MSHUMAA WA PASAKA ISHARA MUHIMU YA KRISTO MFUFUKA

PASAKA ni sherehe kubwa sana ambayo  tunaiadhimisha   kwa muda wa siku hamsini katika Liturujia ya Kanisa. Tunakiri na kuadhimisha imani kwamba Yesu Kristo aliyeteswa, akafa msalabani, akazikwa; amefufuka na sasa yuko nasi. Katika kuadhimisha imani hiyo Liturujia inatumia ishara ya Mshumaa wa Pasaka.
Utengenezwe kwa nta
Mshumaa wa Pasaka unapaswa kutengenezwa kutokana  na nta ya nyuki. Mbiu ya Pasaka inapousifia  inatamka wazi kwamba Mshumaa huo unapoendelea kuwaka  ni tendo la sadaka ambayo Kanisa linamtolea Mwenyezi Mungu na kwamba umetengenezwa kwa nta ya nyuki. Maneno halisi ya sala ya Mbiu yanasema hivi: “Kanisa takatifu linakupa sadaka hii kwa mikono ya watumishi wake linapokutolea mshumaa huu wa nta ya nyuki”.  
Mbiu inaendelea kutoa sifa ya Mshumaa  wa Pasaka ikieleza kwamba ingawa kutokana na Mshumaa huo imewashwa mishumaa mingi, nguvu yake haikupungua. Sala inasema hivi: “Ingawa moto huu umegawanyika, haukupunguka kwa kuwasha mioto mingine. Kwa maana walishwa na nta inayoyeyuka, iliyotengenezwa na mama nyuki ikapata kuwa taa hii iliyo bora”.
 Basi  maneno haya ya Mbiu ya Pasaka yanashuhudia kuwa Mshumaa huo usiwe mshumaa bandia bali unapaswa kutengenezwa kutokana na nta halisi.
Ukubwa wa Mshumaa
Ukubwa wa Mshumaa umekuwa ukitofautiana kwa nyakati mbalimbali na pia kadiri ya utamaduni wa nchi. Kwa mfano huko Uingereza wakati wa karne za kati ukubwa wa mshumaa huo ulifikia uzito wa kilo kupita 700. Katika kanisa jingine Mshumaa ulikuwa mrefu hadi wa futi 36, yaani yapata mita 11.
Jambo muhimu ni kwamba Mshumaa uwe mkubwa, wenye hadhi na kupambwa vizuri uweze kutumika katika Maadhimisho yote ya Liturujia siku hamsini za kuadhimisha Ufufuko wa Bwana.
Kutokana na aina ya nta inayotumika  na utulivu wa altareni unapowekwa, pengine Mshumaa wa Pasaka huisha haraka. Wanaotengeneza wafahamu kwamba Mshumaa huo unatakiwa kuwashwa katika Maadhimisho yote muhimu  wakati wa Pasaka.
Ishara ya Kristo Mfufuka
Kuelewa vizuri umuhimu wa ishara hii ya Mshumaa wa Pasaka yatupasa kurudi nyuma kuangalia Liturujia ya Alhamisi Kuu jioni. Baada ya kuadhimisha Misa Kuu ya Karamu ya Bwana, mara baada ya Sala baada ya Komunyo, bila hata kutoa Baraka, kuhani anaandaa kuihamisha Ekaristi kuipeleka mahali ambapo waamini wataabudu.
Baada ya kusali mbele ya Ekaristi kwa kitambo anarejea mbele ya Altare; yeye mwenyewe au wahudumu huanza kuizima mishumaa yote na kuiondoa Altareni, kisha huondoa nguo zote za altareni na kuiacha  tupu kabisa. Tendo hilo ni ishara ya uchungu kwani Bwana Yesu   anaingia katika mateso yake.
Kuanzia hapo hatuwashi tena mwanga altareni, na Liturujia ya Ijumaa Takatifu huanza pasipo kutandika nguo altareni wala mishumaa mpaka tunapoanza kuadhimisha Mkesha wa Pasaka. Tendo la kwanza ni kubariki moto mpya nje ya kanisa na wakati huo lazima taa zote ziwe zimezimwa kanisani.
Iwapo waamini wazee wanabaki ndani ya kanisa  wakati wa kubariki moto mpya,   wabaki wakisali kimya katika giza. Tendo la pili ni kuubariki Mshumaa wa Pasaka.
Baraka hiyo hufanyika pia kwa ishara na maneno anayoyatamka kuhani kwa sauti ili waamini  wasikie. Baada ya Baraka ya Mshumaa, kuhani huwasha Mshumaa akisali sala ifuatayo: Mwanga wa Kristo aliyefufuka kwa utukufu, utuondolee giza moyoni na rohoni.”
Basi kwa sala hii tunaona kwamba Mshumaa huo ni ishara ya Kristo Mfufuka ambaye ni nuru ya ulimwengu. Kwa ufufuko wake anakamilisha Ukombozi wetu na anatuondolea giza moyoni na rohoni. Neno giza ni ishara ya dhambi na nuru au mwanga ishara ya neema. Kristo akituangazia nuru yake mioyoni na rohoni mwetu tunaondolewa dhambi, tutakuwa na neema ndani yetu.  
Unatangulia maandamno
Kwa kuwa Mshumaa ni ishara ya Kristo Mfufuka anayeondoa giza, Liturujia inaweka wazi kwamba shemasi au  kama hayupo, padri mwenyewe anaushika Mshumaa wa Pasaka na kuanza kuongoza maandamano akitanguliwa na mhudumu anayeshika cheteso.
Shemasi anapoanza maandamano anauinua Mshumaa juu, huwageukia na kuwatangazia waamini: Mwanga wa Kristo, nao huitikia: Tumshukuru Mungu. Tangazo hilo analitoa mara tatu mpaka kufika altareni.
Tendo hilo lina maana kubwa kwamba Kristo Mfufuka anatutangulia njia; anaondoa  giza kwa ishara ya Mshumaa wa Pasaka. Waamini wote kwa zamu huwasha mishumaa yao kutokana na Mshumaa huo wa Pasaka.
Tendo hilo nalo ni ishara kubwa hasa tukikumbuka sala ya kuhani wakati alipowasha Mshumaa huo nje aliposema: Mwanga wa  Kristo aliyefufuka kwa utukufu utuondolee giza moyoni na rohoni.
Tunapowasha mishumaa yetu kutoka Mshumaa wa Pasaka ni ishara kwamba Kristo atushirikishe mwanga wake na kumwomba  atuondolee giza mioyoni na rohoni mwetu; yaani  atutakase kabisa dhambi baada ya mfungo na toba tuliyoifanya kipindi  cha Kwaresima. Tazama jinsi Liturujia inavyosema nasi katika utajiri kwa njia ya ishara.
Mbiu ya Pasaka
Baada ya shemasi kutangaza mara ya tatu Mwanga wa Kristo na wote kuwasha mishumaa yao kutoka Mshumaa wa Pasaka taa zote kanisani huwashwa. Baada ya kuingia waamini wote kanisani, shemasi huuweka Mshumaa kwenye stendi yake iliyopambwa vizuri kwa heshima ya Kristo Mfufuka.
Maandalizi yakiwa tayari, shemasi hufukiza kitabu cha Mbiu na baadaye hufukiza Mshumaa wa Pasaka, hurejea kwenye Mbiu na kuanza kupiga au kutangaza Mbiu kwa kuimba. Mbiu inasifia Mshumaa huo na  usiku mtakatifu ambao Kristo alifufuka. Tendo la kufufuka Kristo liliutakatifuza usiku huo.
Mshumaa uheshimiwe
Mshumaa huo unaingizwa  katika kisima cha Ubatizo wakati maji yanapobarikiwa na kusali: “Ee Bwana tunakuomba nguvu ya Roho Mtakatifu ishuke ndani ya maji yote ya kisima hiki kwa njia ya Mwanao...”.
Sala hii inaendana na ishara ya kuuweka Mshumaa ndani ya maji ili watakaobatizwa wafufuke na Kristo, yaani waishi maisha mema. Tena, Mshumaa huo unaongoza maandamano ya wateule wanaobatizwa kwenda mahali watakapobatizwa.
Katika kipindi chote cha Pasaka Mshumaa huo uheshimiwe kama ishara ya Kristo Mfufuka. Uwashwe wakati wa Masifu ya Asubuhi, Misa na pia Masifu ya Jioni.  Baada ya Pentekoste Mshumaa unawekwa kwenye kisima cha Ubatizo utumike wakati wa kuadhimisha Sakramenti ya Ubatizo. Mkristo mpya hupewa Mshumaa huo aushike mkononi; tendo hilo ni ishara ya kuanza maisha mapya na Kristo Mfufuka.

Katika misa za mazishi Mshumaa wa Pasaka  huwekwa karibu na jeneza kama ishara ya Mkristo aliyeanza maisha    yake katika  Ubatizo alipopewa mwanga huo wa Kristo. Mkristo anapofariki Mshumaa unakuwa ishara ya kumwomba Kristo ampeleke mfuasi wake mbinguni. “Leo hii utakuwa pamoja nami peponi”(Lk23:43).

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI