WAWATA NA CARITAS WAWAPA MBINU WANAWAKE MBEYA


 IMEELEZWA  kuwa wanawake ni nguzo ya familia,jamii na Taifa lolote duniani ,hivyo hawapaswi kujiona wanyonge  na badala yake  wajitume katika shughuli mbalimbali za kujipatia kipato bila kujibakisha ili waweze kuzilea vyema familia katika maadili mema  na hata kufikia hatua ya kulitegemeza Kanisa.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Jinsia,,Vijana na  Watoto, Idara ya Caritas  na Maendeleo,Jimbo Katoliki la Mbeya,Praxeda Manyuka katika ziara yao ya kuwatembelea Umoja wa Wanawake wa Kanisa la Moyo Mtakatifu  wa Yesu, Parokia ya Ilambo kujionea shughuli za maendeleo  wanazozifanya  ili kujiingizia kipato.

Praxeda amesema kuwa  wanawake kama walezi wa familia  wanapaswa kujituma katika shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato ili waweze kuilea vema familia,kaya  na kwamba wanao uwezo mkubwa wa kulitegemeza kanisa.

"Akina mama ndiyo nguzo ya familia,mnapaswa kujituma katika shughuli mbalimbali za maendeleo...tunaamini mwanamke licha ya kuwa mzazi pia ni mlezi  na nguzo ya familia,nguzo ikiteteleka nyumba haiwezi kuwa imara,kwa hiyo endeleeni kubuni miradi mbalimbali ya ujasiliamali na tujiwekee malengo,"amesema Praxeda.

Katika ziara hiyo Idara ya Caritas na Maendeleo,Jimbo Katoliki la Mbeya kwa kushirikiana na WAWATA Parokia ya Ilambo wamekubaliana kuweka mpango kazi kuanzia mwezi me,2017 hadi disemba 2018 kuhakikisha wanafanya maandalizi ya mashamba na kufanya ufuatiliaji ikiwemo na kutoka mafunzo kwa nadharia na vitendo.

Mpango kazi mwingine  ilikuwa ni  kuhakikisha  WAWATA  wanakamilisha ujenzi wa mabanda bora  na ufugaji wa Kuku asilia,utengenezaji wa unga wa lishe  na Batiki sanjari na bajeti ya shughuli zote za ujasilimali walizokubaliana.


Na, Thompson Mpanji, Mbeya





Picha katika matukio tofauti zikionesha baadhi ya wanawake wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki (WAWATA) Parokia ya Ilambo,baada ya baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Caritas na Maendeleo, Jimbo Katoliki Mbeya walipotembelea parokiani humo kuonana na  wanawake, kuzungumza na kufundishana  shughuli za ujasiliamali za kuweza kulitegemeza Kanisa,familia na jamii kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU