Wakiwa na mashaka na ukristo wako, wema na kazi zako vikushuhudie
“HUKO
Antiokia, ndiko kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo” (Matendo 11:26)
“Kama
tungetenda kama wakristo kweli, pansigekuwepo na watu ambao siyo wakristo,”
alisema Mt. Papa Yohane XXII. Ni katika
mtazamo huo huo, Soame Jenyns alisema: “Kama nchi za kikristo zingekuwa nchi za
kikristo, pasingekuwepo na vita.” Kama
ungekamatwa kwa kuwa mkristo, je pangekuwepo na ushahidi wa kutosha wa kukutia
hatiani?
Je,
kuna ushahidi gani wa kuwa wewe ni mkristo. Mkristo kama mshumaa lazima atulie
wakati huo huo anawaka mapendo. Mkristo anaonesha ukristo.
Ukristo:
“Ni wema nyumbani. Katika biashara ni ukweli. Katika jamii ni adabu. Kazini ni
kutenda haki. Kwa wenye shida ni huruma. Ni msaada kwa wadhaifu. Upinzani dhidi
ya waovu. Ni imani kwa wenye nguvu za kimaadili. Ni ‘msamaha’ kwa wakosefu. Ni
furaha kwa waliofanikiwa. Ni uchaji na imani kwa Mungu,” alisema mtu fulani.
Ukristo ni kuwa mkristo pale ulipo. Usipokuwa mkristo pale ulipo huwezi kuwa
mkristo popote. Wanafunzi walioitwa wakristo walikuwa kwanza wakristo Antiokia.
Mtoto
wa miaka minne alimuuliza mama yake: “Hivi mama Yesu unayenielezea habari zake
kila mara ni mwema kama wewe? Mama alimjibu: “Yesu ni mwema sana mimi
najitahidi kumuiga.” Mtoto alijibu: “Kama ni hivyo nitampenda.” Wema ni sifa ya
kuwa mkristo. Tunaambiwa juu ya mkristo Barnaba: “Barnaba alikuwa mtu mwema na
mwenye kujaa Roho Mtakatifu na imani. Kundi kubwa la watu lilivutwa kwa Bwana”
(Matendo 11:24).
Sifa
nyingine ya mkristo ni kuwatia wengine moyo. Barnaba maana yake mwana wa kutia
moyo. Alimtia moyo Paulo. Mtu akinunua pikipiki mtie moyo. Usiseme, “Inafanana
na yangu.” Ukaishia hapo. Mtu akinunua nguo nzuri mpongeze. Usiseme, “Nilinunua
kama hii mwaka 1970.” Mwanafunzi anayepata maksi za chini, mtie moyo.
Dante
Gabriel Rossetti mshairi na mchoraji maarufu wa karne ya 19 alitembelewa na
mzee fulani. Mzee huyo alikuwa amebeba picha na michoro mbali mbali ambazo
alitaka zihakikiwe ili kujua kama ni mizuri. Rossetti alizitazama kwa makini
sana. Baada ya kuziangalia chache alisema ukweli kuwa michoro si mizuri. Mgeni
huyo alisikitika sana. Alitoa michoro mingine na kumwambia kuwa imechorwa na
kijana mwanafunzi.
Rosseti
alizitazama na kuchangamka na kuwa na furaha na kusema, “Michoro hii ni mizuri.
Kijana huyo aliyezichora ana kipaji kikubwa. Apewe kila msaada na kutiwa moyo
katika wito wake wa kuwa mchoraji. Kijana huyo ni nani? Ni mtoto wako?” Mzee
alijibu. “Siyo mtoto wangu ila ni mimi miaka arobaini iliyopita. Kama miaka
hiyo ningesikia maneno mazuri kama haya ningekuwa mchoraji mzuri sana.
Hata
kama watu hawakutii moyo jitie moyo. Kuna mwanafunzi ambaye alikuwa hapendwi na
wenzake. Aliitwa Siima. Hata walimtania kuwa hata kivuli chake hakimpendeki
hakiko tayari kumfuata. Siku moja alikuwa anaadhimisha Siku yake ya Kuzaliwa.
Alijua kuwa hakuna atakayemwandikia kadi ya pongezi.
Alifanya
kitu fulani. Wenzake walipokuja kumtembelea na kumkejeli walikuta kadi kumi na
mbili. Walishangaa. Walipozisoma zikuwa zote zinatoka kwa mtu mmoja. Kutoka kwa
Siima kwenda kwa Siima.
Kazi
zako zikushuhudie. “Kazi ninazofanya mimi kwa jina la Baba yangu
zinanishuhudia” (Yohane 10:25). Watu walikuwa wamemuuliza Yesu kama ndiye Kristo.
Kazi zake za huruma zilimshuhudia. Wewe kama ni mkristo kazi zako zikushuhudie.
Matendo ya huruma yakushuhudie. Wewe kama ni daktari wa binadamu, kazi zako
zikushuhudie.
Wewe
kama ni mwalimu kazi zako zikushuhudie. Wewe kama ni mwanasiasa kazi zako zikushuhudie.
Pilato alipoambiwa kuwa kuna watu wanasema anaimba vibaya. Alijibu, “Nitafanya
mazoezi na kuimba vizuri hakuna atakayewaamini.”
Kazi
zako zifanye watu wasiamini mabaya yanayosemwa juu yako. Kuna watu
waliosema vibaya juu ya Bwana Yesu
alipokuja anakula na kunywa tofauti na Yohane Mbatizaji lakini kazi zake nzuri
zilimshuhudia.
Sala:
Ee Bwana Yesu nisaidie niwe mkristo kweli, niwe sauti ambayo kwayo
utazungumza,niwe moyo ambao kwao utapenda, niwe mikono ambayo kwayo utasaidia.
Amina.
Comments
Post a Comment