INJILI YA AMANI KWANZA..
Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Chama cha kitume cha “Pax Christi” hivi karibuni linaendesha mkutano wa kimataifa kuhusu Mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu vita na amani sanjari na kuachana na dhana ya “vita halali na ya haki”, ili kujenga na kudumisha kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, ili kupambana na mauaji ya kimbari. Wajumbe wa mkutano huu katika tamko lao wamekazia umuhimu wa Kanisa Katoliki kujikita zaidi na zaidi katika kukuza na kudumisha Injili ya amani mintarafu Maandiko Matakatifu.
Mpango mkakati huu sasa unapaswa kufundishwa seminarini, kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Wajumbe wanasema, ulimwengu mamboleo unasheheni hofu na wasi wasi ya vita, athari za myumbo wa uchumi kimataifa, vita na mipasuko ya kijamii, changamoto kwa Wakristo kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya amani, ujumbe uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Kanisa linahamasishwa kuwa ni chombo cha Injili amani inayojikita katika ushuhuda wa mchakato wa uponyaji na upatanisho kati ya watu wa mataifa na kazi ya uumbaji.
Wajumbe wa mkutano huu wa kimataifa wameshirikisha mang’amuzi, changamoto na mafanikio yaliyokwisha kufikiwa katika mchakato wa upatanisho, haki na amani huko Uganda, Colombia; wameangalia kwa matumaini mgogoro kati ya Israeli na Palestina; umuhimu wa kujikita katika malezi na majiundo ya amani nchini Ufilippini na kwamba, Injili ya amani ina mvuto mkubwa kadiri ya tafiti za kisayansi zilizofanywa hivi karibuni. Huu ni muda muafaka kwa Kanisa kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa Injili ya amani duniani; kwa kuwekeza katika rasilimali watu na majiundo makini yatakayosaidia kukuza na kudumisha msingi ya haki, amani na maridhiano, daima Kristo Yesu akiwa ni mfano bora wa kuigwa!
Yesu katika maisha na utume wake, aliwafundisha wanafunzi wake kuonesha upendo na msamaha kwa adui zao kama kielelezo cha kuheshimu na kuthamini utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Aliwataka wafuasi wake kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani; kutubu, kusamehe na kuwa na huruma, daima mwanadamu akipewa kipaumbele cha pekee. Yesu alionesha na kushuhudia Injili ya amani pale alipomsamehe mwanamke aliyekamatwa akizini; usiku ule alipokamatwa kabla ya kuanza Njia ya Msalaba, alimwambia Mtume Petro kurudisha upanga mahali pake, maana wote waushikao upanga wataangamia kwa upanga.
Hiki ni kielelezo cha nguvu ya huruma na upendo iliyokuwa inatenda kazi ndani mwa Yesu, ufunuo wa Ukweli na Huruma ya Baba wa milele, uliofikia kilele chake kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Maisha, maneno na matendo ya Yesu yalishuhudia chemchemi ya huruma, amani na utulivu, changamoto kwa familia ya Mungu kujenga na kudumisha Injili ya amani duniani. Neno la Mungu kamwe lisitumiwe tena kuhalalisha uhalifu, vita halali na ya haki, kwani kufanya hivi ni kwenda kinyume cha kiini cha Injili ya amani na matokeo yake ni vita, dhuluma, nyanyaso, unyonyaji na vitendo vya kibaguzi. Hakuna vita halali na ya haki kwani kuendelea kushikilia dhana hii ni kwenda kinyume cha kanuni maadili na Mafundisho Jamii ya Kanisa ambayo ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Injili ya amani inafumbatwa katika haki, amani na maendeleo ya watu na kwamba, vita ni dhana ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II. na kwamba, upendo kwa adui ni kiini cha ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu, kama alivyokazia Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Papa Francisko anafafanua kwamba, nguvu ya Mkristo inajikita katika ukweli na upendo na kwamba, imani na vita ni mambo mawili yanayosigana sana na hapa, kuna haja ya kujikita katika Injili ya amani sanjari na kufuta adhabu ya kifo inayokumbatia utamaduni wa kifo!
Wajumbe wanasema, sasa Kanisa Katoliki halina budi kuachana na dhana ya vita halali na ya haki na kuanza kujikita katika Injili ya amani inayofumbata haki, nyenzo muhimu sana kwa wajenzi wa amani duniani. Kanisa liendelee kufundisha na kuhamasisha Injili ya amani, haki na huruma inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wake, kwa kushuhudiwa na familia yote ya Mungu katika ujumla wake. Kanisa lisaidie mchakato wa haki, amani, uponyaji na upatanisho kati ya watu, kwa kuibua mbinu mkakati wa ujenzi wa Injili ya amani.
Kanisa likuze na kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene, kisiasa na kidiplomasia ili kudumisha Injili ya amani. Sasa Kanisa linapaswa kuachana na dhana ya vita halali na ya haki, ili kudhibiti vita, utengenezaji na matumizi ya silaha za nyuklia duniani. Kanisa liendelee kuunga mkono wajenzi wa haki na amani, daima likiomba msaada na karama za Roho Mtakatifu ili kupambana na changamoto za ulimwengu mamboleo. Kanisa liwe kweli ni mfano, chombo na shuhuda wa Injili ya amani duniani, kwa kufundisha na kuimwilisha Injili hii katika uhalisia wa maisha na utume wake. Wajumbe wa mkutano huu wanasema, wanatumaini kwamba, wataendelea kushirikiana na Vatican na Kanisa katika ujumla wake katika kukuza na kudumisha Injili ya amani duniani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment