Kuviringisha jiwe ni tendo la huruma
Kuviringisha jiwe ni
tendo la huruma
Faustin Kamugisha
NI
nani atakayevingirisha lile jiwe? Ni swali tunalojiuliza kila mara
katika maisha yetu. Barabara ya maisha ambayo haina mawe ya kuviringisha
haiendi popote. Ni nani atakayevingirisha lile jiwe? Mungu ana jibu.
Tunasoma
hivi katika Injili ya Marko: “Wakasemezana
wao kwa wao. Ni nani atakayevingirisha lile jiwe mlangoni pa kaburi? Hata
walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuviringishwa; nalo lilikuwa
kubwa mno” (Marko 16: 3-4).
Kuna
mtoto wa miaka saba aliyejaribu kunyanyua jiwe akashindwa. Baba yake alikuwa
amemtazama anavyoangaika kunyanyua jiwe. Alimwambia, “Tumia nguvu zako zote.”
Mtoto alijibu, “Baba nimetumia nguvu zangu zote.”
Baba
alirudia kusema, “Tumia nguvu zako zote.” Mtoto alijibu, ““Baba nimetumia nguvu
zangu zote, nimeshindwa kulinyanyua.” Baba alimwambia, “Hujatumia nguvu zako
zote kwa vile hujaomba nikusaidie kunyanyua.” Mungu anaweza kuusaidia kuviringisha jiwe.
Katika
maisha yetu Mungu Baba mwenye huruma
anatuma malaika wa kuviringisha mawe makubwa katika maisha yetu. Alimtuma
malaika wa ufufuko kuviringisha jiwe kutoka kaburini.
Peter
Marshall (1902-1949) mhubiri wa kiamerika alisema, “Jiwe liliondolewa kutoka mlango wa kaburi, si kumruhusu Yesu atoke bali
kuwawezesha mitume waweze kuingia.”
Tunasoma
hivi: “Akainama na kuchungulia akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini
hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi;
akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwako kichwani pake”
(Yohane 20: 5-7). Mtume
Yohane
aliweza kuchungulia ndani kwa vile jiwe lilikuwa limeviringishwa. Mtume Petro
aliweza kuingia ndani kwa vile jiwe lilikuwa limeviringishwa.
Tunasoma
katika Injili ya Luka kuwa “Wakalikuta
lile jiwe limeviringishwa mbali na kaburi” (Luka 24:2). Hao walikuwa ni Maria
Magdalene na Yoana na Maria mamaye Yakobo. Malaika wa ufufuko aliviringisha
jiwe.
“Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa
sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akaliviringisha lile
jiwe akalikalia” (Mathayo 28:2).
“Jiwe liliviringishwa baada ya ufufuko kwa ajili ya
wanawake, ili waweze kuamini kuwa Bwana amefufuka, kwa kuona kaburi bila
mwili,” alisema Mtakatifu Yohane Kyrisostomu
Jiwe la kifo limeviringishwa: Kwa kuondoa jiwe kaburi la Yesu
lilibaki mlango wazi kuonesha kuwa kaburi si gereza tena kuna kufufuka. Kifo si
nukta bali ni alama ya mkato. Meli ikianza safari yake toka Kisumu hadi Mwanza
Tanzania wale walioko Kisumu wanasema meli imeenda.
Wale
walioko Tanzania wanaoiona kwa mbali wanasema meli imekuja. Mtu akiaga dunia
tunasema “Ameenda.” Walioko mbinguni au toharani wanasema, “Amekuja.”
Hivyo kifo sio kituo bali ni koma. Kwa vile jiwe la kifo limeviringishwa Kwetu kifo sio ukuta ni mlango.
Kwetu kifo sio kizuizi bali ni daraja. Mbio za
sakafuni huishia ukingoni. Mbio zetu haziishii ukutani bali tunapitia zinafika
mlangoni na tunapita. Hadithi ikiwa nzuri sana kwenye gazeti inakatizwa na
chini yake yanaandikwa maneno itaendelea toleo lijalo.
Toleo Lijalo ni motoni, mbinguni au purgatory. Kuna referee aliyeaga dunia akaenda
motoni. Huko alikuta uwanja mzuri sana na watu wamejipanga kucheza mpira
alifurahi sana. Timu mbili ziliingia yeye akashika kipenga.
Wachezaji
wakasalimiana na kushika nafasi zao. Yeye referee akaulizia mpira wapi.
Aliambiwa huku ndio maana kunaitwa motoni. “The hell of it” ni kwamba hakuna
mpira. Huna hamu ya chakula na hauwezi
ukala. Kuna kitu kinakosekana.
Jiwe lililoviringishwa lina ujumbe wa huruma: Kwa kawaida mawe ya kaburini
(tombstones) huwa na ujumbe. Ujumbe wa jiwe hili baada ya ufufuko ni kwa
wafu ni huu: “Mlivyo ndivyo nilivyokuwa. Nilivyo ndivyo mtakavyokuwa.”
Ni
ujumbe wa matumaini ya kufufuka. Ni ujumbe wa huruma. Ni matumaini yasiyo na
mwisho. Ijumaa Kuu ujumbe huu kwa walio hai ulikuwa, “Mlivyo ndivyo
nilivyokuwa. Nilivyo ndivyo mtakavyokuwa,” ulikuwa ni mwisho wa matumaini.
Katika
tamaduni za kiafrika mtu akiwa anaomboleza anamwambia marehemu amsalimie jamaa
zake walioaga dunia. Anasema: Nisalimie babu yangu, nisalimie nyanya yangu.
Nisalimie mjomba wangu. Nisalimie mama mdogo. Mfano wa majina: immortality of
name: mjukuu anapewa jina la babu.
Mtoto
wa kike anapewa jina la nyanya yake. Tunataka jina la mtu liendelee kutajwa.
Immortality of fame: Tunataka sifa ya mtu iishi milele. Tunajenga sanamu za
ukumbusho.
Kuna
immortality of influence: Jina la baba linawapa watoto ushawishi. Immortality
of power: Tunataka mamlaka yaendelee kwa kuanzisha mashirika ya kutoa msaada
mfano Nyerere Foundation au mfano wa aliyeanzisha zawadi ya Nobel Prize.
Jiwe lililoviringishwa na kukaliwa na malaika
linatoa ujumbe wa kupumzika. “Na
tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana
alishuka kutoka mbinguni, akaja akaliviringisha lile jiwe akalikalia” (Mathayo
28:2).
Kukaa
ni kupumzika. Kukaa kwake kunaongea kuwa kazi imemalizika. Ni siku ya Bwana. Ni
siku ya kupumzika. Lakini si kupumzika katika kutenda matendo ya huruma.
Kuhubiri ni kutenda tendo la huruma. Malaika huyu ingawa alipumzika alihubiri.
“Malaika
akajibu akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa
mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema.
Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema.
Njoni
mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi ndeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake,
Amefufuka katika wafu” (Mathayo 28: 5-7). Wanawake wanahubiriwa na kualikwa
kuamini, kushirikisha wengine na kufurahi.
Kupumzika
Jumapili hakuna maana tunapumzika katika kutenda matendo ya huruma. Ni Jumapili
hiyo elimu dini inafundishwa kwa watoto kwenye Sunday School.
Yesu anaviringisha jiwe la dhambi. Yesu ataliviringisha hilo jiwe.
“Mtu yeyote asiomboleze kuwa ameanguka tena na tena; kwa vile msamaha umefufuka
kutoka kaburini – Mt. Yohane Chrysostom . Yesu anaondoa jiwe la dhambi.
Hitimisho:
Katika maisha ya kila siku tufanye utume wa malaika wa ufufuko wa kuondoa mawe:
mawe ya shukrani ya punda, mawe ya kukata tamaa, mawe ya chuki, mawe ya
kujilinganisha na wengine, mawe ya kukufuru, mawe ya kutosamehe, mawe ya nia
mbaya, mawe ya roho ya tuharibikiwe sote, mawe ya kukatisha tamaa, mawe ya
msongo wa mawazo kutaja machache.
Comments
Post a Comment