Huruma ya Mungu imetufikia, kazi kwetu kuikimbilia
MWAKA
Mtakatifu wa Yubilei ya Huruma ya Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu
Fransisko huku ukiongozwa na kaulimbiu “Iweni na huruma” umezinduliwa rasmi
hapo Desemba 8, 2015 katika Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili,
kwa kufungua Lango Kuu ya Yubilei katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro lililoko
mjini Vatikani.
Baba
Mtakatifu, wakili wa Kristo, Mrithi wa Mtume Petro na Kiongozi wa Kanisa zima,
katika Waraka wake wa kichungaji, “Misericodiae Vultus”, “Uso wa huruma”
anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutangaza huruma ya
Mungu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji kutoka katika moyo na akili ya
mwanadamu, kwa kuonesha huruma na mapendo.
Manaa ya Mwaka wa
Yubilei
Kwa
maana ya jumla mwaka wa Yubilei “ni mwaka wa msamaha wa dhambi na maondoleo ya
adhabu zake, ni mwaka wa mapatano kati ya maadui, ni mwaka wa uongofu wa ndani,
ni wakati wa kupokea Sakramenti ya Upatanisho kwa uzito wa hali ya juu kabisa;
Ni
mwaka wa kuimarisha mafungamano ya kidugu na kijamii, ni mwaka wa kuyakumbatia
maisha kwa matumaini makubwa, ni mwaka wa kuzingatia haki na kukuza upendo, ni
mwaka wa kujidhatiti katika kumtumikia Mungu na jirani kwa furaha na hivyo
kujenga amani ya kudumu kati yetu na ndugu zetu wote”.
Hii
inatokana na ukweli kwamba, Kanisa daima ni mtumishi wa upendo. Yubilei ya
Huruma ya Mungu uwe ni mwaka unaowahamasisha waamini kutubu na kumwongokea
Mungu; sanjari na kuwa tayari kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili
kuchuchumia rehema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya
Mwaka Mtakatifu.
Kufungua Lango
katika Kanisa Kuu; Lango hilo linamaanisha nini?
Lango
hilo lililosheheni uzito wa fasihi, linamaanisha mpito kuelekea mwaka wa pekee
wa uinjilishaji na sala. Baba Mtakatifu Fransisko amelisukuma lango hilo ikiwa
ni ishara rasmi ya kuuzindua mwaka wa Yubilei.
Lango
hilo hufunguliwa ili kuashiria na kualika dhana ya msamaha, ambao ni lengo kuu
la Mwaka huo Mtakatifu wa Yubilei. Kadiri ya hati ya “Mondo Vaticano”, yaani
ulimwengu wa Vatikani, historia ya lango hili Kuu ina chimbuko lake tangu
zamani za mwanzo wa Ukristo ambapo wadhambi walifanya toba na wakapekwa
malipizi ya hadhara kabla ya kupewa mandoleo ya dhambi.
Watubu,
hawakuruhusiwa kuingia Kanisani kabla ya kumaliza toba yao. Baada ya
kukamilisha mambo yote, ndipo wakaruhusiwa kuingia Kanisani kwa ibada maalumu.
Ndivyo
hata nyakati zetu hizi, mahajuji wanaingia ndani ya Kanisa Kuu kupitia lango
Kuu kama ishara ya toba yao na kuiambata tena imani kwa moyo mmoja. Hivyo tendo
la kufungua malango na kuyapitia malango hayo kuna maanisha kipindi maalumu
kilichotengwa kwa ajili ya wanadamu kutakasa roho zao.
Kwa
karne nyingi, lango hilo la Jubilei Kuu halikufunguliwa kwa funguo, bali kwa
nyundo, kwa sababu malango ya haki na huruma hufunguka kwa nguvu ya sala na
toba. Lakini katika mwaka Mtakatifu wa Yubilei Kuu ya miaka 2000 tangu kuzaliwa
kwake Kristo, Mtakatifu Yohane Paulo II, hakutumia funguo wala nyundo, bali
alilisukuma lango hilo kwa nguvu na kulifungua.
Lango
hilo linabeba dhamira ya dhambi na huruma ya Mungu kadiri inavyoonekana katika
kipande cha 15 cha shaba zinazopamba lango hilo. Kuna picha pia za matukio ya agano la kale na
Jipya, pamoja na kuanguka kwa mwanadamu, picha ya kupashwa habari Bikira Maria
na picha ile ya Mwana Mpotevu na Baba mwenye huruma. Tafakari ya picha hizo
ndiyo inayotusindikiza katika hija yetu ya Mwaka huo Mtakatifu.
Lakini
kubwa na la muhimu zaidi ni kuwa sote kwa pamoja tunaalikwa kufungua milango ya
mioyo yetu na akili zetu, ili tuweze kutoa msamaha na kupokea msamaha. Malango
ya mioyo yetu na akili zetu, yatafunguka kwa nguvu ya sala na toba.
Mama
Kanisa anatumia nyundo, funguo za kila aina na nguvu takatifu ili kutusaidia
kufungua malango ya mioyo yetu. Kuna nyundo ya Maandiko Matakatifu, nyundo ya
Sakramenti za Kanisa na Visakramenti; nyundo ya Mafundisho mbalimbali ya Kanisa
na funguo za baraka na neema mbalimbali.
Funguka, upokee huruma ya Mungu
Huruma ya Mungu
hutuweka Huru
Kuishi
kwa kutumiani huruma ya Mungu hutupa nafasi ya kufungua milango ya upeo na
hutufanya tuweze kuona mbali na kuwa huru dhidi ya wasiwasi, mashaka, woga na
kutenda dhambi.
Hakuna
sababu za kuwa na hofu au woga katika kuomba msamaha kwa dhambi zetu , kwa kuwa
Mungu wetu ni Mungu Mkuu mwenye kuziona dhambi zetu na hutusamehe kila
tunapoomba kusamehewa.
Binadamu
anapaswa kutambua kwamba, Mungu ni mkuu kuliko dhambi zetu. Tunapokutana na
Kristo katika Sakramenti ya Kitubio tunapaswa kubadilika kiroho. Ni wakati wa
kuanza kuona kile tulichokosea, kuuona ukweli.
Matendo
mema na huruma kwa wengine daima huonyesha ukweli; ukweli wenye kuwa na
matumaini. Na hivyo matumaini hayo kwa Mkristo inakuwa ni fadhila , ambayo ni
zawadi kuu kutoka kwa Mungu, zawadi yenye
kuturuhusu kuona zaidi ya matatizo na
mateso hasa zaidi sana yanayotokana
dhambi zetu.
Ni
Matumaini yenye kuturuhusu sisi kuona
uzuri wa Mungu. Pia kwa wale wenye kuwa na fadhila hii ya matumaini huwa huru
na nguvu za kuona mbele zaidi ya mabaya ya
nyakati, iwe kwa ajili ya afya yao au kwa ajili ya familia yao.
Mwanzo mpya wa
maisha ya kiroho
Hiki
ni kipindi kikuu cha msamaha. Kwa kufungua Malango yote ya Yubilei sehemu
mbalimbali za dunia waamini tunaalikwa kuwa chemchemi ya furaha licha ya shida
na magumu tunayokutana nayo katika maisha kwani Mungu yuko kati yetu.
Tunaalikwa
kufanya tafakari ya kina kuhusu matendo ya huruma kiroho na kimwili, fadhila
ambazo zinaendelea kutoweka pole pole katika uso wa dunia. Waamini tunaalikwa
kwa namna ya pekee, kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kama mwanzo mpya
katika hija ya maisha yao ya kiroho, wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka
Mtakatifu wa Yubilei ya Huruma ya Mungu.
Huruma
ya Mungu ni Yesu mwenyewe, Msamaria mwema aliyejitaabisha kumganga mwanadamu
katika maisha yake ya kiroho kwa kumwondolea dhambi pamoja na kumpatia mahitaji
yake ya msingi.
Yesu
alihubiri na kushuhudia huruma ya Mungu kati ya watu wake inayopita dhambi na
mapungufu ya binadamu, mwaliko kwetu kukimbilia huruma ya Mungu katika hija ya
maisha yetu.
Mwaliko wa kuwa
mashuhuda wa huruma ya Mungu
Pia
waamini tunaalikwa kuwa vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma kwa maskini na
wote waliosahaulika katika jamii.
Huu
ni mwaliko kwetu kufanya tafakari ya kina kuhusu maana ya huruma ya Mungu,
tayari kuishuhudia imani kwa jirani zetu na ulimwengu wote.
Injili ya uhai
Pia
huu ni wakati wa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Injili ya Uhai, kwa kuthamini
maisha kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa na
kuendelezwa.
Uchu
wa mali na utajiri visiwe ni sababu ya kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.
Wafanyabiashara, wanasiasa na wadau mbali mbali wanaojikita katika biashara
chafu ya silaha wanahamasishwa kuwa mstari wa mbele kushuhudia huruma ya Mungu
katika maisha yao.
Huruma
ya Mungu iwaguse watu wa mataifa kutoka katika kila dini, kabila, lugha na
jamaa. Huruma ya Mungu ikimwilishwa katika ustadi mkubwa, inakuwa kweli ni
chachu ya ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi.
Comments
Post a Comment