Waamini Musoma waonywa juu biashara ya dawa za kulevya
Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael
Msonganzila amewataka waamini jimboni humo kutotaka maisha mazuri ya haraka
haraka kwa kutumia njia za mkato kama kilimo cha bhangi na kuuza dawa za
kulevya ili kupata mali na utajiri, bali
watumie njia halali inayompendeza Mungu.
Askofu Msonganzila ameyasema hayo hivi
karibuni wakati wa Misa Takatifu ambayo iliambatana na harambee ya kuchangia
ujenzi wa Kanisa ambapo jumla ya fedha taslimu shilingi milioni 106
zilipatikana pamoja na kutoa sakramenti ya kipaimara kwa watoto 400, Misa
iliyofanyika katika parokia ya Tarime Jimboni hapo.
Askofu Msonganzila amewaambia waamini hao
kuwa mali na utajiri ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama watatumia njia iliyo halali kwani wana
bahati ya kuwa na mifugo mingi ambayo wanaweza
kuitumia kupata mali na utajiri badala ya kuhangaika na kilimo cha
bhangi na kuuza dawa za kulevya ambazo hata serikali inapiga marufuku.
“Naomba niwaambie ndugu zangu msitake
maisha mazuri kwa kutumia njia ya kilimo cha bhangi, kuuza dawa za kulevya,
wizi au njia nyingine yoyote ya kupata mali haraka isiyo halali, zote hizi ni
njia za shetani wala hazimpendezi Mungu. Parokia ya Tarime mmejaaliwa kuwa na
mifugo mingi na kila familia naamini mna mifugo ambayo mna uwezo wa kuitumia
mifugo hiyo kwa ajili ya kupata mali, achaneni na njia hizo kabisa msije
mkajiletea matatizo maana hata serikali inapiga marufuku kabisa njia
hizo,”amesema Askofu Msonganzila.
Pia amewakumbusha waamini wa parokia hiyo
kuhakikisha kila mmoja anawajibika ndani
ya familia yake kudumisha amani na upendo, sambamba na kuhakikisha vitendo vya
ukatili vinakomeshwa ili amani, upendo na uvumilivu vitawale katika familia na
jamii kwa ujumla, ili kusudio la Mungu liweze kutimia kwa kuwa vitendo vingi
vya ukatili ambavyo vimekuwa vikitokea vinatokana na upendo, amani na uvumilivu
kupungua ndani ya familia.
“Wito wangu kwenu wakristo wa Parokia ya
Tarime, nawaombeni sana mshikamane, mpendane, mvumiliane pale mwenzako
anapokukosea msameheane, mkifanya hivyo mtakuwa mmemshinda shetani, na ndio
maana Kanisa Katoliki halichachi
kutokana na kuwa na misingi imara ya upendo,” amefafanua.
Comments
Post a Comment