Wakazi Ngorongoro waiomba serikali kuwanusuru njaa
WANANCHI wanaoishi
katika Tarafa ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wameiomba serikali
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa Ngorongoro (NCAA) kuweka
utaratibu mbadala wa kuwalipa kiasi cha fedha kinachotokana na utalii ili
kuwanusuru na njaa kali inayowakabili.
Tarafa hiyo
yenye zaidi ya wakazi 82,000 kati yao ni asilimia tatu tu ndio wenye uwezo wa
kufuga, huku asilimia 97 wakiwa hawana uwezo wa kufanya chochote kutokana na
wananchi hao kuzuiwa kufanya shughuli zozote za kilimo ndani ya hifadhi hiyo.
Mwenyekiti wa
Baraza la Wafugaji Ngorongoro ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nainokanoka,
Edward Maura akizungumza katika kikao cha kuwanusuru wananchi hao na baa la
njaa, amesema wananchi wa tarafa hiyo wapo katika hali ngumu kimaisha kutokana
na kutokuwa na njia yoyote mbadala ya kuwaingizia kipato huku wakitegemea chakula cha msaada kutoka NCAA ambacho
hakiwatoshelezi.
“Pamoja na
kuahidiwa kuletewa chakula wakati mwingine hakifiki kabisa na hakitoshi,
tunaiomba sana serikali kwa kushirikiana na NCAA waweke utaratibu wa kutulipa
fedha zinazotokana na utalii kila mwezi angalau Sh 300,000 kwa kila kaya ili
waweze kujikimu kimaisha, vinginevyo maisha yanazidi kuwa hatarini,” alieleza.
Naye Meneja
mipangowa Baraza la Wafugaji Wanawake (PWC), Alais Melau amesema wamekuwa
wakivijengea uwezo vikundi vya wakina mama kwa kuwapatia mikopo na kuwaanzishia
miradi midogo midogo ya kujikwamua kiuchumi.
Melau amesema
wamewagawia wananchi hao mbuzi 900 na kuwasaidia kuanzisha maboma ya
kiutamaduni ambayo wamekuwa wakifanya shughuli za utalii na kujipatia kipato
cha kuendeleza familia zao.
NayeNaibu
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro,
William ole Nasha amesema matatizo
yanayowakabili wananchi wa tarafa hiyo ni kutokana na kuwepo kwa sheria
ya ardhi inayowanyima uhuru ndani ya hifadhi hiyo.
Amesema katika
kuhakikisha kuwa wananchi hao wanaondokana na njaa, wameandaa utaratibu wa
kuwaletea wananchi chakula na kuwauzia kwa bei nafuu ya soko ili kila mwananchi
amudu gharama za kununua chakula hicho.
Comments
Post a Comment