“Nguvu nyingi bila kumshirikisha Mungu ni kazi bure”
MOROGORO,Viongozi wa
dini na serikali wametakiwa kutokutumia akili na nguvu zao pekee katika
kusimamia majukumu mbalimbali na badala yake wamtegemee Mungu awaongoze katika
majukumu hayo ya kila siku.
Hayo
ameyasema Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor Mkude alipokuwa akihubiri katika Misa
Takatifu iliyofanyika Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro huku akitoa daraja la
kipaimara na kuwapa daraja la Usomaji na Usindikizaji maflateri.
Askofu Mkude
amesema viongozi mbalimbali wanatakiwa wafanye kazi zao za kuwaongoza wengine
kwa kuomba mwongozo wa Mungu kwakuwa asiposhirikishwa Mungu, kutakuwa na
malalamiko mengi kutoka kwa wanaowaongoza.
“Viongozi wa
dini na serikali tunatakiwa tumshirikishe sana Mungu katika kuibeba dhamana
ambayo tumepewa ya kuwaongoza wengine, tusipomshirikisha Mungu katika kazi zetu
kuna uwezekano mkubwa wa kutokutenda haki kwa tunaowaongoza hivyo kusababisha
malalamiko na hatimaye kukwama na kutokufikia malengo tuliyojiwekea ili Taifa
lisonge mbele,” amesema Askofu Mkude.
Askofu Mkude
amesema baadhi ya viongozi wamekuwa hawawatendei haki wengine hivyo kusababisha
malalamiko huku baadhi ya viongozi wakiamini kuwa hata wasipowatendea haki
wanaowaongoza hawataelewa chochote na kusahau kuwa dunia sasa hivi ni kama
kijiji na kila mtu anapambana ili azijue haki zake.
“Yatupasa
kuwa na hofu ya Mungu katika kuongoza vitengo tulivyokabidhiwa kwa kutenda
haki, tusipotenda haki ipo siku tusiowatendea haki watachoka na kuchukua
maamuzi magumu,” amesema Askofu Mkude.
Wakati huo
huo Askofu Mkude amewaasa viongozi wa dini kuwaombea wafanyakazi mbalimbali ili
wafanye kazi zao kwa moyo pasipo manung’uniko ili taifa lisonge mbele na
kufikia malengo.
“Kuna kazi
ambazo sisi hatuwezi kuingia mtaani na kuzifanya, hivyo tunapoazimisha siku hii
ya wafanyakazi duniani kote ni jukumu letu kuwaombea wafanyakazi wa vitengo
mbalimbali kama barabara, hospitali, maseremala na sekta zingine kwani
tunategemeana katika kila jambo, tuombeane ili tusonge mbele,” amesema Askofu
Mkude.
Comments
Post a Comment