Tanzania inapoteza asilimia 1 ya pato la Taifa kutokana na uduni wa mazingira
IMEELEZWA kuwa ili kuendana na uchumi wa kati
ambao nchi imedhamiria kufikia ifikapo mwaka 2025 upo umuhimu mkubwa wa kuwa na
miundombinu ya usafi inayoakisi hali ya uchumi wa kati.
Hayo
yameelezwa hivi karibuni mkoani hapa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii
,Jinsia,Wazee na Watoto Mh.Ummy Mwalimu pamoja na wadau wa masuala ya usafi wa
mazingira, ambapo kwa pamoja wamepitisha azimio la kutambulisha awamu ya pili
ya kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira.
Pamoja na
mambo mengine kampeni hiyo inahusisha maboresho ya vyoo vya kisasa, kunawa
mikono kwa kutumia sabuni, kutibu maji ya kunywa, usafi mashuleni, usafi kando
ya barabara kuu na kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Akitilia
mkazo suala la usafi wa mazingira Mwalimu amesema kujisaidia hovyo imekuwa ni
tatizo kubwa kwa zaidi ya miaka 25 ambapo kulingana na ripoti ya mwaka 1990
inaonyesha jumla ya asilimia 10 ya watu waishio vijijini hawakuwa na vyoo huku
zaidi ya asilimia 55 ya watanzania walikuwa wakitumia vyoo duni vyenye madhara
kiafya na uchumi.
“Taifa kwa
ujumla linahitaji kupiga vita matumizi ya vyoo duni pamoja na tabia ya
kujisaidia hovyo ili kuondokana na magonjwa ya kuhara, kipindupindu, minyoo na
nimonia,” amesema.
Mbali na
hayo amesema kuwa hali duni ya usafi, huigharimu nchi asilimia moja ya pato la
taifa kila mwaka na kwamba uchafu huchangia kwa kiasi kikubwa kudumaa kwa
watoto nchini kunakosababishwa na kuhara ambapo jumla ya watoto milioni 2.7
huathirika.
Hata hivyo
kulingana na ripoti ya Benki ya dunia inaonyesha kuwa Tanzania inapoteza
asilimia 1 ya pato la ndani ya taifa kutokana na hali duni ya usafi wa
mazingira.
Ripoti
inazidi kueleza kuwa kiasi hiki ni kikubwa sana kwa taifa linalotarajia kuwa na
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na hivyo wizara kutoa wito kwa wananchi wote
kuunga mkono serikali kuhakikisha upatikanaji wa vyoo bora.
Kwa mujibu
wa utafiti uliofanywa na shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto
(UNICEF) takwimu zinaonesha kuwa dunia inapoteza watoto milioni 1.7 kila mwaka
kutokana na magonjwa ya kuhara na nimonia.
Hata hivyo
ripoti hiyo inaeleza kuwa vifo hivyo vinaweza kuzuilika kwa kunawa mikono kwa
sabuni kila baada ya kutoka chooni ikiwa ni pamoja na serikali kuelekeza bajeti
ya mapato katika masuala ya mazingira kwa ujumla.
Kampeni ya
kitaifa ya usafi wa mazingira ilizinduliwa mwaka 2012 ili kuongeza kasi ya
kuboresha hali ya usafi wa mazingira nchini ikiwa ni pamoja na kuunganisha
nguvu ya pamoja na wadau wote kuhamasisha jamii kuwa na vyoo bora.
Comments
Post a Comment