Fahamu undani wa Ensikliko ya Papa Fransisko juu ya Mazingira
Swali:
Hivi karibuni Baba Mtakatifu Fransisko ametoa ensikliko yake kuhusu mazingira
na kuiita ‘Laudato Si’ unaweza kutuambia maana yake ni nini?
NI
ada ya nyaraka zote za kimawasiliano kutoka Vatikani kujulikana kwa jina
linalotokana na sentensi (au kishazi) ya kwanza katika waraka ule. Katika
ensikliko hii maneno hayo ni ‘Laudato Si’ yaani ‘ sifa kwako ee Bwana’.
Maneno
haya yametoka katika ‘mashairi ya Mtakatifu Fransisko’ juu ya mazingira. Lakini
waraka wenyewe, kama zilivyo nyingine zote, unajulikana kwa kichwa cha habari
chenye dhima zinayowasilishwa humo: Juu ya uangalizi wa nyumbani mwetu.
Swali:
Je ni mambo yapi ambayo yameongelewa ndani ya ensikliko hii?
Kabla
mtu hajasoma waraka huu anapaswa ajue aina ya uandishi uliotumika. Baba
Mtakatifu anaandika kwa kufuata mtindo wa ‘tafakari tunduizi’: ona, amua na
tenda. Hii inaonekana kadri sura zinavyojitokeza, kuanzia sura ya kwanza hadi
ya mwisho.
Kwa
kufuatia dhima zake kazi hii imegawanyika katika makundi makubwa sita. Dhima
hizi tumeziongelea tayari hapo juu. Uzuri ni kwamba kila sura ya waraka huu
inaongelea kwa kina dhima tofauti.
Swali:
Hebu kwa ufupi kabisa tukumbushie dhima kuu za ensikliko hii
Dhima
kadhaa zimeelezwa kwa mapana kabisa na kwa uwazi wa hali ya juu kiasi kwamba
kusifiwa kwa kuweza kuyasema yale ambayo wenye maslahi mbalimbali walichelea
kuyasema. Dhima hizo ni pamoja na uhusiano kati ya maskini na umaskini pamoja
na unyeti (fragility) wa sayari yetu hii.
Hivi
karibuni, kwa mfano Benki ya Dunia imetoa ripoti yake kuhusu athari za
mabadiliko ya hali ya hewa na upatikanaji wa chakula. Kulingana na ripoti yao,
kwa hakika chakula kimepungua sana na hivyo njaa itaongezeka na umaskini kama
yalivyo magonjwa vitaongezeka vile vile.
Dhima
nyingine ni pamoja na uelewa kuwa vitu vyote vilivyomo duniani kwa asili
vinahusiana, ni mahusiano. Pia upo ukosoaji wa mitazamo kadhaa mipya juu ya
kimazingira na pia nguvu na uwezo utokanao na teknolojia.
Ipo
pia haja ya kutafuta njia mpya na mbadala za kuuelewa uchumi na maendeleo,
thamani halisi ya/kwa kila kiumbe, maana
ya kiutu ya ekolojia, haja ya kuwepo kwa mazungumzo na mijadala ya wazi na
kweli juu ya hali hii, wajibu madhubuti
wa sera za kimataifa na kitaifa juu ya hilo.
Inamalizia na dhima ihusuyo utamaduni hasi uliojitokeza wa utumiaji na
utupaji vitu na mapendekezo ya maisha mapya.
Swali:
Ni mahusiano yapi hayo yanayoongelewa humu?
Ama
kwa hakika mahusiano ndio msingi mkuu kabisa wa maelezo yanayotolewa humu ndani
ya ensikliko hii: mahusiano kati ya binadamu, viumbe wengine na sayari yetu
hii. Dunia inarejelewa mara zote kama nyumbani mwetu, kama mama yetu na kwa
upande mwingine kama dada yetu.
Kwa
bahati mbaya uhusiano huu unaelekea kuendelea kuharibika kadri tunavyoyaharibu
mazingira yetu. Mara nyingi tunasahau kuwa sisi tumepewa uwakili tu wa kutunza
dunia na mazingira yake kwa ajili yetu na kizazi kijacho. Hii yote
inatukumbusha juu ya mahusiano yetu sisi na mazingira yetu.
Swali:
Kulikoni masuala ya mazingira, mbona tungetaraji abakie katika masuala
yanayohusu mafundisho na maadili kama
tulivyozoea?
Kwa
kutumia maneno ya Mtakatifu Agustino (Askofu) wa Hippo (maeneo ya Libya ya
sasa) viongozi wa kidini ni raia kama walivyo raia wengine wote lakini kwa
ajili ya raia hao wanateuliwa kuwa viongozi wao.
Hivyo
basi sio sahihi kumzuia kiongozi huyo asiongelee masuala ambayo yanawagusa
waumini wake na hata yeye mwenyewe. Mwelekeo huu hasi unazidi kujengeka
miongoni mwa wanasiasa wetu ama kwa kutojua au kwa makusudi kabisa, ili
wasiwajibishwe na umma.
Katika
mchakato wa kuandaa ensikliko hii baadhi ya wanasiasa hasa wa kimarekani, kama
ilivyo ada yao kupinga kusikia chochote kutoka kwa viongozi wa kidini sembuse
masuala ya kisayansi, walitahadharisha juu ya kanisa kuongelea juu ya suala
hili kwa kuwa tu eti ni la kisayansi.
Kwa
kuwa huu ndio mwelekeo wao hawakutaka kutambua kuwa, kwanza mwandishi wa
ensikliko hii, Papa Fransisko pia ni mwanasayansi. Anayo shahada ya uzamivu ya
stadi za kemia. Wengine waliwatania kuwa kwa hili walau wao ndio wanaopaswa
kumsikiliza yeye kama wanavyodhanika kufanya kwa wanasayansi wengine.
Pili,
mara zote uandiki wa enskliko kama ilivyo hii uhusisha pia mashauriano mengi,
marefu na ya kina yanayohusisha kada mbalimbali za kitaaluma na kijamii.
Ensikliko hii ilijumuisha michango ya wanasayansi, wanafalsafa, wanateolojia,
na hata makundi ya kijamii. Bahati mbaya wagomvi wa wanasiasa hao mara nyingi
huwa wanateolojia na imani zao.
Mababa
watakatifu wengine pia wamegusia hayo; hivyo kama ni ‘lawama’ au pongezi kuhusu
mafundisho ya aina hiyo hata wao wanastahili. Mtakatifu Yohana Paulo wa Pili
anasisitiza kuwa ni wajibu wetu katika uumbaji na majukumu yetu kwa viumbe,
asili na muumba ni sehemu ya muhimu kwetu kama wakristo na imani yetu.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa 16 naye pia kazi zake zimehusishwa kwa kurejelewa. Labda
kwa taarifa tu, ijulikane pia kuwa wapo watu wengine mbalimbali waliorejelewa
katika kazi hii. Hawa ni pamoja na watakatifu Fransisko, Bonaventura, na Tomasi
wa Akwino. Wamo pia wanafalsafa kama vile Pd. Teilhard de Chardin na Romano Guardini.
Jambo
la kutia moyo ni kwamba baadhi ya watu na vyombo vya habari vilikiri kuwa walau
kwa mara ya kwanza suala hili limesemewa kwa uwazi na hakika kabisa. Mara zote
mijadala inayohusu masuala haya hugubikwa na unafiki, maslahi binafsi na
yanayogongana hivi kwamba mpaka sasa hakuna anayetaka ukweli hasa ujulikane.
Swali:
Katika andiko hili kila tunapoambiwa kuhusu ‘kuona’ kabla hatujaamua na
kutenda, ni nini hasa tunatarajia ‘tukione’ humu ndani?
Sura
ya kwanza inaanza kwa kutuonesha hali halisi; inafanya hivyo kwa kutueleza ni
nini kinatokea ‘nyumbani mwetu’ duniani. Sura hii inaorodhesha mambo kadhaa
ikiwa ni pamoja na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, uchafu,
takataka na utamaduni-potezi (matumizi pindukia na yasiyo ya lazima);
hali
ya hewa kama mali ya wote, masuala ya maji na ukosefu wake, upoteaji wa
bayoanuai, kuporomoka kwa ubora wa maisha ya mwanadamu na kuparaganyika kwa
misingi ya jamii, kutokuwepo kwa usawa, hatua dhaifu dhidi ya haya yote na
kuwepo kwa mitazamo kinzani tofauti juu ya nini cha kufanya kukabiliana na hali
hiyo.
Ni
katika sura hii ndimo tunaoneshwa athari kubwa za kuegemea zaidi kwenye
‘uchumi-ukaa’ katika dunia na maisha ya mwanadamu; pamoja na mambo mengine aina
hii ya uchumi na michakato inayoendana inachangia katika kuongezeka kwa joto la
tufe (dunia) letu hili, magonjwa na kadhia nyingine nyingi tu.
Aidha
athari za kijamii na kimazingira zinazotokana na uchimbaji wa madini
zinazungumziwa pia. Katika sura hii Baba Mtakatifu pia anasifia juhudi zinazofanywa
na asasi mbalimbali zinazojihusisha na mazingira lakini pia anakosoa baadhi ya
mitazamo iliyomo humo kama vile mtazamo hasi juu ya ongezeko la idadi ya watu.
Shida
ya hoja hii ni kwamba husababisha watu kutokukubaliana na haja ya kupunguza
‘ulaji-pindukia’ kwa kuwa tu inadhaniwa kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu ndio
chanzo cha mapungufu yote hayo. La
hasha!
Swali:
Je katika maelezo yote haya nini nafasi ya neno la Mungu?
Kwa
kuwa masuala yahusuyo hali ya hewa na mazingira yanahusisha uumbaji, basi hata
neno la Mungu ndani ya ensikliko hii litahusianisha uumbaji. Katika ensikliko
hii, kama zilivyo nyingine zote, usingetegemea kukosa sehemu inayohusianisha
Habari Njema (neno la Mungu) na masuala yanayozungumziwa humo ndani; hii ndio
injili yake yaani injili ya uumbaji.
Sura
ya pili imejikita katika kutufikishia Injili ya uumbaji. Humu tunapatiwa mwanga
kama unavyotolewa na imani, tunapata busara za simulizi za kibiblia,
tunaoneshwa fumbo la ulimwengu, ujumbe kwa kila kiumbe ndani ya utangamano wa uumbaji,
ushirika wa wote na hatma ya jumla ya vitu vyote.
Hapana
shaka Biblia haitoi ruhusa ya mitazamo potofu ya kibinadamu juu ya viumbe
wengine. Mitazamo hii potofu inapelekea hata kusafirisha nyara na wanyama walio
hatarini kutoweka; hata kuruhusu biashara ya binadamu vile vile.
Swali:
Je waweza kuongelea juu ya nafasi ya teknolojia katika kadhia yote hii?
Sura
ya tatu kama zilivyo zile zilizoitangulia inajikita katika kuelezea hali halisi
na hapa inajikita katika kuelezea nafasi ya teknolojia katika madhila yote
haya. Pamoja na kuelezea ubunifu na uzalishaji, pia sura inazungumzia juu ya
utandawazi wa mtazamo wa mfumo-kiteknolojia.
Pia
inatanabaisha madhara na mkanganyiko wa mitazamo ya kisasa juu ya nafasi ya
binadamu katika mambo yote haya. Inaelezea pia shida ya mitazamo inayotegemea
msimamo wa mtu binafsi. Katika yote haya zinajadiliwa hoja za kuhakikisha ajira
zinapatikana na kulindwa na mwisho zinaainishwa teknolojia mbali mbali za
kibaiolojia.
Sura
hii inatazama mizizi ya ‘shida’ hizi kutoka katika dhana pacha zinazovuma na
kutawala sasa: kwamba teknolojia inaendesha kila kitu (technocratic paradigm)
na pia kuwa mwanadamu ndiye kila kitu (anthropocentrism). Dhana hizi
zimesababisha wengi kuona kuwa asili ipo tu kwa ajili ya kutumika na kwamba
haina thamani yoyote kitasaufi (kiroho);
maana
yake ndio kusema kimakosa kuwa raslimali za dunia na maendeleo ya kiuchumi na
kiteknolojia pekee yanaweza kutokomeza njaa na umaskini duniani. Hapana shaka mtazamo huu potofu umepelekea
kutojaliwa mazingira, kutothamini uhai wa mwanadamu na hasa kwa wale walio na
thamani ‘ndogo’ au wasio na ‘faida’ kama vile mimba, masikini na hata walemavu
pia.
Tabia
hii ya ‘ulaji’ na itikadi za kiuchumi zinazosukumwa na haja ya kutengeneza
faida zimepelekea kwenye tamaa ya kushinda na kutawala inayosababisha
kuendekeza tabia na mwelekeo wa ‘kutupilia mbali’ asili na ubinadamu. Labda tabia ovu ya matumizi ya madawa ya
kuongeza nguvu kwa wanariadha hivi karibuni yaweza kuwa ni moja ya utamaduni
huo mpya.
Swali:
Je sura ya nne inapozungumzia juu ya ekolojia-jumuishi inamaanisha kitu gani
hasa?
Katika
sura hii Baba Mtakatifu anaongelea juu ya ekolojia-jumuishi. Hapa anaziongelea
ekolojia za kimazingira, kiuchumi na hata kijamii kabla ya kugusia utamaduni wa
kiekolojia na ekolojia ya kila siku.
Japo
kubwa la msingi hapa ni ile kanuni ya manufaa ya wote (common good) na kwa
sababu hiyo lipo pendekezo la kuwepo kwa haki miongoni mwa vizazi vyote juu ya
masuala ya matumizi ya kimazingira.
Kubwa
la msingi hapa ni ile haja ya kukubali ukweli kuwa athari za uharibifu wa
mazingira hasa juu ya ekolojia ya utamaduni zinaanza kuonekana wazi wazi
miongoni mwa jamii mbalimbali na hasa wenyeji wa asili ya maeneo husika.
Swali;
Je ni nini kinapendekezwa kifanyike kukabiliana na kadhia hii?
Kwa
kufuata mtindo wa ona-amua-tenda, sura hii ya tano inaainisha nini na namna ya
hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabili tatizo na changamoto zinazotokana na
kadhia hizi. Humu hatua mbalimbali zimeorodheshwa na kuainishwa.
Si
jambo rahisi lakini inaonesha umuhimu wa kubadilisha matumizi toka
nishati-makaa kuelekea nishati-rejeshi na pengine ijumuishe pia motisha ya
ruzuku kutoka Serikali.
Sura
hii inaendelea kusisitiza haja ya kuwepo makubaliano na sheria za kimataifa juu
ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, bayoanuai na bahari. Pia
inatahadharisha matumizi mabaya ya vocha-ukaa (carbon credits).
Labda
tuseme kwa ufupi tu kuwa sura hii inakazia juu ya majadiliano juu ya mazingira,
majadiliano juu ya sera mpya za kieneo, kitaifa, kikanda na kimataifa juu ya
mambo haya, majadiliano na uwazi katika kutoa maamuzi yahusuyo mambo
yanayosababisha na kutokana na kadhia hizi.
Katika
kukidhi haja na mahitaji ya kiutu, siasa na uchumi vinapaswa kutiliwa maanani
pamoja na dini vilevile. Hapana shaka umuhimu wa dini kujadiliana na sayansi
umesistizwa pia.
Swali:
Ni ipi nafasi ya elimu ya mazingira na tasaufi (kiroho) katika juhudi zote hizi
zinazopendekezwa?
Ensikliko
inasisitiza haja ya kubadilisha mitindo yetu ya maisha na kuwa na mitindo mipya
kwani mitindo iliyopo ndio imechangia aina hii ya ‘ulaji’ uliopelekea kadhia
zinazotukumba. Walaji wanapaswa kufanya ulaji wenye kiasi, unaozuia upotevu wa
vitu na mali.
Watu
wanapaswa waelimishwe juu ya ‘agano’ kati ya utu na mazingira. Pamoja na kuwepo
kwa upendo wa kiraia na kisiasa, mahusiano kati ya viumbe yanapaswa pia
kusisitizwa. Ama kwa hakika hata nafasi ya viumbe wengine nao si budi ijaliwe
pia kwani lengo la kuwepo kwao si kwa ajili ya mwanadamu tu bali ni zaidi ya
hapo.
Kwa
namna ya pekee kabisa tunakumbushwa kufikiria masuala ya kimazingira zaidi ya
jua, yaani tusiishie kufikiria kuwa jua ndio chanzo na mwisho wa maisha hapa
duniani.
Swali:
Je kuna jingine lolote unaloweza kuwaambia wasomaji wetu?
Yapo
mengi ya kusema kwani matatizo yanayoendana hayapungui vilevile. Labda niliseme
hili moja hapa kuwa, Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
aliyemaliza muda wake Dkt Mohamed Gharib Bilal, wakati wa uzinduzi wa chuo
kikuu kishiriki cha Marian kule Bagamoyo alituambia kuwa wakati mmoja
alipomtembelea Baba Mtakatifu Fransisko, papa alimwambia haya kuhusu uharibifu
wa mazingira:
kwamba
Mungu husamehe, mwanadamu husahau, lakini katu mazingira hayasahau na wala
hayasamehi! Hivyo basi kila ‘ovu’ tuliongezalo kwenye mazingira linasababisha
madhara makubwa kabisa, kwa namna yoyote ile tutalilipia tu!
Swali:
Ni nini wito wako juu ya yote haya?
Kwa
kutumia maneno ya Julius Kambarage Nyerere, tuchukue hatua sasa wakati ndio huu
na sio vinginevyo. Hivi karibuni taasisi za Umoja wa Mataifa zimetoa angalizo
kuwa kwa takwimu zilivyo sasa baadae mwakani duniani zitafikia rekodi ambayo
haijafikiwa kabla na mbaya zaidi hiyo zitavuka viwango vinavyoweza kuzuilika
tena! Ndo maana tunasema wakati ndio huu tukiukosa baasi tena!
Comments
Post a Comment