KUADHIMISHA PASAKA KWA SIKU NANE
KUADHIMISHA PASAKA KWA SIKU NANE
TUANZE kwa kujikumbusha neno Pasaka. Mwenyezi Mungu
alilikomboa taifa lake Waisraeli kutoka utumwa wa Farao nchini Misri kwa tendo la Pasaka alipopita kuwaua
wazaliwa wa kwanza wa wanadamu na wanyama katika nyumba za Wamisri ndipo Farao
alipowaacha huru Waisraeli waondoke(Kut 12:1-14).
Tendo
hili la Mwenyezi Mungu kuwakomboa watu wake kutoka Misri lilikuwa kubwa na
muhimu sana katika historia ya Waisraeli; waliliadhimisha kila mwaka, na
walipofanya vile waliona ukombozi wao
anatendeka upya. Pasaka ni kupita kwa Bwana (Kut.12:12-13 ).
Mateso kifo na
Ufufuko
Kwetu
Wakristo Pasaka ni pia kupita kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Baada ya kuadhimisha Karamu ya mwisho na kuweka Sakramenti ya Ekaristi, Upadri
na amri ya Mapendo, Bwana Yesu
alianza Pasaka yake yaani kuteswa, kufa
msalabani, kuzikwa na hatimaye kufufuka kwake.
Pasaka
isieleweke tendo la Ufufuko pekee, bali kupita kwake Bwana katika matendo hayo yote.
Ni kwa sababu hiyo kilele cha kuadhimisha Liturujia yetu ni Siku Tatu Kuu za
Pasaka katika siku ambazo tunaadhimisha matendo hayo yote. Tendo la kufufuka ni
kilele
au upeo wa Pasaka, kupita kwa Bwana.
Kwani hatuwezi kuadhimisha Ufufuko bila mateso na kufa kwake.
Kutokana
na Pasaka kuwa kilele cha Ukombozi wetu Kanisa huadhimisha Sherehe hiyo kwa
namna ya pekee sana kama siku moja ndefu ya siku nane. Siku nane hizo
huitwa Oktava.
Neno
hilo hutokana na neno la kilatini octo maana yake nane. Kwa
hiyo Oktava
ya Pasaka ni siku nane za kuadhimisha Pasaka tangu Dominika ya Pasaka
mpaka Dominika ya pili ya Pasaka. Hakuna Maadhimisho mengine siku hizo bali ni PASAKA TU.
Asili ya Oktava
Kanisa
imepokea utaratibu wa kuadhimisha Oktava kutoka kwa Waisraeli. Wao
waliadhimisha sherehe zao kuu za kidini
kwa muda wa siku saba au nane. Sikukuu ya Pasaka ambayo tumeitaja hapo juu iliadhimishwa kila
mwaka kwa muda wa siku saba na muda huo walikuwa wakila mikate isiyotiwa
chachu.
Sikukuu
ya Vibanda pia ilikuwa kati ya sikukuu kubwa katika dini ya Waisraeli.
Walijenga vibanda na kuishi humo kwa siku nane wakiadhimisha tendo la
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa safari yao kutoka Misri: kwani walipokuwa njiani
wakitembea kwenda Isareli walifanya vituo sehemu mbalimbali. Katika vituo hivyo
walijenga vibanda na kuishi humo mpaka walipoamua kuendelea na safari yao.
Kutokana
na hali hiyo Liturujia ya Kanisa Katoliki imepokea utaratibu wa kuadhimisha
Sherehe ya Pasaka kwa namna ya pekee kwa Siku nane.
Katika
historia, karne za Kati, kulikuwa Sikukuu kadhaa zilizoadhimishwa kwa Oktava
lakini katika marekebisho Oktava nyingi zikaja kufutwa. Tumebaki na Sherehe
mbili tu ambazo tunaadhimisha kwa Oktava katika Liturujia ya Kanisa, Noeli au
Krismasi na Pasaka.
Oktava ya Noeli imeruhusu kuwa na
sikukuu kadhaa zinazoadhimishwa katika siku hizo nane lakini Oktava hii ya Pasaka hairuhusu Sikukuu
ye yote. Iwapo Sherehe yoyote inaangukia wakati wa Juma Kuu au Oktava hupelekwa
mbele na kuadhimishwa Jumatatu baada ya kumaliza Oktava ya Pasaka.
Tunaadhimisha
Juma Kuu au Juma Takatifu kuanzia Dominika ya Matawi ya Mateso ya Bwana na
kufuatiwa na Ufufuko wake kwa muda wa
siku nane.
Hii ndiyo Siku
Katika
kila siku ya Oktava ya Pasaka Liturujia husisitiza: Hii ndiyo Siku aliyoifanya
Bwana, tufurahi na kuishangilia, Aleluya(Zb 118:24). Maneno hayo humaanisha
kwamba siku nane ni kama siku moja ndefu yenye urefu unaolingana na
siku nane.
Kila
siku ni kama Dominika ile ya Pasaka. Kwa maneno mengine: Ukuu na hadhi ya
Dominika ile ya Pasaka ni kubwa hivi inaadhimishwa katika siku hizo nane. Ndiyo
maana kila siku katika siku nane hizo tunasali: Hii ndiyo
siku
aliyoifanya Bwana
...Inafaa sana kuliimba Shangilio hilo kila
linapotokea, iwe wakati wa Misa au wakati wa Masifu ya Asubuhi hata ya Jioni;
kwani ni ujumbe mkubwa katika Oktava ya Pasaka.
Sekwensia ya Pasaka
Katika
siku nane hizo kuu za Pasaka wakati wa Adhimisho la Ekaristi ni vizuri kuimba
shairi hilo muhimu Victimae Paschali ndivyo
sekwensia hiyo muhimu inavyoanza kwa kilatini. Mtunzi wake kwa uhakika
hafahamiki lakini kwa hakika limetungwa mnamo karne ya 11 au 12.
Beti wa
kwanza na wa pili unatoa wito kumtukuza Mwanakondoo aliyewakomboa kondoo wake.
Huyo Mwanakondoo ni Kristo asiye
dhambi. Beti zinazofuata ni mazungumzo kati ya mitume na Maria Magdalena.
Hatimaye linaishia na sifa kwa Mfalme mshindaji na kumwomba atuhurumie.
Mshumaa wa Pasaka
Jambo
jingine muhimu sana ambalo ni ishara kubwa
katika kipindi chote cha Pasaka ni mshumaa
wa Pasaka. Tunakumbuka Alhamisi kuu baada ya kuhamisha Ekaristi nguo
na mishumaa ziliondolewa altareni ishara ya Bwana wetu kuingia katika mateso
yake.
Mshumaa
wa Pasaka unaowashwa baada ya kubariki moto mpya nje ya kanisa ndio unaoongoza
maandamano kuingia kanisani ishara ya Kristo anayefukuza giza la dhambi.
Kwa namna ya pekee katika siku hizo nane mshumaa wa Pasaka uwe unawashwa wakati
wa Maadhimisho yote ya Liturujia, iwe adhimisho la Ekaristi au Masifu ya
Asubuhi au Masifu ya Jioni.
Ni
jambo la kupongeza sana kuona parokia nyingi waamini wanashirikishwa katika
kusali au kuimba Masifu ya Asubuhi kabla ya Misa. Basi mshumaa huo wa Pasaka
uwe unawashwa sio tu wakati wa Misa inapoanza, bali bali mwanzoni mwa Masifu
hayo ya Asubuhi, ishara ya kumshangilia Yesu Mfufuka. Inapoanza misa ndipo
iwashwe mishumaa ya altareni.
Kuwaombea Wakristo wapya
Wakristo
waliobatizwa katika Mkesha wa Pasaka na kuvishwa nguo nyeupe walitakiwa kuja
kanisani kila siku katika Oktava wakiwa
na nguo zao nyeupe.
Sala za
Misa katika Oktava mara nyingi zinawataja hao kwamba waizingatie kwa dhati hiyo
imani waliyoipokea. Katika Oktava, Kanisa lilikuwa likiwaombea kwa namna ya
pekee wakristo hao wachanga ili wawe imara katika maisha yao mapya.
Kwa mara ya mwisho walipotakiwa kuja kanisani
na nguo zao nyeupe ilikuwa Dominika ya pili ya Pasaka, ndiyo kilele cha Oktava. Kutokana na kuja kanisani na nguo
nyeupe basi Dominika hiyo ikaja kujulikana kama Dominika nyeupe, jina ambalo
limetumika mpaka miaka ya karibuni. Papa Benedikto XVI (kumi na sita)
aliipa Dominika hiyo jina jipya:
Dominika ya Huruma ya Mungu.
Katika
kuadhimisha Oktava ya Pasaka kulikuwa na mkazo wa pekee kuwahimiza wakristo
wapya waliobatizwa Mkesha wa Pasaka pia wakristo wengine kushiriki misa hasa
juma hilo la Oktava.
Siku
hizo zilikuwa pia nafasi kwa wakristo hao wachanga kupata mafundisho yaliyowasaidia kuimarisha imani waliyoipokea.
Hatuna budi sote kuimarisha imani yetu kwa kushiriki Misa wakati wa Pasaka.
Comments
Post a Comment