Historia ya Huruma ya Mungu kwa jicho la Mababa Watakatifu
IBADA ya Huruma ya Mungu imepata msukumo na kuhamasishwa katika Kanisa
Katoliki katika Karne ya 20 kutokana na ufunuo binafsi aliopewa sista Maria
Faustina Kowalska mwaka 1935.
Lakini pia ndani ya Kanisa, Ibada ya Huruma ya Mungu ina
historia pana yenye kukita mizizi na kuimarika miongoni mwa Kanisa na waamini.
Mwito kwa Ibada ya Huruma ya Mungu imepata kutolewa na
kusisitizwa kwa nyakati tofauti ndani ya Kanisa kupitia mababa watakatifu
watatu ambao ni; Papa Yohane XXIII, Papa Yohane Paulo II na Papa Fransisko
(Baba Mtakatifu wa sasa). Mababa hawa wametoa mchango mkubwa katika ibada hii
ya Huruma ya Mungu kila mmoja kadiri ya nafasi na nyakati yake.
Mchango wa Papa Yohane XXIII
Moja ya mambo ambayo Kanisa linamkumbuka baba huyu ni
Mtaguso wa pili wa Vatikano. Katika hotuba yake ya ufunguzi mnamo Oktoba 11,
1962, Papa Yohane XXIII alitoa muongozo wa Mtaguso kuwa ni ufunguo wa huruma na
mtazamo mpya wa maisha ya kikristu (aggiornamento).
Akifafanua lengo la kuitisha Mtaguso wa Pili wa
Vatikano, Papa Yohane XXIII alisema; “Lengo la Mtaguso ni kutoa muongozo na
kufundisha kwa ufasaha ‘hazina azizi za mafundisho ya Kikristu’ (sacred deposit
of the Christian doctrine)...”
Aliongeza kwa kusema; “Hapo zamani, Kanisa lililaani
vikali (condemned with utmost severity) makosa na uzushi wa kimafundisho katika
vipindi mbalimbali...Lakini leo, Kanisa halina budi kuelekeza kwa upole na
huruma badala ya kulaani (the church must prefer ‘the balm of mercy to the arm
of severity) katika kuelezea kwa kina undani wa mafundisho yake badala ya
kulaani wanaoyapotosha...”
Bila shaka ndio maana wakati fulani Papa Yohane XXIII
alifahamika kama “Mwalimu wa Huruma na Ukweli” kwani alifahamu fika kuwa yote
mawili yanahitajika.
Paenetentiam Agere (Msamaha wa dhambi):
Mnamo Julai Mosi, 1962, Baba Mtakatifu Yohane XXIII
alitoa barua ya kichungaji iitwayo “Paenitentiam Agere” ama Msamaha wa dhambi
ikiwa ni barua yake ya saba ya kichungaji.
Barua hii iliyofafanua juu ya zawadi ya huruma ya Mungu
na umuhimu wa kila mmoja wetu kutambua hitaji la zawadi hiyo katika maisha yake
na hivyo kuja kuipokea katika sakramenti ya upatanisho na kufanya kwa dhati
kitubio cha ndani (rohoni) na nje.
Baba Mtakatifu Yohane XXIII aliipendekeza njia hii bora
kabisa kama namna muafaka ya maandalizi ya Mtaguso Mkuu wa Pili kusudi “mbegu
bora ya Mtaguso iweze kuenea/kutawanyika mbali zaidi katika kila pande/pembe ya
Kanisa na wala isipotee bure bali ikute ‘mioyo iliyo tayari na iliyoandaliwa,
iliyo amini na kweli.”
Papa Yohane XXIII aliamini kuwa, Mtaguso ungezaa matunda
mengi na yenye kudumu iwapo tu ‘udongo utakuwa umetiwa rutuba ya huruma ya
Mungu’ (only if the soil of receptivity had been fertilised with God’s mercy).
Ndio maana pengine baadhi ya watu hufikiri kuwa baadhi
ya maazimio ya Mtaguso wa pili wa Vatikano hayafanyiwi kazi au kuzingatiwa
ipasavyo kama ilivyotegemewa kutokana na kutozingatiwa kwa wito wa Yohane XXIII
juu ya uongofu, upatanisho/kitubio na huruma ya Mungu.
Mchango wa Papa Yohane Paulo II
Baba Mtakatifu Yohane Paulo II naye ana mchango mkubwa
sana katika Ibada ya Huruma ya Mungu ndani ya Kanisa Katoliki.
Kati ya majukumu makubwa aliyokuwa nayo ni kutekeleza
kwa ufasaha na ufanisi maazimio ya Mtaguso wa pili wa Vatikano ambao yeye
mwenyewe alishiriki kama askofu. Bila shaka kama Papa alikusudia kueneza ‘balm
of mercy’ aliyokusudia Yohane XXIII katika ulimwengu wa sasa.
Wakati wa uongozi wa Papa Yohane XXIII, Shajara ya Sista
Maria Faustina ilikuwa kati ya orodha ya vitabu vilivyolaaniwa kutokana na
tafsiri ya kiitaliano iliyokosewa ambayo ilionesha kana kwamba msamaha wa
dhambi unaweza kuwepo kupitia mazoezi ya kiroho peke yake pasipo sakramenti ya
Kitubio (Huruma ya Mungu).
Lakini Yohane Paulo II alipokuwa Askofu Mkuu wa Kraków
alimuagiza Padri Ignacy Rozycki ayachunguze kwa ufasaha na umakini mkubwa
maandishi ya Sr Maria Faustina ili athibitishe kama yanaendana na Teolojia na
mafundisho ya Kanisa.
Alipochaguliwa kuwa Baba Mtakatifu, aliufanya uongozi
wake kuwa katika mtazamo wa huruma ya Mungu. Mnamo mwaka 1981 alisema; “Tangu
mwanzo wa utume wangu katika kiti cha Mtume Petro - Roma, ninaufikiria ujumbe
wa huruma ya Mungu kuwa kazi yangu/jukumu langu kubwa...”
Papa Yohane II mnamo mwaka 1997 aliongezea kusema;
“Ujumbe wa huruma ya Mungu umekuwa daima karibu nami na mahususi kwangu...
Umekuwa pia uzoefu wangu binafsi, ambao nimeambatana nao katika kiti cha Mtume
Petro, na ambao kwa namna fulani umekuwa/ umefanya muundo wa upapa wangu.”
Agosti 1992, Yohane Paulo II, aliukabidhi ulimwengu kwa
huruma ya Mungu, ili ujumbe wa upendo wenye huruma ufahamike na kujulikana kwa
watu wote wa dunia.
Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alisisitiza sana kwamba;
“ Hakuna kitu ambacho mtu awaye yote uhitaji zaidi kuliko huruma ya Mungu...”
Kwa kupitia barua yake ya kichungaji aliyoipa jina;
“Mungu Mwingi wa Huruma” (God is Rich in Mercy) alitoa mwito hasa kwa Kanisa
kutolea ushuhuda wa Huruma ya Mungu.
Kwa kupitia andiko lake hilo alisisitiza;”…Kanisa halina
budi kutolea ushuhuda huruma ya Mungu inayodhihirika katika
Kristu...ikijitambulisha na kukaa katika maisha ya waamini na watu wote wenye
mapenzi mema...na kuwaalika wote kuja kuitafuta huruma ya Mungu katika maovu
yote na mabaya yote...”
Mnamo mwaka 1993 Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II
alimtangaza Sista Maria Faustina kuwa Mwenyeheri na miaka saba (7) baadae
(2000), akamtangaza kuwa Mtakatifu.
Sambamba na kumtangaza huko Sista Maria Faustina kuwa
Mtakatifu, alitangaza rasmi pia kuwa Jumapili ya pili ya Pasaka kuwa Jumapili
ya huruma ya Mungu.
Jambo la kipekee la kustaajabisha na kutafakarisha
ambayo tunaweza kuhusianisha maisha binafsi ya kujitoa na kuipa kipaumbele
ibada ya huruma ya Mungu aliyoishi sambamba na kuitangaza Injili ya Upendo
wenye Huruma ya Mungu Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II ni matukio ya mwisho
katika uhai wake kwani Mungu mwenyewe ilimpendeza kumuita kwake usiku wa mkesha
wa sherehe ya Huruma ya Mungu mnamo mwaka 2005.
Lakini pia, cha kustaajabisha zaidi na kutafakarisha ni
kwamba Baba Yohane Paulo II alitangazwa kuwa Mwenyeheri siku ya Jumapili ya
Huruma ya Mungu ya mwaka 2011.
Pia alitangazwa kuwa Mtakatifu Yohane Paulo II siku ya
Jumapili ya Huruma ya Mungu ya mwaka 2015.
Mchango wa Papa Fransisko
Ujumbe wa huruma ya Mungu umeendelezwa sasa na Baba
Mtakatifu Fransisko. Alipoulizwa, mara tu baada ya kuchaguliwa na Makardinali,
kama anakubali kuwa Baba Mtakatifu, alionesha imani yake binafsi katika huruma
ya Mungu alipojibu; “Mimi ni mdhambi. Lakini nina imani katika huruma ya Mungu
na uvumilivu usio na kikomo/mipaka wa Bwana wetu Yesu Kristu...nakubali.”
Huruma imekuwa sehemu msingi ya historia ya wito wake,
akiupokea utume wa upadri kama wito wa ajabu wa huruma ya Mungu.
Kauli mbiu (Motto) yake ikiwa ni; “Miserando Atque
Eligendo” (‘by having mercy, by choosing him’) yaani, “kwa huruma kwa kumchagua
yeye”. Kauli mbiu yake hiyo inaonesha msisitizo kuwa katika maisha yake yote,
na hata katika maisha ya mtu yeyote yule, Mungu hutuita katika huruma na kutukumbatia
kwa huruma na upendo.
Papa Fransisko alimsifu Yohane Paulo II kwa kutambua kwa
njia ya msaada wa Sr. Maria Faustina kuwa nyakati zetu za ulimwengu wa sasa ni
“Kairos” au wakati muafaka wa huruma ya Mungu.
Papa Fransisko alisema kuwa, “Injili nzima, ukristu
wote” (whole Gospel, all of Christianity) inajumuishwa katika furaha aliyo nayo
Mungu katika kutusamehe sisi...na kuwa huruma ya Mungu ndiyo msukumo wa kweli
ambao humuokoa mtu na kuukomboa ulimwengu.
Na kwa namna ya kipekee, Baba Mtakatifu Fransisko
alitangaza mnamo Desemba 8, 2015 kuanza kwa Yubilei ya kipekee ya Huruma ya
Mungu ambayo inadumu mpaka Novemba 20, 2016 huku akualika Kanisa lote
kujinyenyekeza, kuendesha ibada, kuomba msamaha na kutafuta huruma ya Mungu.
“Heri walio na huruma maana watahurumiwa” (Mathayo 5:7).
Nimeelimika
ReplyDelete