YALIYOJIRI KATIKA WOSIA WA KITUME:FURAHA YA UPENDO!

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko Furaha ya Upendo ndani ya familia ”Amoris Laetitia” ni habari njema kwa familia ya Mungu. Hii ni zawadi kubwa ambayo Baba Mtakatifu Francisko analizawadia Kanisa baada ya safari ya miaka miwili ya maadhimisho ya Sinodi za maaskofu kuhusu familia zilizoadhimishwa mjini Vatican kati ya mwaka 2014- 2015. Huu ni wosia unaogusia furaha ya upendo ndani ya familia, changamoto na kinzani zinazoendelea kuiandama familia ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Hii ni changamoto ya toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho, ili kweli familia iweze kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anakaza kusema Kardinali Baldisseri ni habari njema kwa familia hususan familia zenye madonda na makovu ya maisha ya ndoa na zile ambazo kwa kweli zinanyanyasika na kudhalilishwa kutokana na sababu mbali mbali.
Kardinali Baldisseri wakati wa uzinduzi wa Wosia wa Furaha ya Upendo ndani ya familia amekazia kuhusu jina la wosia huu, namna ya kuusoma ili kuweza kuufahamu zaidi; muundo wake; nyaraka rejea na mambo muhimu yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Furaha ya Upendo ndani ya familia.
Wosia huu umegawanyika katika sura tisa na mwishoni kuna sala maalum ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Ni wosia unaojikita katika Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia: upendo ndani ya familia unaogeuka kuwa ni chemchemi ya maisha mapya. Sura ya tano ni kiini cha wosia huu wa kitume inayofuatiwa na maelekezo ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ilikujenga na kuimarisha familia mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Baba Mtakatifu anatoa mchango wake juu ya umuhimu wa elimu na makuzi kwa watoto; umuhimu wa familia kujikita katika huruma ya Mungu na mang’amuzi sahihi kwa familia ambazo haziendani na mafundisho ya Kristo kwa waja wake, mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha wosia wake wa Furaha ya Upendo ndani ya familia kwa kutoa mwongozo wa tasaufi ya familia.
Kardinali Baldisseri anasema Nyaraka Rejea zilizotumika katika wosia huu ni ushuhuda wa utume wa Baba Mtakatifu Francisko unaofumbatwa katika muhtasari wa safari ya maadhimisho ya Sinodi za maaskofu kuhusu familia. Wosia huu unachota utajiri wake mkubwa kutoka katika Waraka wa Mababa wa Sinodi ya mwaka 2014 na Waraka elekezi wa Mababa wa Sinodi ya mwaka 2015. Baba Mtakatifu anachota utajiri wa mafundisho ya Mababa wa Kanisa, wanataalimungu mahiri pamoja na waandishi maarufu wa nyakati hizi, bila kusahau nyaraka za Mababa wa Kanisa, Katekesi kuhusu: familia, upendo wa binadamu; Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki; Mungu ni Upendo, Injili ya furaha pamoja na kuchota utajiri unaofumbatwa kutoka katika nyaraka mbali mbali za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.
Kardinali Baldisseri anakaza kusema, mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu katika Wosia huu ni mwelekeo chanya wa uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, kwani kila tendo la upendo ni utenzi wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, mwaliko kwa wanandoa kukuza na kudumisha fadhila ya upendo ushuhuda wa imani tendaji! Maaskofu wanahamasishwa kuwa ni kielelezo na mfano wa Kristo mchungaji mwema anayejitaabisha kufunga, kuganga na kuponya madonda ya waja wake, anawatambua wanakondoo wake na anawaita kwa majina.
Maaskofu wanapaswa kutambua kwamba, wamepewa dhamana ya huduma ya kichungaji na wanawajibu wa kutoa maamuzi kwa waamini ambao amekabidhiwa na Mama Kanisa. Maaskofu kwa kushiriana na wakleri na wahudumu wa shughuli za kichungaji walioandaliwa vyema wanaweza kutoa huduma makini kwa familia zinazoogelea katika shida na magumu ya maisha ya ndoa! Maaskofu wanapaswa kusoma alama za nyakati na kutoa maamuzi makini kadiri ya kesi iliyoko mbele yao na wala hakuna mwongozo wa jumla kwa kila kesi.
Kanisa liwe ni mahali pa kuwahusisha watu wote na wala si kuwatenga. Mapadre wawasaidie waamini wanaoogelea katika shida za maisha ya ndoa, ili kuweza kupata mang’amuzi mapana zaidi kwa njia ya tafakari, toba na wongofu wa ndani. Ushuhuda wa waamini waliotalakiana na kuamua kuoa au kuolewa tena unapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa ili kuona ikiwa kama kumekuwepo na jitihada za upatanisho, mahusiano yaliyopo kati ya waamini hawa na Jumuiya ya Kikristo na ni mfano gani ambao vijana wanaojiandaa kwa maisha ya ndoa na familia wanaweza kuuona kutoka kwao! Huu ni mchakato wa majadiliano unaojikita katika kiti cha huruma, majiundo makini na hatimaye, ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Wosia huu unatoa mkazo wa pekee kwa maandalizi ya wanandoa watarajiwa, ili Kanisa liweze kuwapatia majiundo kamili kuhusu Sakramenti ya Ndoa ili waweze kuanza mchakato wa ujenzi wa msingi wa ndoa imara na thabiti. Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia; utajiri wa maisha, mang’amuzi na mifano hai ya wanandoa iwasaidie wanandoa watarajiwa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia.
Wosia unagusia pia ndoa za Serikali na uchumba sugu; hii ni fursa makini ya kuweza kuwasaidia waamini katika mazingira kama haya kuanza mchakato wa kufunga Ndoa. Kwa wanandoa wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, wasaidiwe kuonja huruma, upendo na uwepo wa karibu wa Kanisa katika maisha yao ushuhuda endelevu wa huruma ya Mungu na kwamba, hakuna sababu ya kuwatenga watu kwani kufanya hivi ni kwenda kinyume cha Injili ya Kristo!
Kuna walimwengu wanaogelea katika dimbwi na kinzani, machafuko, mipasuko na migawanyiko kama inavyojionesha hata katika maisha ya ndoa na familia. Yesu, kielelezo cha Msamaria mwema kwa binadamu anapenda kuwaonesha wote hawa huruma na upendo na mshikamano wake; huruma ambayo kimsingi ni haki ya Mungu inayomkirimia mwamini matumaini mapya. Huruma ya Mungu ni utimilifu wa haki na ushuhuda angavu wa ukweli wa Mungu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI