Ask.Nkwande: Ubabe na ushabiki hautatatua kero Zanzibar
·
Asema
mazungumzo yangefaa kabla ya uchaguzi
Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda Mhashamu Renatus Nkwande |
BAADA ya Zanzibar kupata serikali mpya inayoongozwa na Rais
Mohamed Ali Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufuatia uchaguzi wa marudio wa
Machi 20 mwaka huu, na Chama kikuu cha upinzani visiwani humo CUF kusema hakimtambui Dkt Shein na
serikali yake, Askofu wa Jimbo Katoliki Bunda Mhashamu Renatus Nkwande amesema mgogoro
huo ukitatuliwa kwa ushabiki na ubabe Zanzibar haitapata suluhisho na hali hiyo
italeta italeta madhara kwa wananchi.
Akizungumza
na gazeti Kiongozi jijini Dar es Salaam, Askofu Nkwande ameeleza kuwa, kwa sasa
siasa hizo zenye mikanganyiko mbalimbali zina athari kubwa zaidi ya watu
wanavyo fikiri.
Amesema
kabla ya uchaguzi huo wa marudio kufanyika kulikuwa na haja ya kukaa pamoja kwa
ajili ya mazungumzo ambayo kwa namna ya pekee yangesaidia kuleta hali ya
utulivu visiwani humo.
“Suala
hili lilipaswa lizungumziwe na kujadiliwa ili kupata suluhisho kabla ya kufanya
uchaguzi huo kwani kwa kufanya uchaguzi wakati hakujafanyika mazungumzo yenye
kuhusisha vyama vilivyosusia uchaguzi huo ni ubabe na ushabiki usiyo na maana
utakao waathiri watu wasiyo na hatia.
Amesema
kuwa ingefaa kufanya mazungumzo kabla ya uchaguzi huo kwa ajili ya kupata mwafaka
ili wakati na baada ya uchaguzi pande zote mbili ziwe tayari zimepata
maridhiano na wote kushiriki uchaguzi huo kwa uhuru na haki.
Akizungumzia
nini kifanyike Zanzibar kwa sasa ili kuleta suluhisho amesema ni vigumu kupata
suluhisho la haraka kutokana na kila upande kuwa na msimamo mkali ambapo
pengine misimamo ya aina hiyo inaweza kuleta hali ya mtafaruku na kuhatarisha
amani.
Katika
hatua nyingine Askofu Nkwande amesema hali tete ya kisiasa viwani Zanzibar inaweza
kuathiri hata uhuru wa kuabudu baina ya waislamu na wakristo endapo serikali
haitakuwa makini.
Amesema
ili waamini waabudu katika makanisa yao na misikiti yao suala la amani ni
muhimu kuwepo na kulindwa kuwawezesha waamini hao kutimiza wajibu wao kiroho
bila ya bughudha yoyote.
Tangu kuibuka kwa mgogoro wa kisiasa Zanzibar
watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakisema mwarobaini wa mgogoro huo kwa kutumia
jitihada za ndani, ufanywe na Rais Magufuli baada ya jitihada za viongozi wa
kisiasa visiwani kukwama.
CUF
wenyewe walitaka maridhiano kabla ya kurudia uchaguzi lakini mbinu hizo
zilikwama na kuwasukuma wadau mbalimbali kumtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dakt. John Magufuli awashawishi Wazanzibar kufanya maridhiano ambapo wanasheria waliyasema haya yafuatayo;
Mwanaseria Mkuu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), George Masaju alisema Rais Magufuli hana mamlaka ya kikatiba ya kuingilia
masuala ya Zanzibar ukiwamo uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20.
Alisema;
“Katiba ya Zanzibar si ya Muungano, masuala ya ulinzi na usalama ndiyo ya
Muungano na ndiyo sababu ulinzi umeimarishwa visiwani humo kuhakikisha nchi
hiyo inakuwa salama."
Alitoa kauli hiyo wakati akifafanua mambo
mbalimbali yaliyozungumzwa na wabunge wakati wa mjadala wa mwongozo wa mpango
wa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/17 na Mapendekezo ya Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.
“Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uwepo wa Serikali mbili. Hizi
Serikali uwepo wake ni Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar. Ukisoma Ibara
ya nne ya Katiba si tu kwamba inaweka mgawanyo wa madaraka katika mihimili
mitatu ya Dola, bali inaweka mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali ya Muungano
na Serikali ya Zanzibar,” alieleza Masaju
Jaji Lubuva
Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi nchini Jaji Damiani Lubuva alieleza kuwa wanaosema Rais anapaswa
kuingilia kati masuala ya uchaguzi iwe Tanzania bara ama Zanzibar wanafanya
makosa, kwani kwa namna yoyote Rais hana mamlaka hayo na hivyo hawezi kuingilia
maamuzi ya tume hizo.
“Unaposikia kwamba Rais
wa Jamhuri ya Muungano aingilie hilo suala la uchaguzi wa Zanzibar, yeye kwa
kweli hana mamlaka kabisa. Pili ni kama kujikanganya, huku unasema tuwe na tume
huru isiyoingiliwa halafu huku unasema aingilie kati maamuzi ya tume” alisema
Jaji Lubuva.
Tangu wakati huo, Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein,
Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd na marais wa zamani wa Zanzibar, Dk
Salmin Amour, Ali Hassan Mwinyi na Amani Karume wamekuwa kwenye mazungumzo
ambayo hayakuzaa mwafaka.
Nini Kifanyike
Askofu
Nkwande amesema pamoja na kwamba uchaguzi umeishapita ipo haja kwa serikali ya
Zanzibar kukaa na vyama vilivyosusia uchaguzi huo hasa chama kikuu cha upinzani
(CUF) kwa ajili ya maridhiano yatakayoleta amani visiwani humo.
Amesema hali ilivyo si ya
kukaa kimya bali mbinu mbalimbali za maridhiano zinapaswa kufanyika na kusisitiza
kuwa viongozi wa siasa wanapaswa kuangalia maslahi yawaliowengi na suala la
amani lipewe kipaumbele cha kwanza.
“Hata kama kuna
wanaoamini serikali na wasiyoamini serikali lazima mbinu zifanyike za kuleta
suluhisho.
Kama ni maandamano ya
amani yafanyike na sauti za wanaoandamana zisikilizwe na pia wanaoandamana
wasikilize sauti za wanaoiamini na kuikubali serikali.
Amesema wanapaswa kuketi
chini wajadiliane na kufikia mwafaka kwani bila hivyo mambo yanaweza kuharibika
na kuathiri maisha ya watu kwa pande zote mbili za bara na visiwani,” amesema.
Comments
Post a Comment