Huruma ni jina na utambulisho wa Mungu
Fahamu yaliyomo
kwenye kitabu kiitwacho ‘Jina la Mungu ni huruma’
PAPA Fransisko
ameeleza kuwa Huruma ndilo jina na utambulisho wa Mwenyezi Mungu. Ameeleza hayo
katika mahojiano maalum na Andrea Tornielli, mwandishi wa habari za gazeti la
‘La Stampa’ na mhariri mkuu wa tovuti ya ‘Vatican insider’ katika kitabu
ambacho kimezinduliwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatikani
“Jina la Mungu ni huruma”.
Kitabu
hicho kimegawanyika katika sura tisa ambazo ni majibu ya maswali 40 aliyoulizwa
Papa Fransisko kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa
Yubilei ya Huruma ya Mungu.
Katika
mahojiano hayo Papa amefanya rejea katika Maandiko Matakatifu, Mafundisho ya
Mababa wa Kanisa pamoja na watangulizi wake, yaani Papa mstaafu Benedikto XVI,
Mtakatifu Yohane Paulo II, Mtakatifu Yohane XXIII na Mwenyeheri Paulo VI.
Kitabu hiki kimechapishwa katika lugha tano na nakala ya kwanza ikawasilishwa
kwa Papa Fransisko hivi karibuni.
Katika
sura ya kwanza, Baba Mtakatifu
anafafanua sababu msingi zilizomfanya kuitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu
wa Yubilei ya Huruma ya Mungu: kwanza kabisa ni sala, tafakari na mafundisho ya
viongozi wa Kanisa waliotangulia, kwa kuona kwamba Kanisa ni sawa na hospitali
iliyoko kwenye uwanja wa vita, linapaswa kuwa karibu zaidi na waamini wake ili
kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu.
Kanisa
lilikuwa linahitaji muda wa mageuzi katika maisha na utume wake, kwani watu
wengi kwa sasa wamepoteza dhana ya dhambi pamoja na kuhisi kwamba hakuna
uwezekano wa kusamahewa dhambi zao.
Sura
ya Pili, Baba Mtakatifu anazungumzia
kuhusu zawadi na umuhimu wa maungamo. Anakiri kwamba, muumini anaweza kuomba
huruma ya Mungu moja kwa moja bila kupitia kwa viongozi wa Kanisa waliopewa
dhamana na kuwaondolea watu dhambi zao.
Lakini
Mama Kanisa kwa busara yake, anataka watoto wake kuonesha moyo wa toba kwa
kumwendea Padri anayemwakilisha Kristo Yesu katika kiti cha maungamo.
Hii
ndiyo njia sahihi ya kuweza kupata huruma ya Mungu ambayo kimsingi ina mwelekeo
pia wa kijamii, tayari kuponya madonda, mipasuko na kinzani za kijamii. Waamini
wanakwenda kwenye kiti cha huruma ya Mungu si kwa kutaka kuhukumiwa, bali
kukutana na hatimaye kuambata huruma ya Mungu inayoendelea kuusimamisha
ulimwengu.
Sura
ya tatu, Papa anawaalika waamini
kujitambua kwamba wao ni wadhambi, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu ili aweze
kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani.
Hii
ni neema ambayo waamini wanapaswa kuiomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa
kutambua kwamba, huruma ya Mungu ni kubwa zaidi kuliko hata dhambi zinazotendwa
na mwanadamu na kwamba msamaha wake ni dawa makini dhidi ya dhambi.
Mwenyezi
Mungu kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma daima anawasubiri watoto wake
kukimbilia huruma, kwa njia ya toba. Kitendo cha muumini kukimbilia kiti cha
huruma ya Mungu kinaonesha toba ya ndani, sala inayopaswa kujikita katika
unyenyekevu wa moyo badala ya litania ya maneno mengi.
Sura
ya nne, Baba Mtakatifu anasema kuwa
hata Khalifa wa Mtakatifu Petro anahitaji kuonja huruma ya Mungu katika maisha
yake, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro pale alipotambua mapungufu yake
akaangua kilio.
Ameeleza
kuwa muungamishaji asiwe ni mtu mwenye kiburi, bali aoneshe unyenyekevu na
ukweli wa maisha kwa kutambua kwamba hata yeye pia ni mdhambi anahitaji huruma
ya Mungu.
Sura
ya tano, Baba Mtakatifu Fransisko
anasema kuwa Kanisa linalaani dhambi, lakini linamkumbatia mdhambi anayetambua
dhambi zake, tayari kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.
Kanisa
halina budi kusamehe bila kuchoka kama anavyofundisha Yesu mwenyewe kwa wafuasi
wake. Mwenyezi Mungu yuko radhi kumpokea muumini anayeonesha moyo wa toba na
wongofu wa ndani, tayari kukumbatia huruma ya Mungu. Kanisa lipo ili kuwawezesha
waamini kukutana na huruma ya Mungu katika maisha yao.
Sura
ya sita, Papa anawaonya waamini
wanaodhani kwamba wanaweza kujiondolea wenyewe dhambi zao kwani tabia kama hii
inamchukiza Mwenyezi Mungu na kwamba, ni “ugonjwa wa kiroho” unaopaswa kupewa
tiba muafaka.
Waamini
waoneshe nia ya kutaka kutubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao, hapa
watapata tiba kamili bila kujiaminisha kwamba wanajiweza kwa kila jambo.
Binadamu
ni mavumbi mbele ya Mungu, kumbe anapaswa kujinyenyekesha, kutubu na kuomba
msamaha na huruma ya Mungu.
Onyo
hili, anasema Papa, si tu kwa waamini walei hata kwa Wakleri na Watawa ambao
wanadhani kwamba kutokana na maisha na utume wao hawana sababu ya kukimbilia
huruma ya Mungu.
Kwa
waamini hata wale ambao jamii inawaona kuwa wamekengeuka kiasi hata cha
kupoteza dira na mwelekeo wa maisha kama wale wanaoshabikia ushoga na mifumo ya
utamaduni wa kifo, wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma kama Katekisimu
Mpya ya Kanisa Katoliki inavyofundisha.
Huruma
ya Mungu si dhana ya kufikirika inayoelea kwenye ombwe, anasema Papa, bali ni
sifa kuu ya Mungu na mafundisho ya Kanisa. Yesu alikuja ulimwenguni ili
kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti kwa kumjalia maisha ya uzima
wa milele.
Ni
mganga wa kweli anayewatafuta wagonjwa na wala si wenye haki ambao hawahitaji
kutubu na kumwongokea Mungu.
Katika
Sura ya Saba, Baba Mtakatifu anasema
kuwa mdhambi anaweza kuvumiliwa lakini fisadi na mla rushwa, hawa ni watu
hatari kwani wanatenda dhambi lakini si wepesi kuungama dhambi zao tayari
kujipatanisha na Mungu.
Mafisadi
na wala rushwa ni watu wanaowatesa na kudhalilisha wananchi wengine; ni
wanafiki. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu Huruma ya Mungu, Papa Fransisko
anawaalika mafisadi na wala rushwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza
ukurasa mpya wa maisha yao. Wamwombe Mungu neema ya kuona aibu kwa dhambi
walizotenda.
Katika sura
ya nane, Baba Mtakatifu anawakumbusha walimwengu kwamba
Mwenyezi Mungu anawapenda upeo na anataka kuwaonjesha huruma yake isiyokuwa na
mipaka. Mwenyezi Mungu kwanza kabisa anaonesha uso wa binadamu na pili uso wa
Kimungu.
Yesu
anamwangalia mwanadamu kutoka katika undani wa maisha yake na wala si kama
mpiga picha anayeangalia mambo ya nje.
Sura
ya tisa ambayo ni hitimisho la
maswali 40 ambayo Papa Fransisko amejitahidi kuyajibu kwa ufasaha, inajikita
katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; mambo msingi yanayomwezesha
muumini kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake.
Comments
Post a Comment