kwa Mama Bikira Maria
kwa mujibu wa kanuni au mafundisho ya Kanisa Katoliki: Ibada hizi ni pamoja na
zile zinazohusu mafundisho juu ya Mama Bikira Maria kuwa yeye ni Mama wa Mungu,
au ile imani kwamba Mama Maria amekuwa daima Bikira na alikingiwa dhambi ya
asili na kwamba alipazwa mbinguni.
Ibada zenye uhusiano kama huu zinaweza
kuanza kufanywa hata kabla ya tamshi
rasmi la Kanisa la kiimani kuhusu fundisho husika kutolewa kwa kuwa
ibada zingine zinaendelea polepole na hivyo kuchukua muda mrefu. Mfano mzuri wa
ibada iliyokuwa inaendelea polepole ni ile ya muungano wa ibada ya Moyo
Mtakatifu wa Yesu na ile ya Moyo Safi wa Bikira Maria kuwa ibada ya Mioyo Mitakatifu
ya Yesu na Maria.
Hata hivyo, ibada zingine zinaweza
kulaaniwa kama ilivyotokea mwaka 1677, Roma ilipolaani ile imani kuwa Mama
Maria mwenyewe alishika mimba kibikira, imani iliyokuwa imezagaa kuanzia karne ya 4.
Maisha ya Mama Bikira Maria: Matukio fulani
fulani maalum katika maisha ya Mama Bikira Maria yamesababisha kuibuka kwa
ibada zinazolenga hivi vipengele maalum vya maisha yake. Mfano hai ni pamoja na ile Ibada ya Mateso Saba ya Mama
Bikira Maria inayokumbusha yale mateso aliyoyapata Mama Bikira Maria kama
alivyokuwa ametabiri Nabii Simeoni kuhusu kusulubishwa kwa Yesu Kristo
msalabani.
Kwa upande mwingine tena, kuna yale Matendo
ya Furaha ya Mama Bikira Maria yanayoanza na kupashwa kwake habari kuwa atakuwa
Mama wa Mungu na kuishia na tendo la kuvikwa kwake taji huko mbinguni. Kuna
ibada zingine zinazoendelea muda wote kama zile zinazohusishwa na ulipaji fidia
kwa matendo ya wanadamu ya kumtukana na kumkufuru Mungu yanayoendelea muda wote
bila kikomo.
Ibada zinazohusisha Matokeo ya Mama Bikira
Maria: Matokeo haya ni pamoja na yale yanayojulikana sana ulimwenguni ambayo
yamekubaliwa rasmi na Kanisa Katoliki. Mifano ya hayo matokeo ni kama yale ya
Bibi Yetu wa Guadalupe, Bibi Yetu wa Lurdi, Bibi Yetu wa Fatima, Bibi Yetu wa
Akita, Bibi Yetu wa Kibeho na lukuki ya ibada zingine za kikanda pote
ulimwenguni. Ibada hizi za kikanda ni kama zile za Bibi Yetu wa Afya Njema za kule India au zile
za Bibi Yetu wa Lichen za kule Poland.
Ibada kama hizi zimesaidia sana katika
ujenzi wa makanisa makubwa makubwa yaliyojengwa na kutolewa wakfu kwa Mama Yetu
Bikira Maria.
Picha na Sanamu za miujiza: Picha, sanamu
pamoja na ikoni za aina mbalimbali za Mama Bikira Maria zimekuwa zikihusishwa
na miujiza mbalimbali kama ile ya uponyaji iliyosababisha ibada hizi za
kitakatifu kufanyika katika nchi kadhaa na kuhimiza ujenzi wa vituo maalumu vya
hija kwa heshima ya Mama Bikira Maria.
Vitu vya kiibada: Vitu vya uchaji Mungu
vinavyohusiana na heshima kwa Mama Bikira Maria ni pamoja na skapulari za aina
mbalimbali, kama ile skapulari ya Bibi Yetu wa Mlima Karmeli ambayo inajulikana
zaidi. Kati ya medali zote za Mama Bikira Maria, medali inayojulikana na
iliyoenea zaidi ni ile ya Miujiza. Imani
inayohusu vitu vya kiibada kama medali
imekuwepo tangu miaka ya 1830.
Kuonekana mara nyingine kuwa na msisitizo
wa wazo moja katika matokeo mawili ya mahali mbalimbali na nyakati mbalimbali.
Kwa mfano katika matokeo ya Lurdi, ibada iliyosisitizwa ilikuwa ni ile ya
Kusali Rozari Takatifu na matokeo ya Fatima yaliripotiwa kuwa Mama Bikira Maria
alikuwa ameshika Rozari na pia skapilari.
Ibada za kikanda bado zinaendelea kuungwa
mkono na viongozi wa kanda hizo. Kwa mfano sikukuu ya “Bibi yetu wa Upweke wa
Porta Vaga katika visiwa vya Ufilipino imekuwa ikisherehekewa kwa karne na karne
na ikoni yake bado inaendelea kuheshimiwa.
Huko Uhispania, kila mwaka wakati wa
Pentekoste, kwenye watu milioni moja wana sherehe zinazoitwa “Romeria De El
Rocio’’ ambazo zinakuwa sehemu ya
sherehe mahalia za heshima kwa Mama Bikira Maria.
Kunakuwa pia na ibada zingine za aina
mbalimbali kwa heshima ya Mama Bikira Maria kwa mfano uwepo wa altare maalum
katika makanisa ya Kikatoliki, altare ambazo zimewekwa wakfu kwa heshima ya
Mama Bikira Maria.
Heshima kwa Mama Bikira Maria hazitolewi na
wakristo wakatoliki tu na wala si na wakristo tu bali na hata waumini wa dini
ya Kiislamu. Ibada ya Sala ya Rozari Takatifu, kwa mfano, hufanywa na wakristo
Waanglikana na pia na Walutheri ingawa namna yao ya kusali ni tofauti na
inavyosaliwa na waamini Wakatoliki.
Mwandishi ni Mhadhiri Mstaafu,Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dar
es Salaam.
Comments
Post a Comment